Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mambo ya kuzingatiwa kwa wanaozaa na umri mkubwa

Ni jambo la faraja kwa wanandoa wanapopata watoto, lakini uhusiano huingia dosari kati ya wawili hao wanapochelewa kupata au kukosa kabisa mtoto.

Kitaalamu inaelezwa mwanamke anapofikisha miaka 35 na kuendelea, uwezo wake wa kubeba ujauzito hupungua na afikishapo miaka 40 uwezekano huzidi kupotea kabisa.

Uwezo wa kushika mimba huwa mkubwa zaidi kwa wenye umri wa miaka 20. Daktari bingwa wa magonjwa ya kina mama katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk Hellen Mrina anasema mwanamke ana idadi ya mayai katika ovari ambayo hayaongezeki, kadiri umri unavyoongezeka idadi ya mayai nayo huzidi kupungua.

“Mayai yanayobaki yana uwezekeno mkubwa zaidi wa kupata hitilifu na mwili huwa rahisi kuanza kupata changamoto ambazo huathiri uwezo wa kubeba mimba, pia mhusika hupata baadhi ya changamoto, ikiwemo ugonjwa unaosababishwa na uwepo wa tishu zinazofanana na ukuta wa ndani wa kifuko cha uzazi na sehemu nyingine kwenye mwili (Endometriosis) pamoja na uvimbe usio wa saratani unaojitokeza kwenye kuta za mfuko wa mimba,” anasema.

Dk Hellen anasema kwa wanandoa wenye siha njema wenye umri kuanzia miaka 20 hadi 35, takwimu zinaonyesha mwanamke mmoja kati ya wanne hupata mimba kwenye mzunguko mmoja wa hedhi, tofauti na miaka 40 ambapo mwanamke mmoja kati ya 10 ndio hupata ujauzito.

Japo hata uwezo wa mwanamume hupungua, lakini si wa kutabirika kama ulivyo kwa mwanamke.

Anasema ingawa athari hizo si za kuonekana kwa mara moja, lakini mwanamke anapofikisha umri wa miaka 40 huingia kwenye hatari kubwa ya kupata shinikizo la juu la damu wakati wa ujauzito (Preeclampia), kisukari pamoja na maradhi ya figo na mtoto mwenye mtindio wa ubongo.

“Kuwa na umri mkubwa kunaongeza hatari ya kupata magonjwa ikilinganishwa na kuwa kijana, hivyo kuwa na shinikizo la juu la damu kabla ya ujauzito kunaongeza shinikizo kuwa juu zaidi baada ya kubeba ujauzito,” anasema Dk Hellen.

Ili kupunguza hatari ya kupata shida hiyo wakati wa ujauzito, Dk Hellen anasema mwanamke anapofikisha miaka 35 au zaidi ni muhimu apate ushauri wa watalaamu, ili kupata tiba itakayomsaidia kupunguza athari zitokanazo na ugonjwa huo wakati wa ujauzito.

Kwa upande wake, Daktari bingwa wa magonjwa ya kina mama katika Hospitali ya Aga Khan, Munawar Kaguta anasema mwanamke mwenye umri mkubwa anapobeba ujauzito anapaswa kufanya uchunguzi wa kina juu ya afya ya mtoto aliye tumboni.

Anasema endapo mtoto atagundulika kuwa na hitilafu katika kipindi cha wiki 20 ya uzazi inashauriwa kiumbe kilichopo tumboni kitolewe.

Naye daktari bingwa wa magonjwa ya kina mama na uzazi katika Hospitali ya Aga Khan, Dk Lynn Moshi anasema mama anapopata afua mbalimbali za kumtayarisha kabla ya kupata ujauzito kunaweza kumpunguzia hatari ya kupata mtoto mwenye changamoto mbalimbali.

“Tunaweza kupunguza athari kwa kula vyakula vyenye kuupa mwili afya, pia kutumia vitamin zinazotolewa kwa mama anayejiandaa kupata ujauzito, mafuta ya samaki na vitamin E na nyinginezo ambazo zinajenga maungo na seli kwa wanaume na wanawake,” anasema.

