Judestina Rwechunga Muuguzi aliyehudumia watoto na wajawazito kwa miaka 26

Bukoba. “Awali changamoto kubwa ilikuwa ni wajawazito na watoto kusumbuliwa na malaria yaliyokuwa yakisababisha vifo kwa watoto wachanga, lakini elimu imeanza kusaidia na vifo vinapungua,” anasema Judestina Rwechunga, ambaye ni muuguzi wa Kituo cha Afya Bwekerwa, akielezea safari yake ya miaka 26 akihudumia wajawazito na watoto na mapambano dhidi ya Malaria.

Anasema kwa sasa kuna dawa inayotumika kama kinga na tahadhari ya malaria kwa wajawazito iitwayo Sulfadoxine Pyremethamine (SP), ambayo kwa bahati mbaya wajawazito wengi hawapendi kuzitumia wakilalamika kuwa na maudhi ya hapa na pale, ikiwamo kulala sana na baadhi wakidai zinawafanya wajisikie kichefuchefu, lakini anajitahidi kuendelea kuwapa elimu kuhakikisha wanazitumia.

Anasema kitaalamu mjamzito anatakiwa kupata angalau dozi tatu za SP katika kipindi chote cha ujauzito, ya kwanza akipewa anapohudhuria kliniki wiki ya 14 ya umri wa ujauzito.

“Wajawazito wengi hawamalizi dozi tatu kama inavyoshauriwa kwa sababu ya kuchelewa kuanza kliniki na wengi hupata dozi moja au mbili na siku za kujifungua zinakuwa zimefika,” anasema.

Katika mahojiano maalumu na gazeti hili yaliyofanyika Kituo cha Afya Bwekera kilichopo Bukoba mjini mkoani Kagera, Judestina anayataja madhara anayoweza kupata mjamzito kwa kutotumia kinga hiyo, yakiwamo kupata upungufu wa damu, mtoto kuzaliwa akiwa na uzito pungufu, kujifungua kabla ya wakati, mtoto kuzaliwa akiwa na maambukizi ya malaria.  “Hali ya Malaria kwa sasa imepungua, mfano Aprili sijapata mjamzito hata mmoja hapa kituoni, Mei nilimpata mmoja,” anaeleza.

Safari ya Jusestina ilianzia hapa

Anasema tangu alipoanza kazi ya uuguzi miaka 26 iliyopita, amekuwa akihudumu katika kitengo cha wajawazito na watoto kwenye hospitali mbalimbali.

Safari ya uuguzi alianza Nzega, mkoani Tabora  mwaka 1997 baada ya kuhitimu mafunzo kwenye Chuo cha Uuguzi Nkinga, kabla ya kuhamia Bukoba, mkoani Kagera mwaka 2000 ambako ndiko alikozaliwa.

“Nilipomaliza  mafunzo ya uuguzi nikafanya kazi ya mkataba wa miaka mitatu kuanzia mwaka 1997 mpaka 2000, nikahamia Bukoba Manispaa. “Kwa muda wote huo nimekuwa nikifanya kazi katika vitengo vya wajawazito na watoto kwenye hospitali mbalimbali,” anasema Judestina.


Asiyoyasahau

Anasema jambo ambalo hatalisahau katika utendaji wake wa kazi ni  pale alipokutana kwa mara ya kwanza na  mjamzito aliyepata kifafa cha mimba. 

Judestina anasema akiwa anatekeleza majukumu yake ya kila siku alifika mjamzito kwenye kliniki yake kama kawaida. “Ajabu nilipompima presha ilikuwa juu imefika  200 kwa 110, halafu alikuwa amevimba mikono, uso na miguu. Ila mwenyewe alikuwa anachukulia kuvimba huko ni kawaida.

“Nilipompima mkojo pia ulikuwa  una protini nyingi, nikaanza kumuuliza anajisikiaje huku namuita mfamasia amletee dawa kwa ajili ya kushusha presha.

“Kabla hatujamaliza mahojiano akaanza kupata mtikisiko wa mwili (kutetemeka), nikamwita mwenzangu aje kunisaidia kuleta sindano na dawa nichanganye. Unachanganya na maji ya dripu na unachoma kwenye mishipa na baadaye unamchoma kwenye msuli ukichanganya na dawa za ganzi ili kupunguza maumivu.

“Yule mama nilipomchoma tu akasema mwili mzima unamuuma na akawa anapiga kelele ya maumivu, huku natakiwa nimfanyie vitu vingine, ikiwamo kumuwekea ‘katheta’ na niite  gari ya wagonjwa kwa ajili ya kumpeleka hospitali kubwa kwa matibabu zaidi maana hapa kwetu hatulazi.

“Ilikuwa kazi ya dakika chache, lakini yenye hekaheka nyingi. Nilipompeleka hospitali ya Serikali nikiendesha gari mimi mwenyewe baada ya kupiga simu ya kuita gari na kutoridhika na majibu niliyopata, wenzangu pale hospitali nawashukuru walimpokea na kumpa huduma, kwani nilikuwa nimeshaanza kumpa kabla ya kumpeleka.”

