Jeshi la Uhamiaji laanzisha mtambue jirani yako kudhibiti wahamiaji

Muktasari:

  •  Jeshi la Uhamiaji Tanzania limeanzisha mpango wa utoaji wa elimu kwa wananchi itayosaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi ikiwa ni mpango mkakati wa kudhibiti uingiaji holela wa wageni kutoka mataifa mbalimbali hapa nchini.





Morogoro. Jeshi la Uhamiaji Tanzania limeanzisha mpango wa utoaji wa elimu kwa wananchi itayosaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi ikiwa ni mpango mkakati wa kudhibiti uingiaji holela wa wageni kutoka mataifa mbalimbali hapa nchini.

Akizungumza katika mdahalo wa ulinzi na usalama kwa waandishi wa habari na wakuu wa vyombo vya ulinzi ulinzi na usalama leo Juni 8, mkoani hapa, Mrakibu wa Jeshi la Uhamiaji Tanzania Mkoa wa Morogoro, Richard Sasongwe amesema kampeni hiyo ni mikakati ya Jeshi hilo lenye lengo la udhibiti wageni wanaoingia nchini.

Mrakibu Richard amesema kampeni hiyo ni mtambue jirani yako imelenga kuimarisha usalama wa taifa kwa kudhibiti wageni kutoka nje ya nchi “Wahamiaji Haramu” ili kuepuka madhara ambayo yanaweza kutokea na kuiletea athari nchi.

“Tumeanzisha Kampeni ya Mjue Jirani Yako katika ngazi ya kaya, hii lengo letu ni kudhibiti wahamiaji haramu ambao wanaingia nchini kwa njia zisizo halali, itasaidia kuwatambua wageni wabaya kwani wapo wageni wanaingia katika nchi kwa lengo la kupeleleza jambo fulani kwa manufaa ya nchi zao,”amesema Mrakibu Richard.

Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro, Ralph Meela amesema suala la ulinzi na usalama kwa waandishi wa habari linaanzia kwa mwandishi mwenyewe katika kujilinda.

“Mwandishi ili kujilinda mwenyewe anapaswa kupima kazi anayoenda kuifanya lakini mwandishi kujiepuka kuandika habari ambazo zitaleta taharuki katika jamii na viongozi,”amesema Meela.


Katibu Tawala Msaidizi, Uchumi na Uzalishaji Mali Mkoa wa Morogoro, Dk Rozalia Rwegasila amesema serikali imekuwa ikitambua umuhimu wa waandishi wa habari katika kutoa habari za maendeleo ili jamii kuweza kutambua kitu gani kinafanyika katika eneo husika.


“Mdahalo huo ni kuendelea kuimarishaa mahusiano kati yetu na waandishi wa habari na serikali inatambua mchango wa waandishi wa habari,”amesema Dk Rwegasila.

Mwenyekiti wa Umoja wa Waandishi wa Habari Mkoa wa Morogoro, Nikison Mkilanya amesema mdahalo huo ni mwendelezo wa kuimarisha uhusiano na vyombo vya ulinzi na usalama.