Dk Lynn anataja magonjwa yanayoweza kumchelewesha mwanamke kubeba ujauzito mojawapo ni athari katika njia ya kupitisha mayai, ili kumwezesha mwanamume kutungisha ujauzito (PID) pamoja na uvimbe kwenye eneo la kizazi.

Kauli hiyo inaungwa mkono na mtafiti Dk Egidius Mwemezi, anayekiri kwamba wanawake wanaopata ujauzito wakiwa na umri mkubwa wanaweza kukabiliwa na changamoto za kiafya.

“Hata hivyo, kuna hatua kadhaa wanazoweza kuchukua kupunguza hatari ya matatizo ya kiafya kwa watoto wao. Hapa kuna mambo kadhaa wanawake wanaweza kuzingatia.

“Kupata ushauri wa kiafya. Wanawake waliochelewesha kupata watoto wanapaswa kuzungumza na wataalamu wa afya kama vile daktari wa uzazi au mshauri wa uzazi.

“Wataalamu hawa wanaweza kutoa ushauri muhimu na kufanya uchunguzi wa kiafya, ili kuhakikisha mwili wa mwanamke uko katika hali nzuri ya kuwa na ujauzito,” anasema.

Jambo lingine analoshauri Dk Mwemezi ni wanawake kuzingatia lishe bora na kufanya mazoezi, ili kudumisha afya ya mwili.

Anasema hayo husaidia kupunguza hatari ya matatizo ya kiafya kwa mtoto na kuongeza nafasi za kupata ujauzito.

“Pia ni muhimu kufanya uchunguzi wa vinasaba kwa wanawake wenye umri mkubwa kwa ajili ya kutambua hatari za kuzaa mtoto mwenye matatizo. Uchunguzi huo unatagundua uwepo wa kasoro za vinasaba ambazo zinaweza kuathiri ukuaji na maendeleo ya mtoto,” anasema.

Dk Mwemezi anasema pia ni muhimu mwanamke kufuata ushauri wa kitaalamu, ikiwamo kuchukua dawa zinazohitajika, kufanya matibabu ya uzazi au kufuata njia nyingine za kuongeza nafasi za kupata ujauzito na kuepuka matatizo kwa mtoto.

“Wanawake wanapaswa kuelewa hatari zinazohusiana na kupata watoto wakiwa na umri mkubwa na kuwa tayari kukabiliana na changamoto zinazojitokeza.

“Hii ni pamoja na kuwa tayari kiakili, kihisia na kifedha kukabiliana na uwezekano wa matatizo ya kiafya kwa mtoto na changamoto nyingine za kuwa mzazi,” anasema.

Pamoja na hayo, Dk Mwemezi anasema ni muhimu mwanamume kuangalia afya yake, kwani matatizo ya kiume yanaweza kusababisha ugumu wa kutungisha mimba au matatizo kwa watoto.

Anasema uchunguzi wa afya ya uzazi kwa mwenzi wa kiume kama kuchunguza kiasi na ubora wa manii, inaweza kusaidia kutambua masuala yanayohitaji kushughulikiwa.

Pia Dk Mwemezi anashauri mchakato wa kuhifadhi mayai ya uzazi kwa mwanamke kwa ajili ya matumizi ya baadaye.

“Hii inaweza kuwa chaguo kwa wanawake wanaotaka kuchelewesha kupata watoto, lakini wanahofia kupungua kwa ubora na idadi ya mayai wanayozalisha. Hifadhi ya mayai ya uzazi inaweza kutoa fursa ya kuwa na mayai ya vijana hata wanapokuwa na umri mkubwa,” anasema.

Dk Mwemezi anasema ni muhimu kufanya maamuzi ya kina na kushauriana na wataalamu wa afya, ili kupata mwongozo unaofaa na sahihi kulingana na hali ya mtu binafsi.