Jinsi fundi simu alivyotekwa Kariakoo

Muktasari:

  • Hilo ni miongoni mwa matukio matano ya watu kutekwa na kutoweka katika mazingira ya kutatanisha.

Dar es Salaam. Zimepita siku 56 tangu Innocent Elias Liveti (34) maarufu Macheni, alipotekwa na watu wawili waliokuwa na gari ambalo hadi sasa halijatambuliwa karibu na duka lake la simu Kariakoo, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa mashuhuda na picha za video zilizochukuliwa na kamera za usalama, siku hiyo Desemba mosi, 2023, saa 1:30 asubuhi Liveti alikuwa amekaa mbele ya duka lake lililopo Mtaa wa Narung'ombe, ndipo ghafla walitokea watu wawili waliovalia kofia na kuondoka naye.

Tukio hilo ni miongoni mwa matukio matano ya watu kutekwa na kutoweka katika mazingira ya kutatanisha yaliyotokea mwaka 2023, likiwamo tukio la kutwakwa kwa mfanyabiashara, Mussa Mziba (37) aliyekuwa akimiliki kampuni ya Mziba Empire Investment Ltd yenye ofisi zake Mikocheni, Dar es Salaam.

Mziba alitekwa na watu wawili waliofika ofisini kwake saa 2 usiku, Desemba 7, 2023 wakijitambulisha kuwa ni maofisa  wa polisi.

Kutoweka kwa Mussa Mziba kumekuja sambamba na tukio la kupotea kwa watu watatu waliokuwa wakisafiri kutoka Mbeya kwenda Dar es Salaam ambao hawajulikani walipo mpaka sasa. Tukio hilo lilitokea Desemba 6, 2023.

Desemba 28, 2023 ndugu wawili mkoani Singida, Juma Iddi (45) na Haruna Iddi (50) waliotoweka, saa 10 jioni katika maeneo tofauti ya Mwenge na Mghanga, mjini Singida.

Matukio hayo yalitanguliwa na kutoweka kwa Charles Wetinyi aliyedaiwa kukamatwa na watu waliojitambulisha kuwa polisi, eneo la Mugumu wilayani Serengeti Mkoa wa Mara Oktoba 23, 2023.


Innocent alivyotekwa

Akizungumza na Mwananchi juzi Januari 23, 2024 mchumba wa Innocent, Janeth John (25) amesema mwenzi wake alipokea simu asubuhi ya Desemba mosi,2023 na alichokisikia kutoka kwake ni neno la “nakuja nipo njiani.”

"Alijiandaa kama kawaida yake kwa ajili ya kwenda kwenye shughuli zake Kariakoo, maana yeye ni fundi simu, lakini siku hiyo alipigiwa simu asubuhi na alisema anakwenda, lakini hadi leo hajarudi," amesema.

Amesema ilipofika saa 9 alasiri alimpigia simu, lakini haikupatikana na ndipo alipompigia rafiki yake ambaye yupo naye kwenye duka analofanyia kazi na ndipo alipoelezewa kuwa Innocent amekamatwa.

Amesema rafiki huyo alimwambia kuwa kwa mujibu wa mashuhuda walimuona Innocent amekamatwa na watu wawili na kuingizwa kwenye gari na kuhisi kuwa walikuwa ni polisi na alimfuatilia.

"Rafiki yake aliniambia walizunguka kwenye vituo vya karibu kumuangalia kama yupo lakini waliambiwa hakuna mtu huyo, ndipo nikaamua kumpigia simu dada yake," amesema Janeth.

Janeth amesema kwa mujibu wa CCTV camera, wakati watu hao walipokuja walikuwa wakibishana na Innocent, kabla ya kuondoka naye.

“Karibu na duka lake kuna saluni na pembeni kuna mama anayepika vitumbua, ndiye aliyesema aliwaona hao watu wakimchukua Innocent na kumwingiza kwenye gari, japo hawakujua ni gari aina gani,” amesema.

