Safari ngumu ya kutafuta mtoto kwa upandikizaji
Dar es Salaam. Saa moja usiku ndani ya ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) nikielekea jijini Arusha nikiwa na mawazo lukuki kichwani, hasa kuhusu majibu ya vipimo ambavyo hadi muda huo sikuwa nimevifanya.
Sijui nitafanyiwa tena upasuaji au nitapewa dawa tu na kutumia kisha kuruhusiwa kurejea Dar es Salaam kuendelea na majukumu yangu ya kazi.
Si jambo rahisi, niliwaza bila kuwa na majibu. Ukweli ni nilifanya safari yangu ya Arusha ikiwa imepita miezi minane tangu nifanyiwe upasuaji wa kuondoa uvimbe tumboni pamoja na kutibu tatizo la endometriosis ambalo niligundulika kuwa nalo miaka saba iliyopita.
Endometriosis ni ugonjwa unaohusisha seli zinazofaa kuwa ndani ya mji wa uzazi kuwa nje ya mji huo, hivyo kusababisha maumivu makali wakati wa hedhi na kuathiri mishipa ya uzazi (fallopian tube), uterus na mji wote wa uzazi.
“Hivi mimi nitakuja kupata mtoto wangu kama huyu dada, tazama anavyocheka na kufurahi na mwanaye. Mungu nisaidie na mimi nitimize ndoto yangu,” Niliwaza hayo nilipokuwa nikimwangalia mwanamke mmoja aliyekuwa amekaa mbele yangu akiwa na mtoto wake wa kike ambaye muda wote alikuwa akicheza na kufurahi na mwanaye.
“Dada tumefika KIA una shida yoyote tukuhudumie?” Sauti ya mhudumu wa ndege iliniamsha baada ya kupitiwa na usingizi. “Hamna neno dada niko sawa”, nilimjibu kisha kubeba mkoba wangu na kuanza kutembea kueleka mlangoni akili yangu ikiwaza matibabu.
Hekaheka za usafiri kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kuelekea Arusha katika Hospitali ya Avinta Care sikuzijali sana, nitakutwa na tatizo gani, nitakutana na kina nani na watanihudumiaje, hayo ndio maswali yaliyoteka fikra zangu kwa wakati huo.
Mwanzo wa matumaini
Saa mbili asubuhi nafika Avinta Care iliyopo eneo la Uzunguni jijini Arusha ambayo inatoa huduma na matibabu kwa wanawake walioshindwa kupata mimba kwa njia ya kawaida ambayo inajulikana kama upandikizaji wa mimba (In Vitro Fertilization-IVF) ambako ninakutana na mabinti wawili Joyce Kimario (26) na Elizabeth Leyan (28).
Hawa ni wauguzi ambao licha ya umri wao wanafanya mambo makubwa ambayo aghalabu watu wazima ambao baadhi ya watu wa kada yao wameshindwa. Kwanza wanaijua vyema kazi yao, lakini pia ni wachangamfu waliojaa maneno ya kutia moyo na wenye uwezo mkubwa wa kutoa ushauri wa kitaalamu.
“Usiwe na wasiwasi, hapa tunapokea wanawake wenye matatizo mbalimbali lakini baada ya muda wanapata nafuu na wengi hupata ujauzito,” Ni kauli iliyotoka kwa Joyce baada ya kujitambulisha na kueleza shida yangu.
“Hivi hawa wauguzi wanapumzika muda gani?’’ Nilijiuliza swali hili siku ya 10 baada ya kuanza matibabu katika hospitali hii. Elizabeth na Joyce walikuwa kila eneo, kila jambo kubwa na muhimu walikuwa nyuma yake. Wanakutana na wanawake waliotafuta ujauzito kwa njia ya kawaida kwa muda mrefu bila mafaniko, waliopandikiza mimba lakini hawakufanikiwa, na waliopandikiza mimba na kufanikiwa.
