Janabi: Ukipata dalili hizi mwilini shtuka

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi.

Dar es Salaam. Kama unahisi harufu isiyo ya kawaida, unaona vitu viwili viwili, unashindwa kutafuna chakula, basi mtafute mtaalamu kwa kuwa unasumbuliwa na kiharusi (yaani kupooza upande mmoja wa mwili).

Pia, kuhisi kichefuchefu, kuchoka sana, maumivu makali ya kichwa, kushindwa kusoma au kuandika, kupoteza usikivu, kuona mawingu na kuongea vitu visivyoeleweka nazo ni miongoni mwa dalili za mtu anayenyemelewa na kiharusi.

Hayo ni maneno ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi alipokuwa akizungumza jana kuhusu ugonjwa wa kiharusi kupitia mtandao wa kijamii wa hospitali hiyo.

Profesa Janabi alisema mtu hupatwa na ugonjwa baada ya kupoteza fahamu ghafla kutokana na mshipa wa damu uliopo kwenye ubongo upande wa kulia au kushoto kuziba, hivyo kushindwa kuruhusu mzunguko wa damu.

“Damu inaposhindwa kuzunguka husababisha seli ndani ya ubongo kupoteza uhai kutokana na kukosa hewa safi ya oksijeni.

“Unaposikia harufu usiyoielewa ni dalili za kiharusi ambayo inaonyesha kiashiria cha ubongo kuwa na shida, mkianza kuona hivyo viashiria ujue mgonjwa wako amepata kiharusi,” alisema.

Profesa Janabi alisema yapo magonjwa yanayochangia mtu kushambuliwa na kiharusi, ikiwamo shinikizo la juu la damu.

“Kuwa na mafuta mengi mwilini, ugonjwa wa kisukari, kuvuta sigara na uzito kupitiliza ndio sababu kubwa zinazosababisha watu kupata kiharusi,” alisema.

Akizungumzia kisababishi kingine, profesa huyo alisema ni ulaji wa vyakula vyenye sukari nyingi na wanga ambavyo husababisha mwili kubadili vyakula hivyo na kuwa mafuta, na mafuta mengi alisema mwilini ni hatari.


Aina za kiharusi

Akizungumzia aina ya kiharusi, Profesa Janabi alisema kuna kiharusi kitokanacho na mshipa wa damu kwenye ubongo kuziba.

“Hii ni kutokana na kuganda kwa damu hivyo kuzuia upande mwingine kupata damu, jambo linalosababisha seli kufa na katika kila wagonjwa 100 wenye kiharusi, 87 wana aina hii ya kiharusi,” alisema.

Aina nyingine alisema ni kile kinachotokana na mishipa ya damu kwenye ubongo kupasuka na damu kujaa ndani ya ubongo.

“Aina hii ya kiharusi ni hatari zaidi, asilimia 50 ya wagonjwa wake wanafariki palepale au baada ya mwaka mmoja na hali zao zinakuwa mbaya sana,” alisema.


Unachopaswa kujua

Hata hivyo, Profesa huyo alisema mtu akipata kiharusi upande wa kulia anapooza upande wa kushoto na akipata upande wa kushoto anapooza upande wa kulia.

“Utafiti unaonyesha wengi wanaotumia mkono wa kulia wanapata kiharusi upande wa kushoto na wanaotumia mkono wa kushoto wanapata kiharusi upande wa kulia,” alisema Profesa Janabi.


Hali ilivyo

Lakini alisema zaidi ya watu milioni 100 wanaishi na ugonjwa huo duniani mpaka sasa.

Alisema isipokuwa kinachotia wasiwasi ni asilimia 80 ya wagonjwa wa kiharusi wapo nchi zinazoendelea na miongoni mwao ambao ni milioni 15 wapo Afrika.

“Hiyo ina maana katika kila watu wanne mmoja ana kiharusi,” alisema Profesa Janabi.

Alisema asilimia 63 ya wanaopata kiharusi wana umri chini ya miaka 60.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanyika Tanzania mwaka 2010 na kunukuliwa na Wizara ya Afya nchini, Watanzania 95 kati ya 100,000 walioko vijijini wameathirika na kiharusi.

Kwa maeno ya mijini, ni watu 108 kati ya 100,000 ndio wameathirika na kiharusi.

Kwa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), kila sekunde 40 duniani kuna watu wanapata kiharusi na kati yao, watatu hadi wanne hupoteza maisha.


Usifanye haya kwa mwenye kiharusi

Mtaalamu wa tiba kwa njia ya mazoezi, Abdallah Makalla alipotafutwa na gazeti hili azungumzia tatizo hilo, alisema mgonjwa mwenye kiharusi hapaswi kuchuliwa huku akisisitiza kufanya hivyo si jambo sahihi.

Alisema mtu anapopata kiharusi, hatua ya kwanza, misuli yake ya upande ulioathirika hulegea hali inayosababisha uwezo wa mkono kushika au kukunja kupungua.

