Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kijue chanzo mimba kufikisha miezi 11

Dar es Salaam. Kardinali mteule Protase Rugambwa alipozungumzia historia yake baada ya uteuzi alisema wataalamu wa afya walieleza alizaliwa akiwa na ngozi ya ajabu.

“Wataalamu wa baiolojia wanaweza kuona ni vigumu, lakini hata wataalamu kipindi hicho walisema nilizaliwa na ngozi ya ajabu ajabu,” alisema Kardinali mteule Rugambwa.

Hali hiyo ilitokea miaka 63 iliyopita, aliposubiriwa azaliwe baada ya kukaa tumboni kwa miezi 11 tofauti na ilivyozoeleka ujauzito ni miezi tisa.

Kauli ya Kardinali mteule Rugambwa, aliyeteuliwa na Baba Mtakatifu Fransisko, Julai 9, mwaka huu imeibua hisia za baadhi ya watu.

Wapo waliosema wamewahi kusikia mtu kabeba ujauzito kwa miezi 11 na wengine kushuhudia tukio hilo. Lakini je, kuna ukweli wowote katika hilo?

Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama, Vincent Tarimo, alipoulizwa swali hilo na Mwananchi alisema, “inawezekana kuzaliwa na miezi 11 na vilevile ukibatika kuzaliwa na miezi 11 ni kawaida ngozi kuwa mbaya kwa kuwa (mtoto) anakuwa amedumaa na ngozi inakuwa imenyauka. Mtoto anakuwa kama mzee.”

Dk Tarimo, anayefanya kazi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili anasema sababu zipo nyingi, “inawezekana mtoto mkubwa kuliko nyonga, nyonga ndogo kuliko mtoto, hutokea bila sababu, kuna uvimbe ‘fibroid’ chini unazuia mtoto asishuke, na mama hakumbuki vizuri siku zake.”

Daktari mwingine wa magonjwa ya kinamama na uzazi wa Hospitali ya Rufaa ya Morogoro, Daniel Nkungu anasema kitaalamu mtoto huzaliwa kati ya wiki ya 37 hadi 40.

“Anaweza kufikisha hadi wiki ya 43, akizidi hapo uwezekano wa kufia tumboni ni mkubwa. Nakosa sayansi ya kuisimamia mimba ya miezi 11, lakini kitaalamu kuna vitu viwili; aidha mimba ilitungwa juu ya uvimbe au mama alikosa taarifa sahihi za lini alishika ujauzito.

“Kuna mwingine anaweza kuwa na uvimbe au mafuta, akiona tumbo kubwa anahisi ni mimba, kumbe ni uvimbe, halafu wakati uvimbe ukiendelea kukua juu yake akabeba mimba, huwa tunapokea kesi za mimba kufika miezi 11 lakini ukichunguza inakuwa ni tofauti.

“Kitaalamu mtoto akipitiliza umri wa mimba, kondo la nyuma haliwezi kumtosha kumlisha akiwa tumboni, atasinyaa au kufia tumboni. Kifupi mimba ikifikisha wiki ya 34 mtoto anakuwa amekomaa, si njiti. Akifika wiki ya 37 hadi 42 anazaliwa, baada ya hapo tunasema mtoto anazeekea tumboni,” anasema.


Mimba juu ya uvimbe

Dk Nkungu anasema kuna uwezekano mtu mwenye uvimbe tumboni akajifungua salama.

“Itategemea uvimbe ulipo, kuna maeneo yanaruhusu mimba ikae na ikue hadi kujifungua na mengine hayaruhusu. Inategemea na kondo la nyuma, uvimbe ukikaa hapo ukizidi kukomaa kuna changamoto ya kukosa damu ya kutosha, lakini kama uko mbali mimba inakua vizuri,” anasema.

Baada ya Kardinali mteule Rugambwa kueleza kuhusu ngozi yake alipozaliwa kuwa ya ajabu, baadhi ya watu walisema wanaamini mtoto akipitiliza siku za kuzaliwa viungo vyake huwa vimeanza kukomaa na kuwa kama mtoto ambaye tayari amefikisha mwezi mmoja au miwili duniani.

Dk Nkungu anasema mwonekano tofauti wa mtoto hutegemea mambo kadhaa.

