Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Je, kuna uhusiano wa maumivu ya mgongo, kujifungua kwa upasuaji

Dar es Salaam. Simulizi ya Shani Mwalimu na Rukia Mzee kuhusu maumivu wanayopitia ya mgongo na kiuno baada ya kujifungua kwa njia ya upasuaji inafanana.

Shani, mkazi wa jijini Arusha, anasema alipoambiwa atajifungua kwa upasuaji, waliopitia hali hiyo walimng’ata sikio wakimwambia ajiandae kuumwa mgongo na kiuno kwa kuwa sindano atakayochomwa kwenye uti wa mgongo ndiyo itakayosababisha hali hiyo.

“Kweli nahisi maumivu ya mara kwa mara, wakati mwingine nahisi mgongo unawaka moto kama vile ndiyo nachomwa ile sindano,” anasema Shani akishadidia tahadhari aliyopewa na kinachomsibu sasa.

Rukia, mkazi wa Madale jijini Dar es Salaam, anasema hupata maumivu ya kiuno, hasa pale anapobeba vitu vizito na kuna wakati hushindwa kukaa.

“Tangu nimefanyiwa upasuaji wa mtoto wa kwanza na baadaye wa pili nilijifunza kuacha kubeba vitu vizito na ikilazimika, basi nitapunguza kiwe nusu ili nisipate madhara,” anasema Rukia.

Simulizi hizi ni za kawaida kwa kinamama, kila mmoja akisimulia anavyohisi maumivu anayopitia kutokana na kile anachoamini kimesababishwa na upasuaji.

Kwa mujibu wa wataalamu hao, maneno hayo ni hisia tu na upotoshaji unaofanywa mtaani.


Chanzo cha maumivu

Goodluck Lema, daktari bingwa wa magonjwa ya mgongo na ubongo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili -Mlongazila, anasema yapo mambo mbalimbali yanayosababisha kinamama kupata maumivu hayo.

Dk Lema anasema mama anapokuwa mjamzito huongezeka uzito kwa mbele na wengine hupinda mgongo, hali inayoweza kuendelea hadi anapojifungua ingawa siyo wote hupitia hali hiyo.

Anasema kwa wanaopitia hali hiyo maumivu ya mgongo na kiuno ni jambo la kawaida na huisha baada ya kujifungua.

Dk Lema anasema hakuna utafiti uliofanywa kwenye eneo hilo na kubaini uhusiano kati ya kufanyiwa upasuaji na kuumwa mgongo na kiuno.

Anasema uwezekano mkubwa katika hilo upo katika chanzo cha kufanyika upasuaji ambacho chaweza kuwa mtoto mkubwa, hivyo kurudi kwenye sababu ya uzito kuzidi mbele wakati wa ukuaji wa mimba.

“Mfano, watu walikuwa wanajiuliza wanywa kahawa kijiweni wana uhusiano gani katika kupata ugonjwa wa mapafu, wakati kahawa haisababishi hayo.

“Hapa ukweli ni kwamba, wanapokaa kwenye vijiwe vile kuna wanaovuta sigara, hivyo moshi kwa namna moja au nyingine wanauvuta pasipo wao kujua na kuja kupata ugonjwa wa mapafu baadaye,” anasema Dk Lema.


Nini kifanyike

Dk Lema anashauri ni muhimu mama katika kipindi cha ujauzito kuhakikisha anafanya mazoezi hata madogo madogo.

Anasema ni vyema kupata ushauri kwa madaktari wa mazoezi tiba kwa kuwa yanayofanyika ni tofauti na ya wasio wajawazito.

Pia, anashauri kufuatwa utaratibu wa unyonyeshaji akisema baadhi ya kinamama kutokana na kutumia muda mrefu kunyonyesha wakiwa wamekaa hupata matatizo ya mgongo.

“Katika kunyonyesha kuna namna ya ukaaji, wataalamu wa masuala ya wanawake hutoa elimu ya njia bora za unyonyeshaji, hivyo ni muhimu kuzingatia.

“Nasema hivi kwa kuwa wengi wanaokumbana na matatizo haya ni wale ambao watoto wao ni wa kwanza, hivyo hawajui namna ya kumnyonyesha mtoto na kukaa mikao ambayo siyo,” anasema.

Anawashauri wenye maumivu hayo kwenda hospitali ambako watapimwa kubaini tatizo na kupata tiba sahihi.

“Jamii inapaswa kujua kila mtu kaumbwa kivyake na ana namna ya kukabiliana na mazingira. Kuna ambaye akibeba ujauzito anapata shida ya mifupa kutokana na umbile lake dogo, lakini kuna mwingine wa umbo dogo ana uwezo mkubwa tu wa kusukuma mtoto.

“Vilevile kuna walio na miili mikubwa lakini wanashindwa kusukuma mtoto, baadhi ni kutokana na maisha waliyokuwa wanaishi, ikiwamo kutofanya mazoezi. Hivyo huwezi kuwaweka hawa kwenye kapu moja,” anasema.


Sababu nyingine

Dk Lema anasema yapo matatizo kadhaa yanayosababisha maumivu ya mgongo mbali ya yanayowapata wajawazito.

Sababu hizo anasema ni kukaa muda mrefu, kusimama, kukaa vibaya kwenye kiti unachotumia ofisini, kufanya kazi kwenye mitetemo muda mrefu na wakati mwingine huchangiwa na uvaaji wa viatu usio sahihi.


Kwa nini upasuaji

Jane Muzo, daktari bingwa wa magonjwa ya kina mama na masuala ya ujauzito katika Hospitali ya Aga Khan, anasema zipo sababu mbalimbali zinazosababisha kujifungua kwa njia ya upasuaji.

Sababu za msingi anasema ni mama tangu alipohudhuria kliniki kuonekana ana viashiria hatarishi vya kuweza kujifungua kwa njia ya kawaida.

Nyingine ni mtoto kuwa na uzito mkubwa kupitiliza, akisema wapo wanaofika hadi kilo tano, hivyo kuwa vigumu mama kujifungua kwa njia ya kawaida.

“Pia, kuna mtoto kutoka kwa njia ambayo siyo sahihi wakati wa kujifungua; kwa ama kutanguliza mguu, mkono au makalio. Hapo lazima madaktari wamsaidie huyu mama, ikiwemo kumfanyia upasuaji.

“Lakini kuna mama kupatwa shida akiwa katika hali ya kujifungua, ikiwamo shinikizo la damu au kifafa cha mimba ambacho husababisha kupoteza fahamu, hivyo kushindwa kusukuma mtoto,” anasema Dk Muzo.

Pia, anasema wapo ambao awali walishazaa kwa njia ya upasuaji, ambao ni nadra kwa mara nyingine kujifungua kwa njia ya kawaida.

Hata hivyo, anasema kuna sababu ambazo siyo za msingi za kujifungua kwa upasuaji.

Anazitaja kuwa ni woga wa mama kujifungua kawaida kwa kusikiliza simulizi mtaani kuhusu maumivu atakayopitia.

Dk Muzo anasema wengine wana imani wakijifungua kawaida maeneo ya siri yataharibika kwa kuwa makubwa, jambo analosema halina ukweli wowote.