KCMC yaanza upandikizaji kioo cha mbele cha macho

Daktari wa macho, Dk Elisante Muna

Muktasari:

  • Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) imeanza kufanya upandikizaji wa kioo cha mbele cha jicho (kornea) kwa wagonjwa wenye matatizo ya macho.

Moshi. Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) imeanza kufanya upandikizaji wa kioo cha mbele cha jicho (kornea) kwa wagonjwa wenye matatizo ya macho huku ikiwataka wananchi kuchukua hatua ya haraka kwenda kwenye vituo vya kupata huduma ya afya pale wanapogundua kuwa na aleji ya macho kuwasha.

 Hayo yamebainishwa leo Jumanne, Septemba 13, 2022 na Mtaalamu wa macho aliyebobea katika matibabu ya Kornea Hospitali ya KCMC, Dk, Elisante Muna wakati akielezea hatua ya upandikizwaji wa kioo cha mbele cha jicho iliyoanza kufanyika hospitalini hapo.

Amesema Serikali kupitia wizara ya afya kwa kushirikiana na KCMC wamewezesha kupatikana kwa vifaa tiba kwa ajili ya kufanya upandikizwaji wa kioo cha mbele cha jicho huduma ambayo hapo awali haikuwezekana kufanyika hapa nchini.

Amesema hatua hiyo itawawezesha wananchi kupata huduma hiyo hapa nchini kwa bei nafuu.

Awali, wagonjwa walilazimika kusafiri nje ya nchi huku wakitumia gharama kubwa katika matibabu.

"Matibabu ya upandikizwaji wa kornea kwa KCMC ni ya gharama nafuu,  kwa mgonjwa anayelipia atapata huduma hiyo kwa Sh 500,000 na kwa mgonjwa anayetumia bima, Bima ya Afya inamsaidia, kugharamia matibabu, hii ni tofauti na mgonjwa akienda kupatiwa matibabu nje ya nchi ambayo gharama yake sio chini ya milioni sita," amesema

Dk Muna amesema hatua ya kuwa na vifaa tiba pia imewezesha kutoa matibabu ya macho kwa  wagonjwa wenye aleji ya macho ambao bado hawajapoteza uwezo wa kuona na kutakiwa kufanyiwa upandikizwaji wa kornea.

"Wapo ambao tumewasaidia kutibu macho yao mapema kabla madhara hayajawa makubwa na kupelekea kupoteza uwezo wa kuona na kutakiwa kufanya upandikizaji lakini pia tumeweza kuwafanyia upandikizaji wa kornea kwa wagonjwa 24 ambao tayari walishaanza kupoteza uwezo wao wa kuona na wengine walikua vipofu," amesema

Akielezea  sababu zinazosababisha kornea ya jicho kufa na kupelekea mtu kukosa uwezo wa kuona, Dk Muna amesema kornea kama kioo cha mbele cha jicho kinapopata kidonda kutokana na miwasho, au kuumizwa huacha kovu sehemu ya kuona  na kunasababisha mtu kushindwa kuona kutokana na kovu hilo ambapo tiba pekee ni kuondoa kioo kilicho na  kovu.

"Tunachokifanya tunaondoa kornea iliyoharibika(yenye kovu) na kupandikiza kornea nyingine ambayo haina kovu, kwahiyo kovu likiondoka  mwanga unafika kwenye jicho na mtu anaweza kuona"

Awali, Simon Shayo ambaye ni mgonjwa aliyefanyiwa upandikizwaji wa Kornea amesema alianza kutibiwa hospitalini hapo tangu mwaka 1994, ambapo akiwa na umri wa miaka saba aliwahi kuwa kipofu uliosababishwa na macho kuwasha kwa muda mrefu.

"Niliendelea kupewa dawa na mwaka 2012 nikagundulika tatizo langu lilikua ni kovu kwenye kornea, lakini baada ya kupandikizwa kornea jana, tayari uwezo wangu wa kuona umeanza kurejea na mimi najiona mwenye mabadiliko makubwa"