Jalada kesi ya wizi wa shehena ya mafuta lipo kwa DPP

Muktasari:
- Washtakiwa katika kesi hiyo wanadaiwa kuiba mafuta aina ya dizeli na petroli lita 9.9 milioni, mali ya kampuni ya mafuta ya Tiper yenye thamani ya zaidi ya Sh26 bilioni.
Dar es Salaam. Jalada la kesi ya wizi wa mafuta katika visima vya Kimataifa ya Kuhifadhi Mafuta, Tiper Tanzania Ltd (Tiper), inayowakabili washtakiwa wanane, lipo ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kwa ajili ya kupitiwa na kutolewa uamuzi.
Jalada hilo limepelekwa ofisi ya DPP, baada ya kutoka Polisi.
Washtakiwa katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi ni aliyekuwa dereva wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Tino Ndekela, mfanyabiashara Fikiri Kidevu; Amani Yamba, Mselem Abdallah , Kika Sanguti, Twaha Salum, Gaudence Shayo na Hamisi Hamisi.
Kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 20 yakiwemo ya kutakatisha fedha na wizi wa mafuta ya Petroli na dizeli zaidi ya lita 9.9 milioni na kuisababishia hasara kampuni ya Tiper ya zaidi ya Sh26 bilioni.
Hayo yameelewa leo Jumatatu Juni 30, 2025 kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na wakili wa Serikali, Titus Aron, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
"Jalada la kesi hii lipo ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kwa ajili ya kupitiwa na kutolewa uamuzi ili iweze kujulikana iwapo upelelezi wake umekamilika au laa, kwa sababu hiyo tunaomba Mahakama yako itupangie tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa," amesema Aron.
Hakimu Nyaki baada ya kusikiliza hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 14, 2025 na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili kutokuwa na dhamana kisheria.
Katika mashtaka yanayowakabili, mawili ni ya uharibifu wa mali wanayodaiwa kutenda kati ya Januari Mosi, 2019 na Desemba 31, 2022 eneo la Tungi, Kigamboni, wakidaiwa kuharibu bomba la kusafirishia mafuta aina ya petroli na dizeli mali ya kampuni ya Tiper.
Pia washtakiwa hao, wanakabiliwa na mashitaka 16 ya wizi wa mafuta wakidaiwa kuiba lita 3,599,458 za mafuta ya aina ya petroli na lita 6,392,356 za mafuta ya dizeli yaliyokuwa yakishushwa kutoka katika meli yakipitishwa katika visima vya kampuni hiyo ya Tiper.
Vilevile, wanakabiliwa na shitaka la kuisababishia kampuni hiyo ya Tiper hasara ya zaidi ya Sh26.01 bilioni, wakidaiwa kutenda kosa hilo tarehe hizohizo eneo la Tungi, Kigamboni, Dar es Salaam.
Washtakiwa hao pia wanakabiliwa na shitaka moja la kutakatisha fedha zaidi ya Sh20.73 bilioni, kosa wanalodaiwa kulitenda katika tarehe hizo na eneo hilo, huku wakijua zilitokana na kosa tangulizi la wizi.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo, Oktoba 22, 2024 na kusomewa mashitaka yanayowakabili.