Joe Biden rasmi Ikulu ajiandikia historia mpya Marekani kisiasa

Joe Biden rasmi Ikulu ajiandikia historia mpya Marekani kisiasa

Muktasari:

  • “Daima baba yangu alisema, kipimo cha mtu sio mara ngapi anapigwa chini, lakini anaamka haraka vipi.” Hiyo ni kauli ya Joe Bide ambaye amejaribu mara kadhaa bila mafanikio kuwania urais wa Marekani na sasa ni Rais wa 46 wa Taifa hilo kubwa duniani na anaapishwa leo.

“Daima baba yangu alisema, kipimo cha mtu sio mara ngapi anapigwa chini, lakini anaamka haraka vipi.” Hiyo ni kauli ya Joe Bide ambaye amejaribu mara kadhaa bila mafanikio kuwania urais wa Marekani na sasa ni Rais wa 46 wa Taifa hilo kubwa duniani na anaapishwa leo.

Joseph Robinette au Joe Biden Jr mwenye umri wa miaka 79, anakuwa Rais mzee zaidi katika historia ya siasa za Marekani, rekodi ambayo ilikuwa inashikiliwa na Rais wa 45 Donald Trump ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 75.

Biden ameshinda nafasi ya urais baada ya kujaribu mara tatu kugombea na baada ya kushindwa kupata uteuzi wa chama cha Democratic kuwania nafasi hiyo mwaka 1988 na 2008.

Hivi sasa ataongoza Serikali ya Marekani akishirikiana na makamu wake wa Rais ambaye ni Seneta wa California, Kamala Harris mwenye umri wa miaka 57, mwanamke wa kwanza katika historia ya miaka 244 ya nchi hiyo kuchaguliwa kushika wadhifa huo.

Safari ya kisiasa ya Biden ni ndefu, amekuwa makamu wa Rais wa Barack Obama kwa muda wake wote wa uongozi na wakati Obama alipomaliza muda wake wa uongozi alimtunuku Biden nishani ya Rais ya Uhuru.

“Kumjua Biden ni kujua upendo usio na ulaghai, huduma bila kujijali na kuishi maisha kikamilifu,” kauli aliyoitoa Rais Obama baada ya kustaafu urais wa Marekani.

Pia, baadhi ya wachambuzi wa siasa za Marekani wanamchukulia Biden kama mwanasiasa mwerevu, mwenye huruma na yuko tofauti kabisa na Rais Trump, aliyependa kumuita mpinzani wake kama “Joe anayejikongoja.”

Biden, anajulikana katika siasa za Marekani kwa karibu nusu karne na amehudumu kwenye Baraza la Seneti kwa miaka 36 na miaka minane kama makamu wa Rais, alitabiriwa mapema na baadhi ya vyombo vya habari vya Marekani kwamba angeibuka mshindi.

Biden, baada ya kauli mbiu ya Trump ya “America First” (Marekani Kwanza) iliyosababisha kuiondoa Marekani katika mikataba ya kimataifa, ameahidi kuirejesha kwenye ushirikiano na ulimwengu pamoja na mkataba wa kuidhibiti Iran kutengeneza silaha za nyuklia.

Pia, ilielezwa Biden atatia saini amri za kupinga uamuzi kadhaa uliotolewa na Donald Trump ukiwamo wa marufuku ya viza kwa nchi za Kiislamu na kujiondoa kwenye Mkataba wa Hali ya Hewa wa Paris baada tu ya kuingia ofisini.


Safari yake kisisa

Tangu 1973 hadi 2009, Biden alikuwa mbunge wa Senati ya Marekani akiwakilisha jimbo la Delaware. Kisha akawa Makamu wa Rais wa Marekani chini ya Rais Obama kuanzia 2009 hadi 2017, akiwa Mkatoliki wa kwanza na pia Mdelaware wa kwanza kuwa makamu wa Rais.

Ushindi wa Biden umekuja baada ya siku tano mfululizo za kuhesabu kura hali iliyoliweka Taifa la Marekani katika taharuki huku mpinzani wake Trump na wafuasi wake wakidai kuibiwa kura kwenye uchaguzi huo.

