JICHO LETU MAHAKAMANI: Mwanamke alivyomsaidia mumewe kumbaka mwanawe wa miaka minne

Muktasari:

Si rahisi kuamini lakini ilitokea huko Mbarali, mkoani Mbeya bila kuripotiwa.

Si rahisi kuamini lakini ilitokea huko Mbarali, mkoani Mbeya bila kuripotiwa.

Hiki ni kisa cha kusikitisha cha mtoto wa miaka minne, *Jane Mwikila (si jina halisi), aliyebakwa na baba yake wa kambo na kuharibiwa sehemu za siri huku mama yake mzazi akisaidia kutekelezwa kwa unyama huo.

Elias Mwangoka, maarufu kwa jina la Kingloli, alifanya ukatili huo asubuhi ya Aprili 30, 2006 katika Kijiji cha Muhelwa, Wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya huku mke wake, Agnes Mwakisyala akimsaidia kwa kumbana miguu mwanawe asifurukute.

Baada ya kukwepa mkono wa dola kwa miaka minne, hatimaye Mwangoka alikamatwa mwaka 2010, akashtakiwa na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela. Atasalia huko kwa maisha yake yaliyobaki baada ya Mahakama ya Rufani kutupilia mbali rufaa yake ya hivi karibu aliyokuwa akipinga adhabu aliyopewa.

Majaji wa Mahakama ya Rufani-Jacobs Mwambegele, Lugano Mwandambo na Lilian Mashaka wamekataa kutengua uamuzi wakisema kesi dhidi yake ilithibitishwa bila kuacha shaka.


Ilivyokuwa

Tukio la kubakwa Jane lina mizizi mirefu. Mwangoka na Agnes Mwakisyala (mama wa mtoto aliyebakwa) waliishi pamoja kama mume na mke, wakati mwanamke akiwa ameshampata mtoto huyo na mwanamume mwingine, Christopher Mbeyela.

Mwangoka alimkamata Jane, akamuingiza chumbani kwao na kuanza kumuingizia uume wake kwa nguvu, ajabu ni kwamba unyama huo ulipokuwa ukifanyika, mama yake Jane (Agnes) ndiye alikuwa amembana mwanawe minguu yote ili asifurukute wakati wa kitendo hicho kikiendelea.

Nyaraka zilizopo mahakamani na maelezo ya mashahidi, akiwemo mwathirika, vinaonyesha kuwa baada ya tukio hilo, Jane alikuwa na hali mbaya.


Kwa mganga wa kienyeji

Baada ya kuona hali ya mtoto inaziki kuwa mbaya, Mwangoka na mke wake walimchukua Jane na kumpeleka kwa mganga wa kienyeji eneo la Usangu.

Alipomchunguza mtoto, mganga huyo aliwapatia dawa na kuwaelekeza wampake mwathirika sehemu za siri kwani alikuwa ameumia vibaya.


Wampeleka Jane kwa baba yake

Siku mbili baadaye, mama yake Jane alianza kuhamanika kutokana na hali ya mtoto. Alimwomba Neri Ngonya, jirani yake ambaye alikuwa amepanga kwenda Mbeya Mjini, amsaidie kuondoka na Jane ili ampeleke kwa baba yake mzazi (Mbeyela) kwa ajili ya matibabu.

Agnes na Neri wote walikuwa wamezaa na Mbeyela aliyekuwa akiishi Mbeya Mjini.

Kabla hajamkabidhi, mtoto kwa Neri, mama Jane alimfunga mwanawe kwa nepi iliyotengenezwa kienyeji maarufu kwa jina la kibwende katika jitihada za kuzuia mkojo uliokuwa ukimtoka pasipo kujizuia. Neri aliitikia wito wa Agnes na kumpeleke Jane kwa baba yake ambaye pia alimpeleka mtoto huyo kwa bibi yake mzaa baba ili akae naye.

Unyama aliotendewa Jane ulianza kujulikana siku moja baada ya kuanza kuishi na bibi yake, Atatugela Kyando. Akiwa chini ya ulezi wa bibi yake, Jane alionekana mwenye hali isiyokuwa ya kawaida ikiwemo ya kushindwa kuzuia mkojo na kutoa harufu mbaya.

Hali hiyo ilimtia wasiwasi bibi yake aliyeamua kumkagua mjukuu wake sehemu za siri. Bibi huyo aligundua kuwa sehemu hizo zilikuwa wazi na zimelegea kuliko kawaida, hali iliyofanya aamini mjukuu wake alikuwa ameingiliwa.

Bila kupoteza muda, alimpeleka Hospitali ya Meta mjini Mbeya kwa uchunguzi wa kitabibu, baada ya kuwa amepata fomu ya polisi ya matibabu.

Katika Hospitali ya Meta, Daktari Cosmas Chacha ndiye aliyechunguza sehemu za siri za mbele na nyuma za Jane. Daktari huyo ambaye baadaye alitoa ushahidi mahakamani alihitimisha kuwa Jane alikuwa amepoteza ubikira, hali iliyoashiria alikuwa ameingiliwa.

