Jinsi fedha zinavyovunja uhusiano

Jinsi fedha zinavyovunja uhusiano

Muktasari:

  • Kipanya yeye anasisitiza kuwa mwanaume ndiye mwenye jukumu la kumhudumia mwanamke na familia kwa ujumla hata kama mwenza wake ana uwezo kiuchumi.

Dar es Salaam. Mjadala mkali umeibuka siku za karibuni kati ya wanawake na wanaume, ambao unataja fedha kuwa chanzo kikubwa cha ndoa na uhusiano wa mapenzi kuvunjika.

Mjadala huo umekuja ikiwa ni siku chache baada ya gazeti hili kuripoti mfululizo wa ripoti maalum kuhusu ongezeko la talaka na ndoa zinazovunjika, huku wanawake wakitupa lawama kwa wanaume kuwa hawataki kuwajibika katika suala zima la kuendesha familia kiuchumi.

Kilichozua mjadala zaidi ni video inayomuonyesha mjasiriamali Max Rioba akieleza kwamba, hataki mwanamke anayeomba pesa na ana utaratibu wa kumpa pesa mpenzi wake bila kuombwa.

“Hakuna kitu wanaume wanachukia kama kuombwa hela, ukiniomba pesa nakublock kabisa, nakata mawasiliano yaani ndio tunamalizana kihivyo, kwanza kwa nini uniombe. Unajua mwanaume anayempa mwanamke fedha bila kuombwa anampa nyingi kuliko anayeomba,” alisema Max.

Kauli hii ya Max imeonekana kuwaudhi wanawake wengi na kuwafurahisha baadhi ya wanaume, ambao nao wanaamini kuwa mapenzi ya kweli hayashikiliwi na fedha.

Raymond Kweka mkazi wa Sinza anaungana na Max na kueleza kuwa tabia ya wanawake kupenda kuomba fedha imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa uhusiano kuvunjika.

“Kuwa na wewe kwenye uhusiano haina maana unifanye mimi chanzo chako cha mapato. Tufurahie mapenzi, nikiwa nacho nitakupatia lakini usinilazimishe nikupe kila siku tena na wewe unafanya kazi kwa nini usitumie hela yako,” alisema Kweka.

Wakati Max na Kweka wakiwa na mtazamo huo kuna video nyingine inayotembea mtandaoni ya mtangazani na mchora katuni Masoud Kipanya.

Kipanya yeye anasisitiza kuwa mwanaume ndiye mwenye jukumu la kumhudumia mwanamke na familia kwa ujumla hata kama mwenza wake ana uwezo kiuchumi.

“Mwanaume anayeshindana na mwanamke ni mpumbavu, hawa wanawake wanahitaji kutunzwa na kulelewa hata kama anafanya kazi mpaka pilipili unatakiwa kutoa wewe. Huwezi kushindana eti kwamba wewe umelipa kodi mwaka jana yeye alipe mwaka huu. Sisi ni walinzi, wahudumiaji wanawake wanatugemea sisi,” alisema Kipanya.

Kauli hiyo ya Kipanya imeonekana kama ahueni kwa wanawake akiwamo Rosina Tarimo aliyeeleza kwamba, anashangazwa na wanaume ambao hawataki kuwahudumia wapenzi wao.

“Haya ni maajabu inawezekana vipi wewe mwanaume una kazi halafu hutaki kumhudumia mwanamke wako, unataka ahudumiwe na nani. Eti asikuombe hela akamwombe nani sasa wakati wewe ndiye mtu wake anayekutegemea. Hii ni changamoto wanaume wetu sijui wametoa wapi tabia hizi,” alisema Rosina.

Naye Halima Bovu alieleza: “Iko wazi mwanamke anampenda mwanaume anayemjali kama hunijali basi nitakutana na mwingine, ambaye atanithamini na kujali mahitaji yangu. Hilo likitokea taratibu nitakusahau na kuhamia kwingine, au nitaendelea kuwa na wewe lakini nina mtu mwingine pembeni.

