Kesi ya Ukahaba: Shahidi adai washtakiwa walipewa vijora wavae wakiwa kituoni

Baadhi ya wanawake wanaotuhumiwa kujihusisha na biashara ya ukahaba wakitoka katika Mahakama ya Sokoine jijini Dar es Salaam. Picha na Mpiga picha Wetu
Dar es Salaam. Shahidi wa tano wa upande wa mashtaka katika kesi ya kujihusisha na vitendo vya ukahaba inayowakabili washtakiwa watano, ameieleza Mahakama jinsi wadada hao walivyopewa vijora wavae na ndugu zao baada ya kufikishwa kituo cha Polisi Mburahati jijini Dar es Salaam wakiwa nusu uchi.
Shahidi huyo ambaye ni askari Polisi mwenye namba F 1379 Sajent Radhamani (47) kutoka Kituo cha Mburahati, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive, Dar es Salaam leo Ijumaa, Julai 12, 2024 wakati akitoa ushahidi wake, mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Lugano Kasebele.
Amedai washtakiwa hao walivyofikishwa polisi walikuwa wameziba sehemu ya matiti na shehemu kiuno, huku sehemu nyingine ya miili yao, ikiwa wazi (yaani haina nguo).
Washtakiwa katika kesi hiyo ya jinai namba 17277 ya mwaka 2024 ni Mariam Yusufu Mkinde (25) mkazi wa Magomeni, Mwazani Nassoro (25), mkazi wa Kigogo, Mwanaidi Salum (25) mkazi wa Mabibo, Faudhia Hassan (35) mkazi wa Ubungo na Tatu Omary (40) mkazi wa Ubungo.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka moja la kufanya vitendo vya aibu mbele ya hadhara kwa ajili ya kufanya umalaya kinyume na kifungu cha 176 (a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 Marejeo ya mwaka 2022.
Akiongozwa kutoa ushahidi wake na jopo la mawakili watano wa upande wa mashtaka wakiongozwa na wakili wa Serikali Mwandamizi, Faraja Ngukah akishirikana na Titus Aaron, Winfrida Ouko, Masua Clement na Cathbert Mbilingi, amedai Juni 17, 2024 saa sita mchana akiwa kazini Kituo cha Polisi Mburahati, liletewe jalada na mkuu wake wa uplelezi ASP Geofrey Rumanyika ambalo lilikuwa linahusu kosa la kufanya vitendo vya ukahaba kinyume na maadili.
"Mheshimiwa hakimu, mimi nilipewa jukumu na mkuu wangu wa kazi kuwahoji washtakiwa hao, lakini wakati wameletwa kituoni pale walikuwa hawana nguo kwani walikuwa wamefunia kifua sehemu ya matiti yao na sehemu ya kiunoni huku sehemu nyingine ya miili yao ilikuwa wazi,” adai Sajent Ramadhani.
“Jalada hilo lilikuwa na washtakiwa sita ambao ni Mariamu Yusuph, Mwanzagi Nassoro, Mwanaidi Salum, Faudhia Hassan, Tatu Omari na Antonie Shemdolwa ambaye aliruka dhamana akiwa polisi,” amedai.
Baada ya kupewa jalada hilo, alifanya mahojiano na washtakiwa hao na walikubali walikamatwa na walieleza walikamatwa sehemu mbalimbali katika eneo la Manzese na Tiptop.
“Pia nilipata maelezo ya mashahidi wa tukio hilo ambao ni Juma Ngedele, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Peter, WP Tunusuru na WP Masaji na baada ya kukamilisha upelelezi, jadala lilipelekwa ofisi ya Taifa ya Mashtaka,” amedai.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo aliweza kuwatambua washtakiwa hao mahakamani hapo kwa kuwashika bega.
Alipoulizwa na upande wa mashtaka kwanini washtakiwa hao wameshtakiwa, amejibu nguo walizovaa ndio zilisababishwa washtakiwe kwa sababu zilikuwa zinaonyesha utupu wao.
“Nguo hizi zilikuwa zimeshika sehemu ya kifuani kwenye matiti tu na sehemu ya kiuno kidogo na sehemu ya kwenye makalio kidogo, huku sehemu nyingine ikiwa wazi,” amedia.
Aliulizwa na upande wa mashtaka nguo hizo ziko wapi? Jibu lake alidai kuwa baada ya wanawake hao kukamatwa walipewa vijora na ndugu zao.
“Nguo hizo hatukuweza kuzileta mahakamani hapa kwa sababu tusingeweza kuwavua nguo zao, maana wangebaki uchi,” amedai.
Pia ameulizwa na upande wa mashtaka, washtakiwa wameshtakiwa kwa sheria ipi?
Shahidi huyo amejibu wameshtakiwa chini ya kifungu cha 176 (a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 Marejeo ya mwaka 2022.