Kabla ya hapo, askari mpelelezi, Mary Barnabas, ambaye alielekezwa kupeleleza kesi hiyo, alikwishakagua sehemu za siri za Jane na kutoa maoni kuwa alikuwa amebakwa.


Upelelezi mbovu

Licha ya kwamba Mwangoka alifanya unyama huo Aprili, 2006, hakukamatwa hadi Septemba 2010 kufuatia juhudi kubwa ya baba wa mwathirika, Christopher Mbeyela na mjomba wake, Bise Sanga kwa msaada wa msiri wao.

Wakati wa usikilizwaji wa rufaa ya kwanza ya Mwangoka, Mahakama Kuu ilitamka wazi kuwa kesi hiyo ilipelelezwa vibaya na polisi wa Wilaya ya Mbeya baada ya tukio hilo kuripotiwa Mei 5, 2006.

Askari aliyekuwa akipeleleza kesi hiyo aliwahi kuiambia Mahakama kuwa kuchelewa kumkamatwa mtuhumiwa kwa kiasi fulani kulichangiwa na tukio hilo kutokea nje ya mamlaka ya kiutawala ya kipolisi ya Wilaya ya Mbeya na mpelelezi huyo kutokuwepo kwani alikuwa akihudhuria mafunzo ya miezi mitatu, Moshi.

Baba wa mwathirika aliiambia Mahakama kuwa polisi wa Mbeya walimwambia wasingeweza kumkamata mshukiwa aliyekuwa nje ya mamlaka yao ya kiutawala.

Baada ya kuona anapigwa danadana, mjomba wa mzazi wa mwathirika, Bise Sanga na binamu yake waliamua kusafiri hadi Kituo cha Polisi, Isanya.

Polisi katika kituo hicho walifanyia kazi malalamiko yao kwa kutoa gari kusaidia kumsaka mtuhumiwa aliyeaminika kujificha katika Kijiji cha Muhwela wakiambatana na askari polisi watatu.

Zamu hii hawakufanikiwa kumkata mshukiwa ambaye alikimbia baada ya kuona gari la polisi.

Kukamatwa kwa Mwangoka miaka minne baadaye kulitokana na jitihada za Sanga akisaidiana na msiri wake waliyekuwa wakifuatilia nyendo za mtuhumiwa na kuripoti polisi kwa simu walipomwona.

Mwangoka alikamatwa Mbarali baada ya kuwa ameitelekeza familia yake kwa miaka minne na alishtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mbeya. Alidai katika utetezi wake kuwa kukamatwa kwake ilikuwa ni sehemu ya jitihada za baba wa mwathirika kulipa kisasi ya kumnyang’anya mke na kumfanya mke wake (Agnes, mama wa mwathirika).

Alidai alilazimika kukiri kosa polisi baada ya kuteswa na kutishiwa kuuawa. Mahakama hiyo iliukataa ushahidi wake, ikisema haukuwa na uzito wa kuviza kesi ya upande wa mashitaka. Hivyo, ilimfunga jela maisha.


Rufaa ya kwanza

Mwangoka alikata rufaa ya kwanza kupinga kutiwa hatiani na kifungo cha maisha Mahakama Kuu mwaka 2018. Baada ya kusikiliza hoja zake, Mahakama hiyo ilitupilia mbali rufaa yake iliyokuwa na hoja baada ya kukubaliana na Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mbeya.


Rufaa ya pili

Baada ya kushindwa rufaa ya kwanza, Mwangoka alikimbilia Mahakama ya Rufani na kuwasilisha hoja 12 kwa nini alipaswa kuachiwa huru.

Moja ya hoja zake ni kwamba Mahakama iliyomfunga ilikosea kwa kupokea ushahidi wa mwathirika ambaye ni mtoto wa chini ya umri wa miaka kumi bila kumhoji kama anajua maana ya kiapo kama sheria inavyotaka.

Wakili wa Serikali Mkuu alikubaliana na hoja hiyo ya kisheria kwa kuwa mwathirika alitoa ushahidi bila kiapo, lakini akasisitiza kuwa ushahidi wa mwathirika ulipata nguvu kisheria kwa sababu uliungwa mkono na ushahidi mwingine.

Alirejea uamuzi wa Mahakama hiyo katika kesi ya Nguza Vicking, maarufu kama Babu Seya na wengine watatu dhidi ya Jamhuri ambao walitoa hoja kama hiyo, lakini walishindwa baada ya Mahakama kuridhika kuwa ushahidi wa waathirka uliungwa mkono na ushahidi mwingine.

Mahakama ilitupilia mbali hoja yake ikisema kuwa ushahidi wa mwathirika uliungwa mkono na ushahidi mwingine.

“Kwa kumbukumbu zilizopo, hakuna shaka kuwa Mahakama mbili za chini (Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya na Mahakama Kuu) hawakukosea waliposema kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha kesi dhidi ya mrufani kwa viwango vinavyotakiwa katika kesi za jinai,” ilisema Mahakama.