Jumuiya Afrika Mashariki yazindua kampeni kuhamasisha utalii wa ndani

Muktasari:

  • Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) imezindua kampeni ya kuhamasisha utalii wa ndani kwa nchi sita wanachama ijulikanayo kama tembea nyumbani.


Arusha. Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) imezindua kampeni ya kuhamasisha utalii wa ndani kwa nchi sita wanachama ijulikanayo kama tembea nyumbani.

Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Dk Peter Mathuki amesema wamezindua kampeni hiyo ikiwa ni sehemu ya kuokoa sekta ya utalii ambayo imeathiriwa na ugonjwa wa Uviko-19.

Amesema katika nchi za EAC utalii ni moja ya sekta muhimu katika kukuza uchumi kwani unachangia asilimia 10 ya mapato, asilimia 10 ajira na asilimia 17 ya fedha za kigeni .

"Sisi Kama EAC tumeamua kuzindua kampeni hii kuanzia Desemba Mosi hadi 22 kuwashawishi wakazi wa Afrika Mashariki kutembelea hifadhi za wanyama badala ya kutegemea watalii kutoka nje ya EAC" amesema

Amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezwaji wa mpango mkakati wa kukuza utalii katika Ukanda wa Afrika ya Mashariki ambao unafadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ).

Mkurugenzi wa sekta ya uzalishaji katika jumuiya ya Afrika ya Mashariki, Jean Havugimana amesema katika kampeni hiyo watashirikiana na Bodi za Utalii katika nchi wanachama na wadau wengine.