Kazi nyingine kubwa na ngumu niliyoishuhudia ni jinsi ya kubadili fikra za wanaume wagumu juu ya kushiriki kwao katika mchakato wa upandikizaji. Usidhani kwamba ni jambo jepesi baadhi ya wanaume uongozana na wenza wao siku ya kwanza lakini baada ya kusikiliza na kupata ushauri wa mambo wanayotakiwa kufanya katika kufanikisha hilo wengi hutokomea.
Nikiwa katika matibabu nilikutana na mwanamke mmoja (jina linahifadhiwa) na kunieleza kuwa amefanya IVF mara tatu na kipindi chote hicho hakufanikiwa kupata mtoto ila alipofanya mara ya nne alifanikiwa.
Aliwataja Joyce na Elizabeth, akizungumzia waliyomsaidia akikumbuka sindano za siku 10 hadi 12 za matibabu kuandaa mayai hadi kuvuna na sindano za siku 14 baada ya upandikizaji kufanyika.
Pia, nilikutana na mwanamke mwingine ambaye alinieleza kuwa wakati anaanza matibabu licha ya kupata ushirikiano wa mwenza wake mimba haikutunga.
Mwanamke huyo kwa uchungu alinieleza, “alivyoona hivyo (mwenza wake) alikata tamaa na kuniacha mwenyewe. Ni jambo gumu nilibaki napambana, si kitu chepesi kuchoma sindano za kuandaa mayai kwa siku 12, pamoja na kuvuna. Ni jambo linalohitaji ukaribu wa mwenza wako. Kipindi cha kusubiri majibu kwa siku 14 nacho ni kigumu kinahitaji ukaribu sana na Mungu kwani tunaamini uumbaji ni kazi ya Mungu.
Mwanamke huyo ambaye alikuwa anajaribu kupandikiza kwa mara ya pili anasimulia kwamba alifarijika alipokutana na wauguzi hao kwani waliamua kubeba jukumu la ushauri na ukaribu kuanzia utaratibu wa kula, kuishi maisha ya matarajio pamoja na kufuata masharti ili kufanikisha upandikizaji.
Nyakati ngumu
Katika kufuatilia matibabu nilikutana pia na mwanamke mwingine ambaye yeye simulizi yake ya tatizo la kupata ujauzito ilikuwa ya muongo mmoja lakini baada ya kufika hospitalini hapo alifanya mara moja na kufanikiwa. “Nimekaa kwenye ndoa miaka 10 ila nilibahatisha nimefanya mara moja na kufanikiwa kubeba ujauzito na sasa una miezi mitano.”
Hili ndilo ambalo wagonjwa wengi wanaofika katika hospitali hizi wanakuwa na matarajio nalo.
Nilikutana na mwanamke aliyefanya upandikizaji kwa mara ya pili bila mafanikio “mimi hii ni mara ya tatu nafanya ila naamini nitafanikiwa ni safari ndefu ambayo kuna nyakati nakataa tamaa”
Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama na uzazi, Nicholaus Mazunguni kutoka kituo hicho anasema wapo baadhi ya wanawake waliofanya IVF zaidi ya mara moja bila mafanikio na wapo wanaofanya mara moja wakafanikiwa hii inatokana na mwili wa mwanamke namna unavyopokea dawa pamoja na tatizo la mwanamke.
Anasema mafanikio ya IVF kupata ujauzito au mtoto ni kuanzia asilimia 32 kushuka hutegemea umri na tatizo alilokuwa nalo mwanamke huku gharama yake ni kuanzia Sh7 milioni hadi Sh12 milioni.
“Kati ya wanawake 10 wanaofanya kwa mara ya kwanza wanaweza kupata wawili hadi watatu, na hawa ni wanawake wenye matatizo tofauti yanayosababisha washindwe kupata ujauzito kwa njia ya kawaida, nawasisitiza wanawake wanaokuja kufanya matibabu kufuata masharti na kutokukata tamaa.
