Jela maisha kwa ulawiti, ubakaji Njombe

Muktasari:
- Hukumu hizo lzimetolewa leo Oktoba 11 na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Njombe, Matilda Kayombo akisema mahakama hiyo imeridhishwa na ushahidi uliotolewa.
Njombe. Mahakama ya hakimu mkazi Wilaya ya Njombe imemhukumu kwenda jela maisha Jackson Makweta (26) kifungo cha maisha kwa kosa la kubaka na kumlawiti mtoto mwenye miaka 14, huku pia ikimhukumu Jonas Lufumbilo (29) kwenda jela miaka 30 kwa kosa la kubaka mtoto mwenye umri wa miaka 12.
Akisoma hukumu hizo leo Oktoba 11 na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Njombe, Matilda Kayombo amesema washtakiwa hao walitenda makosa hayo mapema mwaka huu katika maeneo tofauti ya wilayani humo.
Amesema washtakiwa hao walifanya kosa la ubakaji kinyume na kifungu cha sheria namba 130 kifungu kidogo cha 1 na 2 (e) sambamba na kifungu namba 131(1) cha kwanza cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2002.
Amesema kosa la ulawiti lililofanywa na mmoja ya washtakiwa hao ni kinyume na kifungu cha sheria namba 154 kifungu kidogo cha 1 na 2 cha sheria ya kanuni ya adhabu Sura ya 16 marejeo ya 2002.
Amesema mshtakiwa Jonas Lufumbilo kwenye kesi namba 17 ya mwaka 2023 alimbaka mwanafunzi wa darasa la nne umri miaka 12 katika kijiji cha Kidegembye kilichopo wilaya ya Njombe.
Amesema siku ya tukio mshtakuwa huyo aliyemchukua mwanafunzi huyo na kwenda kumbaka katika shamba la miti lililopo kijijini hapo.
Amesema katika kesi hiyo namba 52 ya mwaka 2023 inayomuhusu Jackson Makweta ambaye ameshtakiwa kwa kosa la kumbaka na kumlawiti msichana mwenye umri wa miaka 14 tukio hilo alilifanya katika kijiji cha Isitu kata ya Ninga wilayani Njombe.
"Mshtakiwa alimkamata mtoto alipokuwa anaelekea kanisani na kumziba mdomo na kumvutia katika shamba la chai kabla ya kumbaka na kumlawiti," amesema Kayombo.
Amesema washtakiwa wote wawili wamekutwa na hatia baada ya mahakama kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na waathirika wa tukio pamoja na taarifa ya uchunguzi kutoka kwa madaktari.
Amesema baada ya kujiridhisha kwa ushahidi huo ndipo akatoa hukumu kwa Jonas Lufumbilo kwenda jela miaka 30 kwa kosa la ubakaji na Jackson Makweta amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na kifungo cha maisha kutokana na kukutwa na makosa mawili ya kubaka na kulawiti.
Awali Wakili wa Serikali, Magdalena Whero aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa watu wenye tabia ya namna hiyo.