“Wanaume sasa hivi usipomuomba hela na yeye hakupi sasa utasubiri hadi lini aamue kukupa hela wakati una mahitaji ya kila siku tena ya muhimu, tukubali kuwa kuna shida kwa wanaume hasa hawa vijana wa kisasa”.


Wasemavyo washauri na wataalamu wa saikolojia

Mwanasaikolojia Modesta Kimonga alisema suala la wanaume kuwa wagumu kuwahudumia wenza wao linatokana na kufuata mkumbo ambao unatokana na mada zinazoibuka kwenye mitandao ya kijamii.

“Kisaikolojia na kisosholojia mwanamke ana hali fulani ya kuhitaji kupatiwa, hata kama anaweza kukipata kile kitu. Yaani, hiyo ni asili yake ila mambo yanabadilika kwa sababu siku hizi wanawake wanafanya kazi na wana kipato kikubwa.

Hata hivyo, hilo halimuondolei ile hali yake ya asili, hata hawa wanaume kusema kuwa hawataki kuombwa pesa ni kufuata mkumbo tu na taratibu mawazo hayo yanasambaa na kuingia kwenye jamii,” alisema.

Akizungumzia hilo mshauri wa uhusiano Deogratius Sukambi, alisema si kweli kuwa wanaume hawataki kuombwa pesa, changamoto ni wanawake kutanguliza pesa mbele kwenye uhusiano.

“Kuna shida moja ambayo inaweza kuwa chanzo cha yote haya, wanawake wa siku hizi wanapoingia kwenye uhusiano wamekuwa wakitanguliza mahitaji na shida zao. Wasichokijua ni kwamba wanaume ni wabinafsi na hilo ni asili kabisa.

“Anapotoa hela anataka kujua yeye atapata nini, sasa kama hujui mahitaji yake na ukamfanya yeye ajihisi mwanaume hapo ndipo atakapoona kero ukimuomba hela. “Mwanaume anapenda mamlaka yaani umheshimu na ajione yeye yuko juu, sasa wanawake wa siku hizi wanaweza kujibu vyovyote, kufanya chochote hapo mwanaume anarudi nyuma,” alisema Sukambi.

Mshauri huyo alieleza kuwa kisaikolojia wanaume wanapenda mamlaka lakini changamoto iliyopo kwa sasa ni kuzungukwa na wanawake ambao, hawataki kujishusha na wana nguvu kwenye maamuzi.

“Maisha wanayopitia wanaume wa miaka hii kuanzia makuzi hadi changamoto wanazokutana nazo zinawafanya kuwa na tatizo la kisaikolojia la kukosa hali ya kujiamini, sasa wanapopata wanawake ndio wanategemea waonyeshe mamlaka yao na wapate heshima sasa bahati mbaya akikutana na mwanamke wa sasa, ambaye hataki kushuka ndio tatizo lipo hapo,” alisema.


Athari ya hali hiyo

Sukambi alieleza kuwa mwanaume akiwa katika uhusiano na mwanamke anayekuwa juu yake, anaweza kupungukiwa na hali ya kujiamini na wakati mwingine kuamua kuacha kila kitu kiamuliwe na mwenza wake, kwa kuwa anahisi hata mawazo yake yanaweza yasiheshimike.

Kwa upande wa wanawake alisema kwa asili mwanamke ameumbwa kupokea, hivyo, anapokuwa na mwenza halafu akose huduma muhimu anapata msongo wa mawazo na kulazimika kujitafutia.

“Msongo wa mawazo kwa mwanamke unakuwa mara mbili, kwanza ile kutoka nyumbani kwenda kujitafutia, pili anapata msongo mwingine akiwaza huyu mwanaume anapeleka wapi pesa,’’ alisema.

Kwa maoni na ushauri kuhusu habari hizi katika ukurasa huu, tuandikie kupitia 0658 376 444.

Ingia Egazeti Kusoma Magazeti yote ya Kampuni ya Mwananchi  https://fupi.co.tz/VZmLChg

Mwananchi Jumamosi, Februari 6, 2021