Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Gharama upandikizaji mimba mwiba, WHO yaingilia kati

Muktasari:

  • Akielezea mkakati wa Serikali juu ya utoaji wa huduma za upandikizaji mimba kwa wenye uhitaji na kupunguzwa kwa gharama, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Grace Magembe anasema tayari Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila ipo kwenye hatua ya kuanza kutoa huduma hiyo.

Dar es Salaam. Wengi wa watu wanaokabiliwa na matatizo kupata ujauzito hulazimika kutumia gharama kubwa kukabiliana na changamoto hiyo ambayo zaidi huwakumba wanawake.

Kutokana na hali hiyo, watu hao wakati mwingine hulazimika kupata huduma za matibabu ya kupandikiza mimba kwa njia ya In Vitro Fertilization (IVF), ili wafanikiwe kupata watoto.

IVF ni upandikizaji wa kiinitete ndani ya kizazi baada ya uchavushaji wa mayai na mbegu kwenye maabara maalumu. Kwa hali ya kawaida utungaji wa mimba hufanyika ndani ya mwili wa mwanamke katika mfuko wa uzazi.

Inavyofanyika yai na mbegu (kiinitete) umri wa siku mbili hadi nne kimoja au zaidi ya kimoja hupandikizwa ndani ya kizazi kwa kutumia chombo maalum baada ya kizazi cha mwanamke kuandaliwa.

Inaelezwa mafanikio ya IVF kupata ujauzito au mtoto ni kuanzia asilimia 32 kushuka, inategemea na umri na tatizo alilokuwa nalo mwanamke, huku gharama yake ikitajwa kuwa kati ya Sh10 milioni hadi Sh17 milioni kutegemea na hospitali inayotoa huduma hiyo.

Kutokana na ukweli huo, hata ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ilionyesha hitaji la dharura la kuongeza ufikiaji wa huduma ya afya ya uzazi kwa gharama nafuu na huduma bora zaidi kwa wenye uhitaji.

Ripoti hiyo iliyotolewa mwezi uliopita inaonyesha takriban asilimia 17.5 ya watu wazima duniani hukumbwa na matatizo hayo, kiwango ambacho ni sawa na mtu mmoja kati ya sita ulimwenguni ambao wanashindwa kuwa na uwezo wa kuzaa.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus amekaririwa akisema, "idadi kubwa ya watu walioathiriwa inaonyesha hitaji la kupanua wigo wa ufikiaji wa huduma ya uzazi na kuhakikisha suala hili haliwekwi kando tena katika utafiti wa afya na katika sera, ili njia salama, bora na za gharama nafuu za kupata uzazi zipatikane kwa wale wanaotafuta.”

Kutokana na gharama za hospitali kuwa juu, baadhi ya watu hulazimika kwenda kwa waganga wa kienyeji kuhakikisha wanafanikisha ndoto yao ya kupata mtoto na wengine hudiriki hata kuiba watoto wa wenzao hospitalini. Ingawa tatizo hili lipo zaidi kwa wanawake, pia wanaume hulipata kutokana na sababu mbalimbali.

Akizungumzia suala hilo, Mtaalamu wa Embrolojia kutoka Hospitali ya Kairuki, George Tryphone anasema tangu walipoanza kutoa huduma hiyo Julai mwaka jana mpaka sasa wamepandikiza wagonjwa 80 na waliofanikiwa kujifungua ni 16, huku wengine wakiwa katika hatua mbalimbali za ujauzito.

Anasema gharama za huduma hiyo zipo juu kutokana na gharama za vifaa, wataalamu pamoja na dawa wanazotumia kwa wenye uhitaji kuuzwa ghali zaidi.

Tunachoiomba Serikali iboreshe mazingira ya upatikanaji wa vifaa tunavyotumia kwenye huduma hii, pia hata tukipata msamaha wa kodi kwenye dawa na vifaa vingine tunavyovitumia vitasaidia kupunguza gharama.

Pia vyuo vianze kutoa taaluma hii ya upandikizaji na hatutakuwa tena na shida na mambo haya," anasema.

Kwa upande wake Mtaalamu wa uzazi kutoka kituo cha Avinta Care kinachojishughulisha na upandikizaji mimba mkoani Arusha, Dk Nicholaus Mazuguni anasema kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita kuanzia mwaka 2019 hadi 2022, wameshawahudumia kinamama zaidi ya 700 na waliofanikiwa kupata watoto ni zaidi ya wanawake 350.

Dk Mazuguni anasema takwimu hizo ni sawa na asilimia 45 ya waliowapatia matibabu, akitaja gharama kutofautiana kati ya mtu na mtu kulingana na aina ya tatizo, lakini uwiano wa gharama ni kati ya Sh10 milioni hadi Sh16 milioni.

“Sababu ya gharama kuwa kubwa ni umri wa mhusika na aina ya tatizo atakalokuwa nalo.

