Kinyozi mbaroni akidaiwa kubaka, kulawiti mtoto
Muktasari:
- Jeshi la Polisi mkoani Geita, linamshikilia Simon Faida (24) Mkazi wa Kijiji cha Msasa, Kata ya Busanda, Wilaya ya Geita; kwa tuhuma za kumbaka na kumlawiti mtoto mwenye umri wa miaka 8.
Geita. Jeshi la Polisi mkoani Geita, linamshikilia Simon Faida (24) Mkazi wa Kijiji cha Msasa, Kata ya Busanda, Wilaya ya Geita; kwa tuhuma za kumbaka na kumlawiti mtoto mwenye umri wa miaka 8.
Mtuhumiwa huyo ambae ni kinyozi, anadaiwa kutenda tukio hilo Julai 23, 2023 huko Msasa, baada ya kumrubuni mtoto huyo kwa kumpa vitu vidogo vidogo.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, Adam Maro, amethibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na kusema tayari wamefanya uchunguzi ikiwa ni pamoja na kupata vipimo kutoka hospitali, vilivyothibitisha mtoto huyo kuingiliwa sehemu zote mbili.
“Huyu mtoto baada ya kuingiliwa, alitembea kwa shida, na akiwa nyumbani, alipotaka kujisaidia alishindwa na kuanza kulia kutokana na maumivu ndipo wazazi wake walimchunguza na kubaini ameingiliwa na kumtaja aliyemuingilia, ndipo wazazi walitoa taarifa, na polisi walimkamata mtuhumiwa, na kumpeleka mtoto hospitali,” amesema Kaimu Kamanda.
Maro amesema uchunguzi umekamilika na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani wakati wowote kujibu shtaka linalomkabili na kuwataka wazazi kuwa karibu na watoto ili kujua mienendo yao mapema.
“Wazazi wawe na utamaduni wa kuzungumza na mtoto lakini wawajengee ujasiri wa kuwaamini wazazi, ili pindi anapofanyiwa tukio lolote la ukatili, awe wazi kusema bila hofu, wapo watoto wanafanyiwa ukatili lakini kutokana na hofu, wanaficha wakiogopa kuchapwa,” amesema.