“Unapomchua kwa sababu hawezi kuongea wala kukupa ishara, huwa inasababisha mhusika kupata maumivu na misuli hukakamaa.

“Mfano upande wa kulia ndio umeathirika, mara nyingi wagonjwa hawa hukunja mkono kuelekea kifua na kiganja ni kama kimekunja ngumi, na wengi wako hivyo hasa ambao hawakupata matibabu mapema au wanakuwa wamechuliwa,” alisema mtaalamu huyo.

Alisema kitendo cha kuchua husababisha mikono kukakamaa, “ndiyo maana tunasema kumchua mgonjwa akiwa katika hali hiyo si salama, bali anapaswa kuwahishwa hospitali akatibiwe na wataalamu.”

Makalla alionya kuwa mtu mwenye kiharusi anaweza kupata ugonjwa huo kwa mara nyingine endapo atatibiwa nyumbani bila kupelekwa hospitali.


Njia ya kuepuka

Naye Dk Rajabu Mlaluko wa Hospitali ya Rufaa kanda ya Mbeya akizungumzia miongoni mwa njia za kuepuka usipate kiharusi, alisema inashauriwa watu wenye magonjwa ya kudumu kama shinikizo la damu, saratani, kisukari na selimundu kutumia dawa kama wanavyoshauriwa na madaktari, pia kuhakikisha wanafika hospitalini kwa uchunguzi kila mara.

“Pia, watu waepuke kuwa na uzito kuliko kawaida. Kupeuka matumizi ya dawa za kulevya kwani kujichoma sindano wakati wa kutumia dawa za kulevya kunaweza kusababisha kiharusi kwa kuwa wakati wa kujichoma sindano mtu anaweza kusukuma hewa kupitia bomba la sindano,” alisema.

Wakati Dk Mlaluko akisema hayo, kwa mujibu wa Wizara ya Afya, ni muhimu kutibu shinikizo la juu la damu, kudhibiti ugonjwa wa sukari na kufanya mazoezi ya mwili walau nusu saa kila siku.

Pia, inasema watu wanapaswa kujiepusha na matumizi ya tumbaku na sigara, kuwa na ulaji unaofaa unaojumuisha mbogamboga, matunda, nafaka zisizokobolewa, karanga na mimea jamii ya kunde na kupunguza ulaji wa nyama nyekundu.

Mambo mengine ya kuepukwa ni matumizi ya chumvi ya mezani isiyopikwa na mafuta, hususan yatokanayo na wanyama.

Naye Dk Isaac Maro kwenye moja ya maandika yake aliyoyachapisha katika gazeti hili, aliwahi kusema miongoni mwa changamoto za kiafya zenye matokeo mabaya zaidi wanazoshuhudia Watanzania kwa sasa ni maradhi yatokanayo na changamoto zinazotokea kwenye mfumo wa damu.

Alisema mifano ya changamoto hizo ni kupanda kupita kiasi kwa shinikizo la damu pamoja na kutanuka kwa moyo.

Dk Maro alisema tatizo hilo husababisha matokeo mengi ya kiafya ambayo huhusisha mifumo mingine kama vile wa fahamu.

Aliyataja maradhi hayo kuwa ni pamoja na kiharusi.

Alisema kiharusi ni tatizo la kiafya linalotokana na hitilafu ambayo imesababisha mzunguko wa damu kwenda kwenye ubongo kushindwa kufanyika.

Inapotokea hitilafu hiyo, ubongo hushindwa kupata hewa safi aina ya oksijeni na virutubisho, hali inayosababisha chembe hai za ubongo kuumia na hatimaye kufa kabisa.

Alisema tatizo la kiharusi huweza kumpata mtu wa jinsia yoyote, lakini inaonekana wanawake hupata zaidi ya wanaume.

“Hii hutegemea sana na uwepo wa maradhi ya shinikizo la juu la damu. Wenye matatizo ya shinikizo la juu la damu huwa kwenye hatari zaidi ya kupata tatizo hili la damu kuliko wale ambao hawana,” alisema Dk Maro.

Alisema watu wasiofanya mazoezi ya mwili na viungo au kwa jumla wasioishi maisha ambayo yanachochea mwili kujijenga, huwa kwenye hatari zaidi ya kupata tatizo la kiharusi hata kama umri wao ni mdogo.

Aliwataja wengine walio katika hatari ya kupata ugonjwa huo ni wenye maradhi yanayoathiri mfumo wa damu, wenye maradhi ya kuambukiza kwa mfano wanaoishi na virusi vya Ukimwi (VVU), wanaokunywa pombe kwa wingi, watumiaji wa dawa za kulevya na kuwepo kwa mtu mwenye historia ya kiharusi katika familia.

Hata hivyo, utafiti unaonyesha watu wenye umri wa zaidi ya miaka 50 huwa kwenye hatari zaidi ya kupata kiharusi ikilinganishwa na watu wenye umri mdogo.