Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Upandikizaji mimba MNH kuanza karibuni

Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) inatarajia kuanza huduma za upandikizaji mimba kupitia maabara mapema mwaka huu, baada ya mchakato muhimu kukamilika.

Huduma hiyo iitwayo In Vitro Fertilization (IVF), inaanzishwa Novemba mwaka huu, ikiwa ni takribani miaka mitano tangu kuanza kwa maandalizi mwaka 2018, yaliyohusisha kusomesha wataalamu, jengo na ununuzi wa vifaa.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Mohammed Janabi wakati wa mahojiano maalumu aliyoyafanya na Mwananchi mwishoni mwa wiki.

“Nilipoingia Muhimbili nilikuta mchakato ukiendelea, Mei mwaka huu tumelipa Sh1 bilioni kununua vifaa ambavyo vinatoka India kwenye kampuni inayoitwa Shibane.

“Siku nne au tano zilizopita wameshavipakia, tayari viko njiani na leo asubuhi tulikuwa na mafundi wanafanya marekebisho ya mwisho ya jengo litakalotumika, kazi ambayo itawachukua wiki nne. Jengo lipo tayari, tunafanya marekebisho ya rangi, furniture (samani) na kila kitu,” alisema.

Kwa mujibu wa Profesa Janabi, baadhi ya wataalamu ambao walikwenda kusoma wamesharudi na kuna wengine watatu mabingwa watakaorudi mwishoni mwa mwaka.

Alisema mpaka vifaa kufika nchini mwezi ujao, wanategemea kutakuwa na kazi kubwa ya kuvisimika.

“Huduma ya upandikizaji wa mimba ni kubwa na inahitaji utayarishaji hasa, hivyo kutakuwa na kazi mbalimbali zitafanyika zikiwemo za kusimika mitambo au vifaa na kuvikagua.

“Lakini jambo moja ambalo nina uhakika nalo, mwisho wa mwaka huu kufikia Novemba tutakuwa tumeanza kliniki na tutaanza upimaji na inshaalah Mungu akipenda, mapema mwakani tutakuwa tumeshaanza kupandikiza,” alisema.

Profesa Janabi alisema mpaka sasa Muhimbili ipo kwenye mchakato wa kusajili wataalamu na kuwaandaa wale waliopata mafunzo kuwa tayari.
Alisema wanaye daktari mmoja kutoka Sudan ya Kusini ambaye alisoma Muhas hapa nchini na baadaye akaenda akasoma shahada yake ya pili Uingereza, aliyemtaja kwa jina moja la Dk Garang, kwamba naye atafika kuungana na wenzake.

“Tunaye Dk Ngarina Matilda ambaye ndiye mkuu wa IVF yupo nasi Muhimbili, kuna madaktari wanasoma nje hivi sasa na Dk Lilian Mnabwiru amerudi ana kama wiki mbili sasa tangu ahitimu masomo yake,” alisema.
Profesa Janabi alisema mpaka sasa anaona mwanga mkubwa kwamba huduma ya upandikizaji mimba itakuwa bora kutokana na vifaa vya kisasa ambavyo Serikali imevinunua.

Alisema katika mkataba wa manunuzi ya hivyo vifaa, wataalamu kutoka India watakuwa bega kwa bega na wenzao nchini katika hatua za awali kwa kuwa vifaa hivyo vimenunuliwa katika kampuni kubwa nchini India.
“Ni huduma itakayokuwa kubwa kuliko mahali popote hapa ndani ya nchi. Kwa sasa tunafanya marekebisho, kutakuwa na vyumba vya kinababa watakaokuja kuchangia mbegu kwa ajili ya wenza wao, kwa hiyo hospitali inaendelea na haya maandalizi ni muhimu sana kwani upandikizaji mimba ni huduma nyeti inayohitahji utaalamu wa hali ya juu,” alisema.
 

Ukubwa wa tatizo

Profesa Janabi alisema huduma hiyo ambayo itapatikana Muhimbili tawi la Upanga, itasaidia wahitaji wengi kwa kuwa takwimu za wanaohitaji huduma inazidi kukua siku hadi siku.

“Wagonjwa tunaowaona hapa katika kliniki zetu za kinamama Muhimbili, inaonyesha kuwa asilimia 40 ya kina mama wanaokuja wanahitaji huduma ya kusaidiwa kupata watoto.
“Kati yao ukiwachambua, kuna wengine unakuta ni vitu vya kawaida vya kurekebisha bila kuhitaji upandikizaji, lakini asilimia 20 wanaweza kuwa wanahitaji huduma ya IVF,” alisema Profesa Janabi.
Kwa mujibu wa Profesa Janabi, huduma hiyo aitasaidia wahitaji wengi kwa kuwa takwimu zinaonyesha wanaohitaji huduma inazidi kukua siku baada ya siku.