“Tunaiomba Serikali huduma hizi zifungamanishwa na bima ya afya, ili kuwanufaisha wananchi, Serikali ingewezesha wananchi kupata baadhi ya dawa na vipimo ingekuwa vizuri zaidi na isaidie watu wengi zaidi wafungue vituo kama hivi,”anasema.

Pia akizungumza na Mwananchi hivi karibuni alisema, “Mafanikio ya IVF kupata ujauzito au mtoto ni asilimia 32 kushuka, kutegemea umri na tatizo husika. Kati ya wanawake 10 wanaopandikizwa, wawili hadi watatu wanaweza kupata ujauzito.”


Kauli ya Serikali

Akielezea mkakati wa Serikali juu ya utoaji wa huduma za upandikizaji mimba kwa wenye uhitaji na kupunguzwa kwa gharama, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Grace Magembe anasema tayari Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila ipo kwenye hatua ya kuanza kutoa huduma hiyo.

Akizungumzia tatizo hilo hivi karibuni, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema Serikali imejipanga kurejea upya gharama za upandikizaji wa mimba kwa wananchi wenye matatizo ya uzazi na kutopata watoto, ili kuwapunguzia mzigo wa gharama kubwa endapo watajiunga na Bima ya Afya kwa wote.

Waziri Ummy akiwa ametembelea Taasisi ya Kairuki iliyopo Bunju A jijini Dar es Salaam inayotoa huduma ya upandikizaji mimba, alisema tatizo la ugumba bado ni kubwa nchini, ingawa mpaka sasa hakuna takwimu rasmi za kitaifa.

“Ila ulifanyika utafiti mdogo ambao unaonyesha asilimia 30 ya watu wana tatizo la ugumba, huku duniani inakadiriwa kuwa katika kila mahusiano ya wenza wanne, mmoja kati yao anakuwa na tatizo la kupata watoto.

"Tatizo la kutopata watoto lipo pande zote mbili (wanaume na wanawake), lakini jamii yetu inachukulia familia isipopata mtoto basi mwanamke ndiyo anaonekana mwenye tatizo. Naamini uwepo wa kituo hiki utasaidia kuondoa fikra potofu," alisema Waziri Ummy.

Ilielezwa kituo hicho kinatoa huduma hiyo kuanzia Sh13 milioni 13 hadi milioni 17 kutegemea na aina ya huduma inayohitajika.

Serikali tutaendelea kuwaunga mkono na kuhakikisha huduma hizi zinatolewa na kuwafikia wengi. Gharama za upandikizaji ni kubwa, Watanzania wengi hawawezi kumudu,” anasema.

Mzizi wa matatizo

Akifafanua kuhusu hali ya wanandoa au wapenzi kukosa watoto, Dk Rajab Mlaluko kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya anasema kushindwa kupata mtoto kwa kipindi cha miezi sita au mwaka mmoja huku wahusika wakiwa hawatumii njia za uzazi wa mpango ni tatizo.

Yapo mambo mengi yanaweza kusababisha kutokea kwa changamoto hiyo na hata matibabu hutegemea na sababu,” anasema.

Sababu ya matatizo hayo, hususan kwa wanawake yanaelezwa na Dk Hellen Mrina kwamba yanasabishwa na kuziba kwa mirija ya uzazi ambayo huchukua yai likaungane na mbegu, ili apatikane mtoto.

“Kama hakuna mawasiliano kati ya yai na eneo la uzazi yaani mirija kuziba, mawasiliano yatakata kati ya yai na mbegu,” anasema.

Kuziba kwa mirija ya uzazi, daktari huyo anasema kunatokana na maambukizi ya magonjwa ya zinaa, ikiwemo klamedia ambayo mara nyingi mtu anapoambukizwa dalili hukawia kuonekana, hivyo mtu anagundua tatizo tayari likiwa limesababisha athari kubwa mwilini.

Jambo lingine alilotaja Dk Hellen kuchangia tatizo hilo ni hitilafu katika vichocheo vya mwili, yaani homoni.

Anasema tatizo hilo la homoni husababisha mama kutopata siku zake mara kwa mara na mara nyingi tatizo hilo likigundulika mapema na mhusika kupatiwa dawa anaweza kupona na kurejea hali ya kawaida.

Kwa upande wa wanaume, anasema tatizo linaweza kutokea pale ambapo eneo la kutengeneza mbegu hadi eneo la kutolea kushindwa kutoa mbegu za kutosha.

Daktari huyo ambaye ni mtaalamu wa magonjwa ya kina mama Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) anasema upo uwezekano mwanamume akazalisha mbegu za kutosha, lakini zikakosa ubora unaohitajika.

“Pia kama mbegu zenyewe haziwezi kuogelea ni shida nyingine kwa mwanamume,” anasema.

