Namna ya wenza kuepuka msongo, mizozo ya ugumba

Februari 6 mwaka huu Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alikiri changamoto ya ugumba inakua kwa kasi nchini.

“Tatizo la kutopata watoto lipo pande zote mbili, upande wa wanaume na wanawake, lakini jamii yetu inachukulia familia isipopata mtoto basi mwanamke ndiyo anaonekana mwenye tatizo. Naamini uwepo wa kituo hiki utasaidia kuondoa fikra potofu,” anasema Ummy alipotembelea Taasisi ya Kairuki iliyopo Bunju A jijini Dar es Salaam Januari mwaka huu.

Hata hivyo, Ummy alionyesha nia ya Serikali kuweka nguvu katika eneo hilo ili kuhakikisha Watanzania wanamudu gharama za huduma za upandikizaji mimba ambazo zimeanza kutolewa nchini.

Takwimu zisizo rasmi hapa nchini zinaonyesha suala la ugumba katika hatua ya awali lipo kwa asilimia 20 kwa wenza ambao hawajawahi kupata mtoto na hatua ya pili ni asilimia 80 ikihusisha kundi la waliowahi kupata mtoto lakini wamechelewa kupata mwingine.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ugumba ni ugonjwa na hubainika baada ya mwenza kushindwa kupata ujauzito akiwa ndani ya uhusiano na kujamiiana mara mara kwa mwaka mmoja hadi miwili bila kinga.

Mwaka 2010 WHO ilitangaza ugumba kuwa ni janga la kimataifa na hadi sasa takwimu zilizochapishwa mwaka 2012, zilionyesha takribani watu milioni 48.5 hukaa kwa muda wa miaka mitano bila kupata ujauzito.


Jamii inasemaje?

Maria Sizya, mkazi wa Tabata anasema hali ya kukosa watoto imekuwa chanzo cha ndoa nyingi kuwa na migogoro na hatimaye kuvunjika.

Hata hivyo, anasikitishwa na mzigo huo kutuliwa mwanamke peke yake hali inayochangia manyanyaso na hata wakati mwingine kupitia ukatili.

“Ambacho nimewahi kusikia hili suala la kukosa mtoto linaweza kuwa pande zote mbili lakini tunashuhudia kwenye maisha yetu wanawake ndiyo wanabebeshwa huu mzigo. Utakuta mwanamke anasakamwa na mawifi na wakwe utafikiri wana uhakika kwamba mtoto wao hana shida,” anasema Maria.

Kwa upande wake George Homera mkazi wa Buza anasema tofauti na wengi wanavyofikiri, tatizo hilo halipaswi kuwa chanzo cha kuwatenganisha wenza zaidi ya kuungana kutafuta suluhisho.

“Nikitolea mfano wangu mimi mwenyewe nimeshawahi kuishi na mwanamke ambaye ana shida hiyo, kwa takribani miaka saba hatukuwahi kupata mtoto, binafsi sikuona kama ni tatizo tuliishi kwa upendo na kushirikiana,” anasema Homera .

“Baadaye tukaachana kwa sababu nyingine tofauti, mimi nikaanzisha uhusiano mwingine kweli nikapata mtoto yeye hadi leo hana lakini siwezi kumuona mtu wa ajabu zaidi namuombea kwa Mungu siku moja apate mtoto wake.”

Jarida la Familia limefanya mahojiano na Daktari bingwa wa masuala ya uzazi na aliyebobea kwenye upandikizaji mimba Clementina Kairuki ambaye ameeleza athari yake kwenye familia na kijamii.

Dk Clementina anasema ugumba umegawanyika kwenye makundi makuu mawili huku akitaja la kwanza lipo kwa asilimia 20 ambalo ni tatizo la msingi (primary infertility).

Anasema katika hilo wenza wanakuwa hawajawahi kupata mtoto na asilimia 80 ni tatizo la sekondari (secondary infertility).

Katika hilo anasema wenza tayari wanakuwa na mtoto mmoja au zaidi ila wanahitaji kupata mtoto au watoto mwingine zaidi.