“Unaporudia matibabu kwa mara ya pili, kila kitu kinaanza upya kuanzia sindano za kupevusha mayai hivyo gharama inategemea na tatizo pia la mwanamke. Tunawashauri wagonjwa huduma ya upandikizaji inavyofanyika ili awe tayari kupokea majibu yoyote bila kukata tamaa” amesema Nicholaus.
Kwa wiki wanahudumia zaidi ya wagonjwa 100 ingawa si wote wanaofika katika kituo hicho hupatiwa huduma ya upandikizaji wengine wakishafanya vipimo hugundulika wanahitaji huduma ya dawa na baada ya muda hupata ujauzito.
Elizabeth anasema ‘”Jambo gumu nililokumbana nalo ni mwanamke mmoja alifanya upandikizaji kwa mara ya kwanza lakini hakufanikiwa kupata ujauzito, wakati nampatia majibu kuwa imeshindikana alilia sana na hata mimi nikajikuta naangua kilio.”
”Ugumu ni kwa zile siku 14 ya kusubiri majibu baada ya kupandikiza kujua kama ni mjamzito ama la. Hapo lazima ujipange utatumia maneno gani kumuelezea mhusika mpaka akuelewe sababu ya mimba kutoshika,’’ amesema Eliza.
Eliza anaelezea mwanamke aliyefanikiwa kubeba ujauzito atatakiwa kuendelea na sindano kila siku kwa kipindi cha miezi mitatu.
Katika maelezo yake Eliza anasema kabla ya kuanza matibabu wanawaeleza ukweli wanawake kwamba wanafanya jukumu lao lakini kwa Mungu ndiye anayepanga ujauzito wa kila mwanamke.
‘’Hii hutusaidia walau wanawake kuelewa kuwa kama tukipandikiza na mimba isipotunga basi wanaweza kujaribu tena na tena bila ya kuchoka na wakafanikiwa,’’ anasema Eliza.
Kutokana na muda, gharama na matarajio wanaume wengi hukata tamaa na kutotoa ushirikiano kwa wenza wao.
Joyce anaeleza namna wanavyowashauri wanaume kuwasaidia wanawake zao kipindi cha IVF.
“Huwa tunawashauri wanawake jinsi ya kuzungumza na waume zao ili waje pamoja hospitali kwa sababu si kila mwanamke asiyebeba ujauzito ndio anakuwa na tatizo. Wapo wanaume wenye matatizo…, tumefanikiwa sana kuwashauri wanaume kuungana na wenza wao katika matibabu,” amesema Joyce.
Joyce anasema, ‘’ugumu tunaokutana nao sana hasa matarajio makubwa ya wanawake. Wengi wanaamini wakipandikiza tu watafanikiwa, sasa majibu yakija tofauti inakuwa ngumu kukubali.’’
‘’Katika kutoa majibu ya mimba kutoshika ni lazima kumuandaa mhusika kisaikolojia kukubaliana na matokeo.’’
Ukweli kuhusu IVF
IVF ni upandikizaji wa kiinitete ndani ya kizazi baada ya uchavushaji wa mayai na mbegu kwenye maabara maalum. Kwa hali ya kawaida utungaji wa mimba hufanyika ndani ya mwili wa mwanamke katika mfuko wa uzazi.
Inavyofanyika yai na mbegu (kiinitete) umri wa siku mbili hadi nne kimoja au zaidi ya kimoja hupandikizwa ndani ya kizazi kwa kutumia chombo maalum baada ya kizazi cha mwanamke kuandaliwa.
Kwa kipindi cha miaka mitatu yaani 2020 hadi 2022 jumla ya wanawake 720 walifanya upandikizaji katika hospitali hiyo.
Niliwatazama hawa wahudumu wawili, nikawapa pongezi huku na mimi nikiendelea na matitabu ya Endometriosis nikiamini siku moja kupakata mtoto wangu lakini pia nikikumbuka kauli zao unaweza kujaribu ukashika mimba na unaweza kupandikiza zaidi ya mara moja lakini usishike mimba. Yote ni kuamini Mungu na kuweka nia mbele.