Prime
KONA YA MALOTO: Samia ni Rais wa sita, si wa Awamu ya Sita

Kuna mazoea ya kimatamshi na kimaandishi, kutambua marais kwa mtindo wa awamu. Mathalan, inatamkwa kwamba Dk Samia Suluhu Hassan, ni Rais wa Awamu ya Sita, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Dk John Magufuli ni Rais wa Awamu ya Tano. Vivyo hivyo, Dk Jakaya Kikwete, Awamu ya Nne, ya tatu ni Benjamin Mkapa, kisha ya pili ni Ali Hassan Mwinyi na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, yake ni ya kwanza. Ndivyo inatamkwa na kutambuliwa hivi kimazoea.
Kuna ubaya na uzuri wa mazoea. Neno awamu, limekuwa likitumika kwa muda mrefu. Nilimsikia mwanamuziki John Komba, akiimba awamu ya kwanza Nyerere, ya pili Mwinyi.
Hata Mwalimu Nyerere, kupitia hotuba zake, alitambua uongozi wake kuwa ulikuwa awamu ya kwanza.
Mtindo wa kutaja muda wa uongozi kama awamu, ndiyo sababu ya kuibuka mkanganyiko baada ya kifo cha Dk Magufuli. Aliapishwa kuwa Rais wa Tanzania kwa muhula wa pili.
Muhula ni miaka mitano, lakini Magufuli aliongoza kwa siku 132, taifa likatangaziwa kifo chake.
Baada ya kifo cha Magufuli, kuna watu kwa kujua na kufanya makusudi au kutokujua, walianzisha maneno kwamba Rais Samia alishika madaraka ya urais na kuongoza awamu ya Magufuli. Hili ni kosa kubwa la kikatiba.
Kwenye Katiba, hakuna awamu za uongozi, ila upo muhula na idadi ya marais.
Mathalan, Dk Magufuli alikuwa Rais wa Tano, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Samia ni Rais wa Sita. Urais wa Magufuli ulikoma tangu Machi 17, 2021, taifa lilipotangaziwa kifo chake.
Kikatiba, Rais anapofariki dunia, papo hapo Makamu wa Rais anatakiwa kula kiapo ili aongoze dola. Soma Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 50, ibara ndogo ya 2 (d), ibara ya 46A ibara ndogo ya 5, ibara ya 40. Kisha, ibara 37, ibara ndogo ya 3 na 5.
Katiba haitambui awamu za uongozi, inaelekeza uchaguzi wa rais, muda wa muhula na fursa ya kuhudumia mihula miwili, ikiwa kiongozi anapata ridhaa ya wananchi, vilevile anapobarikiwa afya na uhai.
Kuweka awamu, ni sawa na kumpangia Mungu. Mfano, Mwalimu Nyerere aliongoza nchi kwa miaka 23, Mwinyi 10, Mkapa 10, Kikwete 10, Magufuli miaka mitano na siku 132. Ukitaja awamu, utakuwa na maana wengine zao ni ndefu na wapo walio na fupi.
Ukitaja Mwalimu Nyerere, ni Rais wa Kwanza, Mwinyi wa Pili, Mkapa wa Tatu, Kikwete wa Nne, Magufuli wa Tano, hapo moja kwa moja Samia ni Rais wa Sita.
Hakutakuwa na maneno ya kupotosha, kwamba yupo kiongozi anaongoza awamu ya mwingine.
Wapo watu, pengine kwa kujua au kutokujua, husema Rais Samia sasa hivi anaongoza awamu ya Magufuli, kwa hiyo Uchaguzi Mkuu 2025, kama atashinda, ndiyo ataanza muhula wake, kwa hiyo Mwenyezi Mungu akimpa afya na uhai, wanataka Uchaguzi Mkuu 2030, agombee muhula wa pili.
Katiba, ibara ya 40, ibara ndogo ya 4, inaelekeza kuwa Makamu wa Rais, aliyeapa kuwa Rais baada ya kifo cha Rais aliyemtangulia, aliyejiuzulu, aliyepoteza sifa za uchaguzi au aliyeshindwa kutekeleza majukumu yake kwa maradhi, kama muda uliobaki kufikia miaka mitano ni pungufu ya miaka mitatu, basi ataweza kugombea urais mara mbili.
Ibara hiyo hiyo, inaeleza kuwa endapo Makamu wa Rais aliyeapa kuwa Rais, ataongoza kwa miaka mitatu au zaidi, ataruhusiwa kuwania urais kwa muhula mmoja tu. Kutoka Machi 19, 2021 hadi Machi 19, 2025, Rais Samia alimitiza miaka minne madarakani.
Kwa msingi huo, Rais Samia, katika muhula wa sasa, kwa baraka ya afya na uhai, itakapofika Novemba 5, 2025, atakuwa ameongoza nchi kwa miaka mitano kasoro siku 134. Ukijumlisha na siku mbili alizoongoza kama Kaimu Rais kabla ya kuapishwa, basi itakuwa miaka mitano kasoro siku 132.
Hesabu hiyo ina maanisha kuwa kusema Rais Samia anamalizia awamu ya Magufuli, ni dhambi kubwa kikatiba.
Hivi sasa, Rais Samia anaongoza muhula wake ambao Katiba inautambua kuwa ni kamili, maana ni zaidi ya miaka mitatu.
Tafsri inayopatikana kwa kuchambua ibara ya 40 (4) ni kwamba muhula ambao siyo kamili ni ule ulio chini ya miaka mitatu. Rais Samia ameshavuka miaka minne.
Maneno kuwa Uchaguzi Mkuu 2025, Rais Samia anagombea kwa mara ya kwanza awamu yake ni kumkosea heshima na kuinyanyapaa Katiba.
Vema kuacha matamshi ya awamu, hayapo kikatiba, ila ni mazoea ambayo ni rahisi kuzalisha upotoshaji.
Rais Samia ni Rais wa Sita, alimpokea Rais wa Tano, Dk Magufuli, ambaye naye alishika usukani baada ya Rais wa Nne, Dk Kikwete, ambaye alipishana Ikulu na Rais wa Tatu, Mkapa. Vivyo hivyo kwa Mwinyi, Rais wa Pili na Nyerere, Rais wa Kwanza.
Huwezi kusikia popote duniani kuwa kuna Rais wa Awamu, marais hutambulika kwa namba zao za kushika madaraka.
George Washington ni Rais wa Kwanza wa Marekani na Donald Trump ni Rais wa 47, vilevile alikuwa Rais wa 45, lakini aliondolewa baada ya muhula mmoja kwa kushindwa uchaguzi.
Rais anayekula kiapo na kupokea utii wa kijeshi kuwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, huyo anakuwa Rais kamili. Ni dhihaka kwa Rais aliye madarakani kikatiba, kuambiwa anaongoza awamu ya mtu mwingine. Ni dhihaka kubwa.