Amesema baadhi ya marafiki zake walizunguka vituo vya polisi bila mafanikio siku hiyo na kesho yake pia waliendelea kumtafuta kwenye vituo vya polisi.

“Ilipofika Jumanne Desemba 5, 2023 tukagawana, baadhi ya ndugu wakaenda hospitali na wengine kwenye vituo vya polisi vilivyobaki.

“Kuna baba yake mdogo alisema amesikia kuna miili miwili imeokotwa na polisi Malamba Mawili na mwili mmoja ni wa mtoto wao, basi tukaweka msiba tukidhani kuwa ni mwenyewe.

“Kesho yake baba wa Innocent, baba mdogo na ndugu wengine wakaenda Hospitali ya Mloganzila kuangalia hiyo miili, walipofika wakafanya ukaguzi, baba yake Innocent anamjua vizuri, kuna alama zake, wakagundua sio yeye,” amesema.

Amesema waliporudi nyumbani wakaitwa baadhi ya ndugu na kuwaabia mwili waliokwenda kuangalia si wa mtoto wao na ndipo msiba ukavunjwa.

Baada ya hapo amesema walirudi polisi na pia walikwenda Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na kufungua jalada lingine kwa ofisa upelelezi wa kanda hiyo.

Janeth anasema Innocent alishamtolea mahari na walipanga kufunga ndoa mwaka huu.


Baba afunguka

Akieleza jinsi walivyokwenda kumtambua mwili uliodaiwa kuwa wa mwanawe, baba mzazi wa Innocent, Elias Liveti amesema walikwenda Hospitali ya Mloganzila akiwa na polisi wawili kwa ajili ya kuthibitisha kama ni yeye.

Amesema walipofika huko walimkuta mtu anayefanana na mwanawe, lakini utofauti wake ni mwanya na nywele hivyo hakuwa mwanawe.

Baada ya kutoka huko anasema waliamua kufanya uchunguzi eneo la Kariakoo alipokamatiwa mtoto wake na ndipo walipobahatika kupata video za CCTV zikiwaonyesha watu waliomkamata mtoto wao.

"Zile video zinaonyesha kila kitu na tulipeleka hadi polisi na mmoja wa watu waliokuwa kwenye ile video mtu alikamatwa na kuhojiwa, lakini baadaye aliachiwa kwa dhamana," amesema.

Amesema mtu wanayemtuhumu kuwepo kwenye video anafahamika kwa jina (anamtaja) na kwamba ni mgambo wa Manzese, pia alikuwa na mwenzake.

Elias amesema licha ya watuhumiwa kuonekana kwenye CCTV camera na kufikisha ushahidi huo polisi, lakini hawapewi taarifa za kinachoendelea.

Naye mama mzazi wa Innocent, Leokadia Mihayo, amesema taarifa za kupotea mwanawe alizipata Desemba 2, 2023 alipokwenda kumtembelea mtoto wake wa kike na ndipo walipoamua kuzunguka katika vituo vya polisi kikiwepo Msimbazi, Sitakishari, Kituo kikuu (Central Police) na Oysterbay, lakini hawakumuona.

"Niliposikia hizo taarifa nilitaka kujua amefanya nini hadi akamatwe? Lakini hatujapata jibu hadi sasa," amesema.

Mama huyo anasema anajikuta akiishiwa nguvu kutokana na majibu yamayotolewa na polisi, kwani hajui wapi pa kumpata kijana wake.


Neno la Polisi

Akizungumza juzi na Mwananchi, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema jalada la kutekwa kwa Innocent lipo kituoni na linafanyiwa kazi.

"Tukipata taarifa za mtu kupotea au kutoonekana na sisi tunatoa taarifa kwenye vituo vyetu pamoja na ofisi za Serikali, ili kuweka wepesi wa kupatikana na mhusika," amesema Muliro.

Amesema matukio ya namna hiyo hayatakiwa kufanywa kwa kushinikizwa, kwani inaweza kuwa chanzo cha kutoa taarifa za uongo, hivyo wanafanya kazi kwa taratibu za sheria.