Jela miaka 60 kwa kumbaka, kumlawiti mtoto wa mkewe

Muktasari:

  • Afungwa miaka 60 kwa kosa la kubaka na kulawiti mtoto wa Mkewe (13) Nanyumbu akiwa miongoni mwa watuhumiwa 84 waliofikishwa mahakamani kwa makosa mbalimbali baada ya kukamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Mtwara.

Mtwara. Mkazi wa Kijiji cha Likokona, wilayani Nanyumbu, Defao Kashimu Abdallah (25), amehukumiwa kifungo cha miaka 60 jela, baada ya kukutwa na hatia ya kubaka na kulawiti mtoto wa mkewe mwenye umri wa miaka 13.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Kamanda Mtaki Kurwijila, hukumu hiyo ilitolewa Agosti, 28 mwaka huu, na kwamba Abdallah alikamatwa Novemba 27, 2022 katika kijiji cha Likokona.

Akizungumza na Mwanachi Digital jana Septemba 13, Kamanda Kurwijila amesema kuwa mdaiwa huyo, amehukumiwa kwenda jela miaka 60 baada ya Mahakama ya Wilaya ya Nanyumbu kumtia hatiani kwa kosa hilo la kubaka na kulawiti.

Mtuhumiwa huyo ni miongoni mwa watuhumiwa wengine 84 waliofikishwa katika mahakama mbalimbali mkoani Mtwara na jeshi hilo, ambapo wamekutwa na hatia.

“Tumekuwa tukitoa elimu ya kupambana na uharifu kwa wananchi kupitia Wakaguzi Kata, ambapo imesaidia kwa kiwango kikubwa kupata ushirikiano na wananchi ili kukomesha matukio ya kiharifu, ambapo pia tumefanikiwa kukamata watuhumiwa 11 kwa kukutwa na pombe ya moshi lita 67,” amesema na kuongeza;

“Lakini pia wapo 45 waliokamatwa kwa makosa mbalimbali ikiwemo wizi wa pikipiki ambapo watuhumiwa wote wamefikishwa mahakamani na kesi zipo katika hatua mbalimbali.”

Kamanda huyo ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa lengo la kukomesha matukio ya kiharifu, hususan unyanyasaji wa kijinsia na matendo ya ukatili kwa watoto, ili hatua kali za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya wote wanaofanya hayo matendo.