Jina la Tanzania laibuka tena siasa za Uingereza

Muktasari:

  • Kinyang’anyiro cha kuwania wadhifa wa Waziri Mkuu wa Uingereza safari hii kinamuhusisha mgombea mwenye wazazi waliozaliwa Afrika Mashariki.

London. Kinyang’anyiro cha kuwania wadhifa wa Waziri Mkuu wa Uingereza safari hii kinamuhusisha mgombea mwenye wazazi waliozaliwa Afrika Mashariki.

Mgombea huyo, Rishi Sunak, alikuwa Waziri wa Fedha wa Uingereza kuanzia mwaka 2020 hadi mwaka huu alipojiuzulu nafasi hiyo.

Sunak, ambaye tayari ametangaza kuwania nafasi ya uongozi wa Chama cha Conservative baada ya Boris Johnson kujiuzulu, baba yake alizaliwa nchini Kenya na mama yake alizaliwa Tanganyika (sasa Tanzania).

Boris Johnson anakuwa Waziri Mkuu wa tatu wa Uingereza kujiuzulu nafasi hiyo ndani ya kipindi cha miaka sita na wote wanatoka chama cha Conservative.

David Cameron, aliyekuwa Waziri Mkuu kuanzia mwaka 2010, alijiuzulu mwaka 2016 kwa shinikizo, ikiwamo masuala ya kutetea ushoga.

Theresa May alichukua nafasi hiyo kuanzia mwaka 2016 na alijiuzulu mwaka 2001 kwa shinikizo la Brexit.

Na sasa, Sunak anawania nafasi hiyo baada ya Boris Johnson kujiuzulu uongozi wa chama cha Conservative na pia ataachia nafasi ya uwaziri mkuu.

Hii itakuwa ni mara nyingine kwa jina la Tanzania kuibuka kwenye siasa za Uingereza.

Hivi karibuni, raia wa Uingereza mwenye asili ya Tanzania, Linda Lusingu aligombea udiwani kupitia Chama cha Labour na kushinda nafasi hiyo katika kata ya East Barnet, iliyoko mji mkuu wa London.

Nia ya kugombea

Sunak, anayechukuliwa kuwa mrithi wa Boris Johnson, alitaja sababu za kugombea nafasi hiyo kuwa nchi ina changamoto nyingi.

Mwanasiasa huyo kijana alichapisha video kwenye ukurasa wake wa Twitter na kuandika:

“Nimesimama kuwa kiongozi ajaye wa Chama cha Conservative na Waziri Mkuu wenu. Turudishe uaminifu, tujenge upya uchumi na kuunganisha nchi.”

Conservative inavyochagua kiongozi mpya

Baada ya kiongozi wa Conservative kujiuzulu, huitishwa uchaguzi wa kiongozi mpya.

Mgombea ili awe na sifa ya kuwania anapaswa kuungwa mkono na wabunge wanane wa chama hicho, wakiidhinishwa kama wapo zaidi ya wawili wabunge watashiriki kuwachagua hadi wabaki wawili kwa sharti la kupata kura tano kila mmoja.

Katika hatua ya pili ni sharti wapate asilimia 10 ya kura, hatua inayofuata atakayekuwa na kura chache ataondolewa.

Wakati wabunge wawili watakaobaki watapigiwa kura na wanachama wote wa chama cha Conservative kumpata mshindi.