Anafafanua kwa mjamzito presha haitakiwi kuzidi 140 kwa 90, ikifika hapo inakuwa mbaya, mbali na hilo hata anapohisi au kuumwa  kichwa hii ni ishara ya hatari  ya kwanza. “Asipochukua  hatua anapata kama degedege, kifafa cha mimba, wengine mpaka wanazimia ingawa huyu hakuzimia. Wajawazito wanapofika kliniki nawafundisha na naamini hospitali zote wanafundishwa dalili za hatari.”

Kuhusu kuwepo protini kwenye mkojo, Judestina anasema haitakiwi kabisa, kwani ikiwepo inaashiria hatari ya kifafa cha mimba, kuvimba uso, mikono na miguu, pia inaambatana na presha kupanda na kuumwa kichwa.

“Ingawa mjamzito anapovimba miguu miezi minane mpaka tisa kwa sababu kichwa cha mtoto kikishuka kinakandamizi mishipa inayosambaza damu huku chini mpaka miguuni, hivyo anaelemewa na uzito na miguu inavimba.

“Ndiyo maana tunawashauri wajawazito, mimba ikifika umri huo mara nyingi wakae chini huku wamenyoosha miguu ili ipungue kuvimba, lakini ukivimba na ukibonyeza inabaki alama, hiyo ni dalili hatari kwa mjamzito,” anashauri Judestina.

Anazitaja dalili za hatari ambazo mjamzito anapaswa kuwa nazo makini kuwa ni maumivu makali ya kichwa, kushindwa kuona vizuri, kupata degedege, maumivu makali ya tumbo, mtoto kupunguza au kuacha kucheza, kutokwa damu au maji mengi ukeni na kupata kizunguzungu au homa.

Judestina analitaja jambo lingine asilolisahau katika safari yake ya uuguzi ya miaka zaidi ya 20 ni mjamzito aliyekunywa dawa za kienyeji na kusukuma mtoto kabla njia haijafunguka.

Anasema akiwa  kituo cha Buhembe, ndani ya Manispaa ya Bukoba kama kilomita nane kutoka Bukoba mjini, siku moja usiku alipata mjamzito aliyeonekana alitumia dawa za kienyeji za kuongeza uchungu.

“Nilibaini hivyo baada ya mjamzito huyo kulalamika kupata uchungu mkali, ilihali njia haijafunguka lakini yeye analazimisha kusukuma.

“Alichokuwa anafanya ni sawa na dawa ya meno, unalazimisha kuitoa huku umeifunika, hivyo ukiendelea kulazimisha itapasuka,” anaeleza.

Anasema licha ya kumwambia njia bado haijafunguka, kwa maumivu aliendelea kusukuma mpaka mdomo wa kizazi ukachanika.

“Alipokuwa akilalamika nilianza kumuandaa kwa kumuwekea kanyula ya kuchomea sindano.  Kwa sababu nimemuwekea sehemu ya kuwekea dripu nikamuita mlinzi aniitie nesi niliyekuwa naye kituoni, huku damu inatoka nyingi, yaani ni kutungua chupa ya damu na kupandisha nyingine ili angalau kumnusuru,” anasema.

Muuguzi huyo anasema wakati mama analalamika kuwa anakufa na kumuacha mwanae, aliendelea kupambana kuokoa maisha yake.

Anasema nesi alipofika kazi yake kubadili chupa za damu, akachukua simu akapiga manispaa ili wamlete gari ya wagonjwa, simu ikawa haipatikani, akiangalia hakuna muda wa kupoteza mgonjwa anahitaji kufika kwenye hospitali yenye vifaa zaidi tofauti na hapo kituoni.

“Uzuri siku hiyo nilikuwa nimekwenda na usafiri, nikampakia mgonjwa nyuma akiwa na nesi ambaye jukumu lake lilikuwa kushikilia chupa ya damu na kuibadili ikiisha, kwani ilikuwa tukiitundika ni kuifungua ishuke kunusuru iliyokuwa ikitoka kwa wingi. Yule mama alikuwa anaendelea kulalamika maumivu,” anaeleza.

Anasema alikuwa anaendesha gari huku akiwa na mipira ya mikono aliyoivaa wakati wa kumuuguza, alibaini hilo baada ya kufika hospitali.

Anafafanua kuwa alipomfikisha hospita ya mkoa walimpokea kwa sababu alikuwa amemuandaa kwa ajili ya huduma na ndiyo jambo wanalosisitiza kuliko kumpeleka tu akiwa katika hali mbaya na bila kuchukua hatua yoyote.

Anasema baada ya kupokelewa alishonwa kwa saa mbili kutokana na eneo lililochanika kuwa kama ini, ukipitisha sindano inavuja, baadaye wakafanikiwa wakamlaza  na baada ya siku tatu akaruhusiwa.

Alisema huwa wanatoa elimu kukemea matumizi ya dawa za kienyeji.


Kitu kinachomfurahisha

Anasema jambo linalomfurahisha kwenye kazi ni anapomzalisha mjamzito. “Nafurahi mtoto anavyotoka, anavyolia na mama anavyokuwa na furaha ya kumpokea mwanaye,” anasema.


Imeandaliwa kwa msaada wa Bill & Melinda Gates