Jinsi Marekani inavyoficha mafuta yake katika mapango

Muktasari:
- Mtandao wa akiba ya mafuta hayo unasema kwamba hadi kufikia Septemba 13 nchi hiyo ilikuwa na mitungi milioni 644.8 ya mafuta ndani ya mapango hayo.
Washington, Marekani. Kufuatia mashambulio katika vituo vikuu vya mafuta Saudi Arabia, maafisa nchini Marekani wamekuwa wakizungumza kuhusu kutumia akiba kubwa ya mafuta iliyofichwa nchini humo.
Wakati bei ya mafuta ikipanda, Rais Donald Trump alituma ujumbe kwamba wanaweza kutumia mafuta waliyonayo kuhakikisha usambazaji upo sawa katika masoko.
Mafuta aliyokuwa akiyataja ni takriban mitungi milioni 640 iliyowekwa katika mapango ya chumvi ya chini katika majimbo ya Texas na Louisiana.
Inaelezwa kuwa wazo la kuweka akiba hiyo ya mafuta ilianza ilitokea katika miaka ya 1970 ambako washirika wote wa shirika la kimataifa la nishati walipaswa kuweka akiba iliyo sawa na mafuta yanayoweza kutumika kwa siku 90.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa akiba ya Marekani ndio iliyo kubwa ya dharura duniani kuliko washirika wengine wote.
Kwa mujibu wa Shirika la habari la BBC, wanasiasa wa Marekani walikuja na wazo hilo la kuweka akiba ya mafuta kwa mara ya kwanza katika miaka ya 1970 baada ya marufuku ya mafuta ya mataifa ya mashariki ya kati kuchangia bei kupanda sana kote duniani.
BBC inasema kuwa hata hivyo, washirika wa shirika la mataifa ya kiarabu yanayosafirisha mafuta zikiwamo Iran, Iraq, Kuwait, Qatar na Saudi Arabia yalikataa kuiuzia Marekani mafuta kwa sababu inaiunga Israel mkono katika vita kati ya mataifa ya kiarabu na Israeli mnamo 1973.
Ilisema kuwa vita hivyo vilidumu kwa wiki tatu hadi Oktoba lakini marufuku iliyoyalenga mataifa mengine pia iliendelea hadi Machi 1974 na kusababisha bei kupanda mara nne zaidi duniani kutoka dola tatu karibu Sh6,900 hadi 12 kwa pipa karibu Sh27,000.
Inaelezwa kuwa Bunge la Marekani lilipitisha Sheria ya sera ya nishati na uhifadhi ya 1975 Iliidhinisha akiba ya kimpango ya mafuta itakayotumika iwapo kutashuhudiwa tatizo jingine kubwa la usambazaji.
Akiba hiyo ni nini?
Kwa mujibu wa BBC, kufikia sasa kuna sehemu nne ambako mafuta yanahifadhiwa ikiwa ni pamoja na karibu na Freeport and Winnie jimboni Texas na nje ya Lake Charles na Baton Rouge, Louisiana.
Inaelezwa kuwa kila eneo lina mapango ya chumvi yalioundwa yalio na urefu wa kilomita moja kushuka chini ambako mafuta yanahifadhiwa na kwamba haigharimu pakubwa ikilinganisha na kuyahifadhi katika matanki juu ya ardhi na pia ni salama kemikali iliomo kwenye chumvi na shinikizo la chini ya ardhi linayazuia mafuta kutovuja.
Pia, eneo kubwa zaidi la Bryan Mound karibu na Freeport lina uwezo wa kuhifadhi takriban mitungi milioni 254 ya mafuta.
Mtandao wa akiba ya mafuta hayo unasema kwamba Septemba 13 kulikuwa na mitungi milioni 644.8 ya mafuta ndani ya mapango hayo.