Shahidi huyo baada ya kumaliza kutoa ushahid wake, upande wa utetezi ukiongzowa na wakili Jebra Kambole na Maria Mushi, ulimuuliza maswali shahidi huyo kutokana na ushahidia alioutoa.
Alianza wakili Jebra kumuuliza maswali shahidi huyo na sehemu ya mswali hayo ilikuwa kama ifuatavyo:
Wakili: Shahidi ni sahihi wewe hukuwepo eneo la tukio
Shahidi: Ni sahihi
Wakili: Kuna sheria yoyote inayosimamia mavazi ya nusu uchi?
Shahidi: Ndio
Wakili: Ulisema hapa mahakamani nani aliyevaa nguo gani?
Shahidi: Sikusema
Wakili: Wala hukutaja rangi za nguo, sindio?
Shahidi: Ndio
Wakili: Utakubaliana na mimi, Mahakama na upande wa mashtaka hatujaziona hizo nguo.
Shahidi: Mimi nimeziona
Wakili: Kwenye upelelezi wako ulichukua chochote kutoka kwa washtakiwa hawa?
Shahidi: Sikuchukua chochote
Wakili: Hivyo vijora walivaa saa ngapi?
Shahidi: Wakati nafanya nao mahojiano
Wakili: Kwa hiyo wakati unafanya nao mahojiano, hawakuwa uchi?
Shahidi: Ndio hawakuwa uchi.
Wakili: Utakubaliana na mimi kuwa kwenye uvaaji wa nguo, mahakama iamue kuamini maneno yako au laa?
Shahidi: Yes, iamue
Wakili: Unatamani washtakiwa wafungwe kwa maneno yako?
Shahidi: Mimi sio mahakama.
Wakili: Mahakama iangalie nini?
Shahidi: Iangalie maelezo ya mashahidi
Wakili: Maelezo yako yasizingatiwe?
Shahidi: Yazingatiwe pamoja na ya mashahidi.
Wakili: Lakini wakati ukahaba unafanyika wewe hukuwepoo...eti eee?
Shahidi: Sikuwepo
Wakili: Uliweza kujua ni askari wangapi waliwakamata washtakiwa hawa?
Shahidi: Walikuwa zaidi ya 10
Wakili: Unaweza kufahamu magari ya polisi yalikuwa mangapi?
Shahidi: Mawili.
Wakili: Unaweza kujua nani alipanda gari gani?
Shahidi: Siwezi kujua, maana sikuwepo eneo hilo.
Wakili: Katika askari hao 10, uliweza kujua askari wa kike walikuwa wangapi?
Shahidi: Zaidi ya wanne.
Wakili: Ulifanya nao mahojiano saa ngapi?
Shahidi: Asubuhi, kuanzia saa mbili.
Wakili Jebra baada ya kumaliza kumhoji Sajent Ramdhani, wakili Maria Mushi naye alimuuliza maswali machache kuhusiana na ushahidi aliotoa sehemu ya maswali hayo ilikuwa kama ifuatavyo.
Wakili: Katika ushahidi wako hujatuambia mlalamikaji katika kesi hii ni nani?
Wakili: Ni kweli?
Shahidi: Ni sahihi sijamtaka
Wakili: Suala la kuvaa mavazi yasiwokuwa ya kujisitiri, umezungumzia sheria gani?
Sahidi: Kimya
Wakili: Utakubaliana na mimi kuwa hakuna sheria inayosimamia maadili
Shahidi: Ipo
Wakili: Tutajie
Wakati shahidi akifikiria ni sheria gani, wakili wa upande wa mashtaka, Ngukah alisimama na kumtaka wakili wa utetezi kutomlisha maneno shahidi wao kwa kuwa ameshazungumza
“Mheshimiwa hakimu, upande wa utetezi wamemuuliza shahidi kama kuna sheria inayosimamia maadili na yeye amejibu ipo, sasa wasimlazimishe aitaje wakati yeye sio mwanasheria na hawezi kukariri kila kitu,” amedia Ngukah
Baada ya maelezo hayo, hakimu alielekeza upande wa utetezi kubadilisha namna ya kuuliza swali lao kama wanaona halijajibiwa na shahidi.
Wakili: Mheshimiwa hakimu, polisi wanajua sheria na wapo waliosomewa hivyo ajibu swali.
Shahidi: Ndio tunajua sheria lakini ni kwa ajili ya utendaji wa kazi zetu.
Wakili: Shahidi hujatuambia ni sheria gani inayotoa maana halisi ya ukahaba.
Shahidi: Nimezungumzia kifungu cha 176 (a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 Marejeo ya mwaka 2022.
Wakili: Je hicho kifungu kinatoa maana halisi ya ukahaba?
Shahidi: Ndani ya hicho kifungu kina eleza maana halisi ya ukahaba.
Baada ya kumaliza kuhojiwa Sajenti Ramdhani, hakimu Kasebela ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 24, 2024 itakapoendelea na washtakiwa wapo nje kwa dhamana.