JPM kujengewa mnara shule aliyofundisha

JPM kujengewa mnara shule aliyofundisha

Muktasari:

  • Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Sengerema, Zakaria Kahema amesema shule hiyo inakusudia kutengeneza mnara wa kumbukumbu ya Hayati John Magufuli, aliyefundisha katika shule hiyo kati ya mwaka 1982 hadi 1983.

Sengerema. Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Sengerema, Zakaria Kahema amesema shule hiyo inakusudia kutengeneza mnara wa kumbukumbu ya Hayati John Magufuli, aliyefundisha katika shule hiyo kati ya mwaka 1982 hadi 1983.

Akizungumza juzi na waandishi wa habari wa Mwananchi shuleni hapo, Kahema alisema licha ya Magufuli kufundisha katika shule hiyo, pia alikuwa akiitembelea alipokuwa waziri na alitarajiwa kuwa mgeni kwenye kumbukizi ya miaka 50 ya shule hiyo.

“Magufuli alifika hapa Agosti 9, 1982 akiwa mwalimu wa hisabati na kemia na alifanya kazi hadi mwishoni mwa 1983. Katika kipindi chake cha uwaziri alikuwa akija hapa na aliwahi kuja kwenye mahafali akiwa naibu waziri na waziri,” alisema.

Akisimulia zaidi, Kahema alisema historia ya shule inamweleza Magufuli kama mwalimu aliyekuwa na bidii kuhakikisha wanafunzi wake wanafanya vizuri katika masomo yake.

“Kwa wanafunzi wasio na uwezo, yeye alikuwa akienda kwa mkuu wa shule na kuomba madaftari na kuwapa wanafunzi. Kwa wale waliokuwa wavivu alikuwa akiwabana sana kuandika notisi.

Alisema akiwa Rais, Magufuli aliiweka shule hiyo miongoni mwa shule kongwe zilizopewa fedha za ukarabati.

“Hii shule imejengwa mwaka 1972 ndipo ilipoanza kupokea wanafunzi, tangu wakati huo haikuwahi kufanyiwa ukarabati. Ilifika mahali shule hii iliharibika, ilikuwa imeezekwa na ‘asbestos’.

“Lakini baada ya utawala wake alipoamua kwamba shule zote kongwe zikarabatiwe, sisi tulipata bahati ya kuwa shule za kwanza. Tulipata Sh1.8 bilioni, kwanza kwenye majengo ya taaluma na baadaye majengo ya wafanyakazi,” alisema Kahema.

“Tulipopata taarifa ya msiba huu ulitushtua sana. Awali tulipanga kwenda Uwanja wa Kirumba lakini waliposema atapita hapa, tutashuka na wanafunzi na picha tuliyochora kwenye kitambaa ili kutoa heshima zetu za mwisho.

“Pia tunapanga kujenga mnara ambao tutachora picha yake na kuiweka mbele ya shule hii,” alisema Mwalimu Kahema.


Mwanafunzi achora picha ya Magufuli

Mwanafunzi wa kidato cha tano katika shule hiyo, Sylivester Matiku alikuwa amechora picha ya Magufuli kama zawadi kwake iliyokamilika saa chache kabla ya kutangaziwa kifo chake.

Mwanafunzi huyo amesema si rahisi kusahahu taarifa za kifo cha Magufuli.

Matiku amesema alitumia saa mbili kuchora picha akilenga kumpa mgeni rasmi atakayeshiriki mahafali ya kidato cha sita, akilenga kumuomba ampelekee Rais Magufuli kama zawadi kutoka kwake.

“Ni ndoto yangu nilikuwa natamani sana picha hii imfikie maana niliamini ataipenda. Mimi nimeanza kuchora toka zamani lakini sijionyeshi kwa watu ila muda wangu mwingi nautumia kwenye kuchora,” alisema Matiku.

Matiku anasema kipaji chake cha uchoraji ameanza akiwa shule ya msingi na hatua kubwa alifikia akiwa kidato cha tatu katika shule ya Kaizirege iliyopo Bukoba mkoani Kagera.

“Kwa hapa shuleni nilianza kuwachora wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi wa shule, baada ya hapo nikapata wazo la kumchora mgeni rasmi, lakini nikasikia ndani yangu nimchore Rais. Nikaomba ruhusa ya kwenda mjini nikaenda kuprint picha ya Magufuli ndio nikaja kuichora Machi 17 jioni.

JPM kujengewa mnara shule aliyofundisha

Mwananfunzi huyo ambaye ndoto yake ni kuja kuwa mchoraji mkubwa, anategemewa na shule kuchora picha kubwa itakayowekwa kwenye kioo na kuwekwa katika uwanja eneo la kuingia shuleni kama kumbukumbu ya kumuenzi Rais Magufuli.

Mzee Levi Ng’welu, mkazi wa Sengerema aliyefanya kazi na Magufuli katika vyama vya ushirika, alisema amepoteza rafiki mwema aliyekuwa na ushirikiano na wenzake.