Jukwaa la Wahariri Tanzania lawafariji waathirika Kilosa
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka akipokea msaada kutoka kwa Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Jane Mihanji kwa ajili ya waathirika wa mafuriko yaliyotokea wilayani Kilosa.
Muktasari:
- Msaada huo ni ishara ya wahariri walivyoguswa na matatizo yaliyowapata wakazi wa Kilosa.
Morogoro.Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), leo Alhamisi Januari 18, 2024 limekabidhi msaada kwa waathirika wa mafuriko wilayani Kilosa mkoani Morogoro yaliyotokea hivi karibuni.
Msaada hiyo ni vyakula na nguo za watoto na watu wazima umewasilishwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa hilo, Jane Mihanji, kwa niaba ya Mwenyekiti, Deodatus Balile kwa Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka.
Akikabidhi msaada huo, Mihanji amesema umetokana na kuguswa kwao na janga hilo lililoleta athari kubwa kwa wakazi wa Kilosa.
Amesema licha ya kufanya kazi ya kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha jamii, wao ni sehemu ya jamii hivyo wameguswa na majanga ya asili yaliyowakuta Watanzania wenzao na wameachangishana fedha walizonunua vitu na kuviwasilisha kwa viongozi kwa ajili ya kuvifikisha kwa walengwa.
Akipokea msaada huo, Shaka kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, ameishukuru TEF kwa kujitoa kwao.
Shaka ameomba ushirikiano kati ya TEF na Serikali udumishwe, huku akiwahakikishia wahariri hao kuwa msaada huo utafika kwa walengwa kama ilivyokusudiwa.
Shaka amesema jamii wilayani Kilosa inatoa shukrani za dhati kwa wadau waliowafariji waathirika kwani kutoa ni moyo, si utajiri.
TEF iliwakilishwa na Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu, Anita Mendoza; Mjumbe Kamati ya Utendaji Jane Mihanji na Mjumbe Rashid Mtagaluka.