Jinsi benki zinavyopigwa mabilioni ya fedha

Muktasari:

  • Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imezitahadharisha benki kuongeza udhibiti kwenye mifumo ya ulinzi wa fedha baada ya kubaini kuwepo wizi wa njia mbalimbali.

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imezitahadharisha benki kuongeza udhibiti wa mifumo ya ulinzi wa fedha baada ya kubaini kwa mwaka mmoja wa 2023 wizi uliofanywa katika sekta ya fedha hiyo nchini ulisababisha hasara ya Sh10.28 bilioni.

BoT imezifahamisha benki hizo kuwa kwa kila robo ya mwaka huo kulikuwa na wizi usiopungua wa Sh2.4 bilioni na kiwango cha juu zaidi kilikuwa ni robo iliyoishia Septemba 2023, ambapo ziliibwa Sh2.67.

Taarifa kwa mabenki iliyotolewa na Kurugenzi ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inayosimamia sekta ya fedha, imebainisha kuwa wizi mkubwa ziadi ulifanywa katika huduma za benki kwa simu (mobile banking) na benki mtandao (internet banking).

“Benki Kuu inapenda kutaarifu juu ya visa vya udanganyifu vilivyotokea katika sekta ya benki kwa robo nne za mwaka 2023 … tunatarajia kuwa mrejesho huu utasaidia kuongeza udhibiti wa ndani kwa muktadha wa kupunguza hasara zitokanazo na udanganyifu,” ilielezea taarifa hiyo ambayo BoT imethibitisha kuiandika.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wizi utokanao na watumishi wa benki katika mwaka husika ulikuwa Sh2.47 bilioni, wizi utokanao na huduma za benki kwa njia ya simu na mtandao ulikuwa Sh4.89 nilioni, wizi kwa mashine za ATM Sh741.13, cheki za kughushi Sh1.02 bilioni na namna nyinginezo Sh1.15 bilioni.

Hata hivyo, tofauti na miaka ya nyuma taarifa hiyo inaonyesha mwaka 2023 hapakuwa na matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha katika sekta hiyo.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Mabenki Tanzania, Tuse Mwaikasu hakuwa tayari kuzungumzia jambo hilo, akisema taarifa ya BoT haikuwa kwa ajili ya umma, bali ilielekezwa kwa watoa huduma za kibenki.

“Mimi kutolea maelezo jambo hilo si sawa kwa kuwa si la umma bali ni la benki, lingekuwa la umma ningesema,” alisema Mwaikasu.

Akizungumza na gazeti la The Citizen, Mchambuzi wa masuala ya kibenki,  Kelvin Mkwawa amesema kuna haja ya kuchukua hatua za haraka kuzuia wizi huo.

“Udanganyifu wa kadi za ATM unaweza kuhusishwa na kushamiri kwa biashara ya mtandaoni na malipo ya mtandaoni, jambo ambalo linahatarisha usalama wa taarifa za wateja,” alisema Mkwawa na kuongeza kuwa teknolojia za sasa za ‘kuchanja’ na ‘kugusisha’ zinaongeza hatari hiyo.


Uhalifu unavyofanyika

Kuhusu mbinu za kisasa zinazotumiwa na wahalifu wa mtandao, Mkwawa anasema wateja wanaweza kupokea viungo vilivyoathiriwa na programu hasidi bila kujua, hivyo kurahisisha upatikanaji wa taarifa zao za fedha bila idhini yao.

Mkwawa pia anabainisha kukithiri wizi wa katika huduma za benki kwa njia ya mtandao kunatokana na utapeli wa watu na wapesi wa benki kutoa taarifa za wateja, jambo ambalo zinawapa uhalali wezi wa kuiba fedha.

Hata hivyo, amesema mara nyingi hii huhusisha watu ndani ya benki ambao sio waaminifu kwa kula njama wa wanaotekeleza uhalifu wa aina hiyo.

"Akaunti zilizolala ziko hatarini zaidi kwa wizi wa namna hiyo," anasema huku akifafanua kuwa baada ya mwizi kupata taarifa zote za akaunti hiyo kwa mtu wa ndani, huenda kuomba idhini kupitia tawi jingine la benki.

Pia kuna ulaghai wa mikopo ambapo wahalifu hutumia utambulisho wa makampuni yanayotambulika ili kupata mikopo kwa wafanyakazi wa uongo.

"Kuwa na mbinu za kisasa za kiteknolojia kudhibiti usalama ni muhimu katika kuzuia wizi wa mtandaoni unaozidi kuongezeka," amesisitiza.

Zaidi ya ulinzi wa kiteknolojia, Mkwawa alisisitiza umuhimu wa kutoa zaidi elimu ya fedha miongoni mwa watumiaji ili kuongeza uelewa na kulinda taarifa zao nyeti.

"Benki lazima pia ziweke kipaumbele katika kuajiri na kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wenye maadili ya viwango vya juu," amesema.


Athari za uhalifu huo

Kwa upande wake Mhadhiri Msaidizi wa Nenki na Fedha katika Chuo Kikuu Ardhi (ARU), Aziz Rashid amesema matukio hayo yasipodhibitiwa yataathiri uchumi wa nchi.

“Miongoni mwa changamoto za uchumi wa kidijitali ni ulaghai na uhalifu wa kimtandao. Ulaghai husababisha kupoteza pesa, hivyo uchumi huathirika, lakini uhalifu wa kimtandao unaweza kutikisha hadi uchumi wa nchi,” alisema Rashid.

Mkufunzi huyo ameongeza kuwa vitendo vya wizi vinapoteza fedha ndogondogo lakini visipodhibitiwa vikahamia kwenye uhalifu wa kuhamisha fedha nyingi zaidi, itakuwa hatari kwa uchumi wa nchi.