Biden hadi anaapishwa leo, amepitia kwenye changamoto nyingi toka kwa Trump kuliko hata uchaguzi wa mwaka 2000 katika jimbo la Florida.

Trump licha ya kushindwa, aliendelea kumpa kazi Biden ya kuliunganisha Taifa hilo, kwanza kufungua kesi mahakamani ya kupinga matokeo katika jimbo la Michigan ikiwamo kurudia kuhesabu kura katika jimbo la Georgia.

Lakini, pia Trump alizua sokomoko lingine kwa kuishambulia kwa maneno Mahakama Kuu kwa kukataa kesi yake ya kupinga ushindi wa Biden.

Kubwa zaidi ni pale wafuasi wake walipoamua kuvamia Bunge wakitaka kubadili matokeo ya uchaguzi wa rais wa Novemba 3, yaliompa ushindi Biden. Uvamizi huo ulichochewa na Rais Trump.

Hata hivyo, Biden anakuwa Rais wa Marekani ambaye uchaguzi wake umeweka rekodi kwa mambo mengi ikilinganishwa na vituko vilivyotokea kwenye uchaguzi wa 2000, wakati jimbo muhimu la Florida lilipogeuka kivutio kimataifa.

Hesabu za awali zilionyesha mgombea wa Democratic, Al Gore na mgombea wa Republican George W. Bush walipishana kura kidogo sana kiasi cha kumfanya Gore kuomba kura zihesabiwe upya na alielekea kushinda hadi kesi hiyo ilipofikishwa Mahakama Kuu ya Florida.

Hata hivyo, Trump bado hajaonyesha kukubali kushindwa na ametangaza kutohudhuria hafla ya kuapishwa Biden huku kukiwa na hofu ya kuzuka maandamano ya kupinga tukio hilo.

Pamoja na ubabe wa Trump, Katiba ya Marekani imeviweka huru vyombo vya usalama kuanzia jeshi, Idara maalumu ya ulinzi, CIA, FBI na wafanyakazi wote wa Ikulu.

Vyombo hivyo hufanya kazi na mtu anayeonekana kubeba matakwa ya watu kupitia sanduku la kura.

Mwaka 1801 Rais wa pili wa Marekani, John Adams alipokataa kukabidhi ofisi baada ya kushindwa kwenye uchaguzi na Thomas Jefferson, vyombo vya dola vilijitenga naye na vikaanza kumtii Rais mpya.

Wakati wa kumwapisha Jefferson, Rais Adams alisusa, lakini wafanyakazi wa Ikulu walitoa mizigo ya kiongozi huyo bila kusubiri maelekezo yake na waliingiza ile ya Jefferson.

Hivyo kwa Trump kususa kuapishwa kwa Biden hakutakuwa jambo jipya kwa Marekani na tayari imelezwa walinzi zaidi ya 20,000 wa kitaifa watalinda tukio hilo la kuapishwa na hatua za usalama zimepandishwa kwa kiwango cha juu.

Kupitia ujumbe aliochapisha kwenye akaunti yake rasmi ya mtandao wa kijamii wa Twitter, Trump amefafanua maswali kuhusu endapo atahudhuria hafla ya kuapishwa kwa Biden. Katika ujumbe wake amesema, “Kwa wale ambao bado hawafahamu, sitohudhuria hafla ya uapishaji itakayofanyika Januari 20.”

Kwa upande mwingine, Joe Biden, alitoa maoni yake juu ya Trump ya kutohudhuria hafla hiyo kwa kusema, “Ni jambo zuri kwamba hatokuja, ni aibu kwa nchi hii.”

Hata hivyo, Biden alisema kwamba watafurahi kumuona Makamu wa Rais Mike Pence na itakuwa heshima kubwa akihudhuria hafla hiyo.

Biden tayari ameonyesha msimamo wake kwa kusisitiza umoja na mshikamano kwa wananchi wa Marekani kwamba wana jukumu la dharura mbele yao kama vile kudhibiti janga la corona na kutoa msaada wa kiuchumi.