“Kati ya akinamama wanaopewa rufaa kuja Muhimbili kwa ajili ya matibabu ya huduma za uzazi asilimia 40 wanakuja kuhitaji huduma ya kusaidiwa kupata mtoto na tunapowapima na wenza, tunaona asilimia 50 changamoto wanazo wanawake na asilimia 50 wanaume.
 

Sheria muhimu

Kutokana na unyeti wa huduma pamoja na mambo yanayowezekana kisheria katika uchangiaji wa mbegu, Profesa Janabi alisema katika hatua za awali watataka baba atoe mbegu.

“Kwa kadri siku zinavyokwenda pindi tutakapopata uzoefu na kila kitu kama sheria zinavyosema, itabidi sheria zingine zipite bungeni au kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali,” alisema.
 

Kuhusu gharama

Alipoulizwa kuhusu gharama za upandikizaji, Profesa Janabi alisema “Gharama kubwa hadi sasa ni upatikanaji wa vifaa, siwezi kukisia tutatoza kiasi gani. Bado tunafanya mazungumzo na bima, Serikali inaweza kuchangia na kuna wale ambao watalipia huduma kwa maana ya fedha taslimu.

“Sisemi kwamba ni mapema sana, lakini mazungumzo haya ya dawa na vitendea kazi ndiyo vitafanya maamuzi mambo yaweje, ndiyo tutakavyoweza kupanga bei ikoje.”

Hata hivyo alisema kwa sasa kinamama na kinababa waliokuwa na changamoto ya upandikizaji mimba, Muhimbili itakuwa kimbilio lao hasa katika suala ya gharama, kwa kuwa ni hospitali ya Serikali na ipo kwa ajili ya kutoa huduma kwa Watanzania na si kwa ajili ya faida.
 

Hali ilivyo nchini

Hapa nchini ni vituo viwili pekee mpaka sasa vinavyotoa huduma ya upandikizaji mimba, ambavyo ni vituo binafsi.

Hivi karibuni gazeti hili liliripoti kuwa zaidi ya wanawake 500 wamepata watoto kwa njia ya upandikizaji kupitia Kituo cha Huduma ya Uzazi na Upandikizaji Mimba cha Avintacare Medical Center kilichopo jijini Arusha.

Vilevile, kufikia Februari mwaka huu, watu 600 walijikuwa wametokeza kutafuta huduma kama hiyo tangu kuanzishwa kwa kituo kingine cha huduma hiyo cha Hubert Kairuki kilichopo jijini Dar es Salaam.

Mtendaji Mkuu wa Hubert Kairuki Hospital Green IVF, Dk Clementina Kairuki alisema wakati wa uzinduzi Machi mwaka huu kati ya hao 600 walipochunguzwa ilibainika 45 kati yao walihitaji huduma hiyo na miongoni mwao 35 walipata ujauzito.

Kuhusu gharama za huduma hiyo, Dk Clementina alisema inagharimu kati ya Sh13 milioni hadi Sh15 milioni kuwezesha mtu kufanyiwa upandikizaji na hiyo inachangiwa na kutegemea vifaa na dawa kutoka nje ya nchi.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema alipotembelea kituo hicho kuwa tatizo la ugumba bado ni kubwa nchini lakini mpaka sasa hakuna takwimu rasmi za kitaifa, lakini utafiti mdogo uliofanyika unaonyesha asilimia 30 ya watu wana tatizo la ugumba.

Pia aligusia ughali wa gharama ya huduma hiyo, “Serikali inajipanga kurejea upya gharama za upandikizaji wa mimba kwa wananchi wenye matatizo ya uzazi na kutopata watoto ili kuwapunguzia mzigo wa gharama kubwa pia tunahamasisha watu wajiunge na bima za afya.”
 

Ukubwa wa tatizo

Naomi John (37) ni miongoni mwa wanawake wanaosubiri huduma ya kupata matibabu hayo kwa usaidizi wa Serikali kutokana na kukosa fedha za huduma hiyo katika hospitali binafsi kutokana na gharama kuwa juu.

"Mimi na mume wangu tulianza kuhangaika kupata mtoto mwaka 2014, miaka miwili tangu tulipooana mwaka 2012. Nilitumia tiba asili nikachoka baadaye tukaenda Hospitali ya Amana ambako wataalamu walisema lazima nifanyiwe vipimo, matibabu.

"Nimepitia mateso ya kusafishwa kizazi zaidi ya mara nne na baadaye tulipewa rufaa ya Muhimbili. Vipimo zaidi vilifanyika na wakati huo hata mume wangu alipimwa na ikabainika shida ipo kwake. Tangu mwaka 2019 tunasubiri hii huduma labda tutafanikisha iwapo huduma itaanza," alisema Naomi.