“Kama hakupata shida tumboni atatoka vizuri, lakini wapo wanaozaliwa ngozi zao zimechafuka au kusinyaa. Mtoto akijisaidia tumboni au kama mama ana shida ya kondo la nyuma, atazaliwa amechafuka au ngozi imesinyaa.

“Mama asipopata chakula vizuri au mtoto akikaa sana tumboni atazaliwa amesinyaa kwa kuwa kondo haliwezi kumlisha vizuri.”

Kwa upande wake, daktari wa magonjwa ya kinamama na uzazi wa Hospitali ya Salaaman iliyopo Manispaa ya Temeke, Abdul Mkeyenge anasema mimba zilizopitiliza umri hutokea na kuna wakati hufikia hadi miezi 12.

“Lakini madhara yake ni makubwa, unaweza kukuta mtoto amefia tumboni hivyo muda wa kujifungua unapofika hajifungui. Mjamzito akiwa anahudhuria kliniki, ikipita wiki ya 42, unaanza kumualati,” anasema Dk Mkeyenge.

Anasema kuna mambo mengi yanayosababisha ujauzito kupitiliza, ingawa wapo wengine wanapoulizwa mara ya mwisho kupata hedhi ilikuwa lini hawakumbuki na kutaja tofauti.

“Anakuwa anaotea, hivyo unapompigia hesabu ya siku ya kujifungua kama ni Septemba, inakuwa ni mbele japo akifanya ultrasound kipimo kitaonyesha,” anasema Dk Mkeyenge.

“Kuna mazingira hatarishi yanayosababisha kupitiliza, mwingine mtoto anakuwa na kichwa kikubwa, lakini pia kikawaida mtoto akiwa tumboni anazungukwa na maji, hivyo kuna wengine yanakuwa machache nayo ni hatarishi.

“Wapo wengine, mtoto anafia tumboni muda wa kujifungua unafika mama hajifungui, lakini pia wapo wengine mtoto wa kwanza anachelewa kujifungua na wengine historia ya familia yao iko hivyo na watu wanene kupitiliza pia.

“Japokuwa wapo wanaochelewa wakazaliwa vizuri, haitakiwi kwa kuwa ukipitiliza sana kondo ambalo hupitisha hewa na chakula mtoto akiwa tumboni likaanza kuharibika, atakosa mahitaji yake na itatokea atapoteza uhai tumboni na hata mjamzito kupata kifafa cha mimba,” anasema Dk Mkeyenge.


Kuhusu kujifungua

Dk Nkungu anasema kwa mama anayejifungua kwa operesheni, wanapanga wiki ya 37 ajifungue kwa kuwa mtoto anakuwa ameshakomaa, na hata akiendelea kukaa tumboni hakuna anachonufaika nacho na akizidi kuwa tumboni, uwezekano wa kufariki dunia ni mkubwa.

Kwa wanaojifungua kawaida anasema inategemea, wapo wanaowahi kuanzia wiki ya 38 na wengine hufikia ya 42.


Mtoto kuzaliwa njiti

Ukiacha mimba kufikisha miezi 11, tukio ambalo wataalamu wanasema ni nadra kutokea, mtoto kuzaliwa kabla ya miezi tisa hujitokeza mara nyingi na wanaopata huduma stahiki huwa na afya njema, ingawa wapo wanaopoteza maisha.

Takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha watoto njiti 210,000 huzaliwa kila mwaka nchini, huku 13,900 kati yao hufariki dunia kwa kukosa huduma wakiwa hospitalini.

Pia, zinaonyesha Tanzania ni nchi ya 12 kwa kuwa na idadi kubwa ya watoto njiti duniani.

Ripoti iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika Linalohudumia Watoto Duniani (Unicef) ya mwaka 2020 inaonyesha kati ya watoto 10 wanaozaliwa, mmoja ni njiti na kila sekunde 40 mtoto mmoja kati ya hao hufariki dunia.

Dk Nkungu anasema mtoto njiti ni anayezaliwa chini ya wiki ya 34 na juu ya wiki ya 28, hiyo ni kwa Tanzania, lakini kwa baadhi ya nchi mtoto njiti anaenda hadi chini ya wiki ya 22.