Dk Clementina anasema aina zote za ugumba zina njia tofauti za matibabu ambazo huchukuliwa baada ya wahusika kufanyiwa vipimo na kubainika kama itahitajika tiba ya awali ya matumizi ya dawa, kusafisha kizazi, kuzibua mirija au upandikizaji wa mimba.

Mbali na hilo anasema kituo hicho kinalenga kutoa mafunzo yanayohusiana na elimu ya uzazi pandikizi ambayo bado ngeni nchini licha ya huduma hiyo kuhitajika kwa kiasi kikubwa.


Kwa nini hupati ujauzito?

Tofauti na jamii inavyoamini suala la kutopata ujauzito linamhusu mwanamke pekee, Dk Clementina anasema hali hiyo huweza kusababishwa na pande zote mbili kwa uwiano wa 50 kwa 50.

Anasema mojawapo ya sababu zinazokuchangia mimba isitungwe ni kuziba mirija ya uzazi kwa mwanamke na matatizo kwenye mfuko wa uzazi kama vile wa fibroids na endometriosis.

Sababu nyingine matatizo ya kupevuka mayai ya mwanamke, ubora na afya ya mbegu za kiume na maradhi mengine yanayoweza kumsumbua mwanamume na matatizo ya kurithi.

Anasema hilo huchagizwa na mfumo wa mbaya wa maisha unaohusisha uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe, lishe duni, magonjwa ya zinaa na kisukari ambayo hayajathibitiwa au yemetibiwa kwa muda mrefu.

Dk Clementina anasema umri wa mama nao huchangia tatizo la ugumba, “tafiti nyingi zinaonyesha kuwa uzazi unaanza kupungua kwa kasi kuanzia umri miaka 35, mfano , mama mwenye miaka 43 uhitaji mayai 80 ili kupata yai moja bora. Uzazi unapungua sana miaka kumi kabla ya mwanamke kukoma hedhi.”

Mtaalamu huyo ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Upandikizaji Mimba cha Kairuki Hospital Green IVF, anasema asilimia 30 ya kundi la watu walio kwenye kundi la umri wa kupata watoto katika nchi za Afrika zilizoko chini ya jangwa la Sahara, hukabiliwa na ugonjwa wa kutopata ujauzito.

“Nchi yetu ya Tanzania haina takwimu za kitaifa, lakini tafiti ndogo ndogo zilizochapishwa mwaka 2006 na 2016, zilionyesha kuwa wenza watatu kati ya kumi (sawa na asilimia 30) kwenye kundi la watu wenye umri wa kupata watoto, wana changamoto ya kutotunga mimba,” anasema Dk Clementina.

Mtaalamu huyo wa uzazi anasema wenza wengi wenye changamoto ya kukosa mtoto hukumbana na tatizo la afya ya akili ambalo ni matokeo ya msongo wa mawazo kupita kiasi.

“Tunasikia takwimu za kutisha kuhusu afya ya akili, kuna uwezo mkubwa tatizo hilo likachangiwa na ugumba, wenye changamoto hii wanapitia msongo wa mawazo. Wanawake ndiyo huathiriwa hukumbana zaidi na unyanyapaa katika ngazi za familia na jamii, hasa kina mama, ingawa kinababa waweza kuchangia tatizo kwa asilimia 50,” anasema Dk Clementina.

“Kuna manyanyaso, vipigo na matusi kwa kina mama, wengi wamekuwa wakitukanwa kuwa wanajaza choo tu. Wapo wanauovumilia na kupambana pamoja ila wengine hufikia uamuzi wa kuvunja ndoa.”

Mbali na hayo anasema ugumba pia ni chanzo cha kuongezeka kwa magojwa ya zinaa kama Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU)kwa sababu ya kujaribu kupata watoto hapa na pale nje ya ndoa.

Dk Clementina anasema changamoto nyingine ni umaskini hasa kuhangaika kupata tiba na kuzunguka kwa waganga wa kienyeji.

“Takwimu zinaonyesha kuwa watu hutumia wastani wa Sh500,000 mpaka Sh30 milioni wakijaribu kupata matibabu ya ujauzito bila mafanikio. Hii huathiri uchumi wa familia, elimu, lishe duni na mambo mengine,” anasema Dk Clementina.