Upungufu wa mbegu kwa mwanamume anaeleza kwamba unaweza kuchangiwa na uvaaji wa nguo zinazobana ambazo hutengeneza joto katika via vya uzazi.

Wakati mwingine hali hiyo huchangiwa na magonjwa yanayotokea ndani ya mwili pamoja na vyakula anavyotumia mhusika.

Akifafanua masuala ya homoni kuchangia changamoto kwenye masuala ya uzazi, Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani ya kihomoni kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili – Mloganzila, Salama Ali anasema kunapotokea tatizo la uzazi ina maana homoni inayohusika na uzazi imepanguka.

“Hali hiyo inapotokea maana yake labda kutakuwa na uvimbe unaogandamiza eneo la kutoa homoni au uvimbe unatoa homoni za ziada kiasi kwamba zinapangua mzunguko mzima wa uzazi, jambo la muhimu homoni inayosababisha hedhi au upevushaji wa mayai kwa ujumla unapanguka na kuleta tatizo kwenye upatikanaji wa mtoto,” anasema.

Dk Salama anasema mwanamke anapopata tatizo lolote linachongia mayai kupanguka na homoni kutozalishwa inapopaswa, huchangia tatizo hilo.

Mambo mengine yanayochangia mvurugiko wa homoni anayotaja Dk Salama ni matumizi ya dawa za wagonjwa wa akili pamoja na mtu kupata msongo wa mawazo.

“Homoni zinapokuwa chini, mfano za kiume kuna matibabu kwa njia ya sindano au kidonge na kwa upande wa wanawake kuna mbadala lakini kwa baadhi si zote,” anaeleza.

Kwa upande wake, Dk Mlaluko akizungumzia matibabu ya maradhi hayo anasema magonjwa hayo kwa wanaume na wanawake yanaweza kusababishwa na matumizi ya mihadarati, sababu za kimaumbile na uzito kupitiliza.

“Tatizo la utasa au ugumba linaweza kutibika kulingana na chanzo chake, inaweza kuwa kwa njia ya dawa au kupandikiza, hivyo watu wenye matatizo haya wafike hospitali kwa ajili ya uchunguzi na matibabu,” anaeleza.


...upandikizaji unavyokuwa

Upandikizaji wa mimba kwa mwanamke hufanyika kupitia kuondolewa kwa yai lake kwenye ovari na kisha kuchavushwa kwa mbegu za mwanaume ndani ya maabara.

Yai linalochavushwa hurejeshwa kwenye tumbo la uzazi wa mwanamke kwa ajili ya kulikuza.

Kwa mujibu wa jarida la kisayansi la The Lancet la nchini Uingereza, karibu watu milioni 48 duniani wanafikisha miaka mitano bila kushika mimba.

Mtaalamu wa magonjwa ya uzazi Hospitali ya Aga Khan, Dk Munawar Kaguta alisema uzazi wa kupandikiza hufanyika baada ya mwanamume na mwanamke kuonekana kuwa na shida.

“Mbegu za kiume zinachukuliwa na yai linatolewa zaidi ya moja kwa kutumia ultra sound. Kuna vifaa vinatumika kuunganisha vitu hivyo na vikishaungana baada ya muda inachaguliwa moja iliyoonekana kuwa sawa anaingiziwa mwanamke kwenye kizazi ikishika mimba inaendelea kama kawaida,"anaeleza.

“Njia hiyo si kwa mwanamke pekee, bali kati ya mwanaume na mwanamke wasio na uwezo wa kupata mtoto, kabla ya hatua ya upandikizaji ni lazima afanyiwe uchunguzi kubaini kama anafaa kufanyiwa tiba hiyo," anasema.

Anasema vitu wanavyoviangalia kabla ya mwanamke kupandikizwa ujauzito ni kama ana uvimbe kwenye kizazi au uwepo wa maji kwenye mirija ya uzazi, matatizo ambayo hupaswa kutibiwa kwanza kabla ya kuanza kwa upandikizaji.

Kwa wanaume, daktari huyo anasema wanaangalia utoshelevu wa mbegu zake na endapo itagundulika ana mbegu chache zaidi, teknolojia ya juu zaidi hutumika, lakini kama hana mbegu kabisa jambo hilo kwake litakuwa gumu kutekelezeka.


Janga zaidi kwa wanawake

Kulingana na chama cha wataalamu wa magonjwa America, kushindwa kupata mtoto kwa mwanamke kunamsababishia kupata aibu, unyanyapaa pamoja na kupitia changamoto ya afya ya akili.

Kulingana na chama hicho, wanaume na wanawake hupitia kiwango cha juu cha msongo wa mawazo na kukosa furaha wakati wa tukio la upandikizaji wa mimba.

 Japo nao wanaume wametajwa kukumbwa tatizo la afya ya akili, lakini changamoto hiyo ipo zaidi kwa wanawake.