JWTZ kushiriki mazoezi ya utayari majeshi ya EAC

Mkuu wa Kamandi ya Nchi Kavu ya JWTZ, Meja Jenerali Anthony Sibuti (kushoto) akikabidhi Bendera ya Taifa kwa Luteni Kanali Lucas Ryoba ambaye ni kiongozi wa kikosi cha Tanzania kinachoenda nchini Uganda kushiriki mazoezi ya pamoja ya majeshi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC. Wengine pichani kushoto ni askari wa kikosi cha bendara. Picha na Peter Saramba.
Muktasari:
Pamoja na utayari wa operesheni za kijeshi, kukabiliana na vitendo vya kigaidi, majang na uharamia baharini, mazoezi ya pamoja pia yanalenga kuyaandaa majeshi ya nchi wanachama wa EAC kudhibiti machafuko na kulinda amani ndani ya nchi wanachama.
Mwanza. Timu ya washiriki 299 wakiwemo askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Polisi, Magereza, Uhamiaji na kikosi cha Zimamoto na Uokoaji inaondoka nchini kuanzia leo Mei 24 kwenda nchini Uganda kushiriki mazoezi ya pamoja ya utayari ya majeshi ya Jumuiya ya Afrika Mashiriki (EAC).
Mazoezi hayo ya wiki mbili ya kila mwaka yanayojulikana kwa jina la “Zoezi la Ushirikiano Imara” yanayotarajiwa kuanza Mei 28 pia yatashirikisha maofisa kutoka Ofisi ya Rais, Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa hafla fupi ya kukabidhi Bendera ya Taifa iliyofanyika jijini Mwanza leo Jumanne Mei 24, Mkuu wa Kikosi cha Tanzania kinachoenda kushiriki mazoezi hayo, Brigedia Jeneralli Charles Ndwege amesema mazoezi hayo yatahusisha operesheni za ulinzi wa amani, kukabiliana na majanga, ugaidi na uharamia baharini.
“Washiriki pia watanolewa kuhusu sheria za kimataifa katika operesheni za ulinzi na amani,” amesema Brigedia Jeneralli Ndwege
Pamoja na Tanzania, washiriki wengine wanatoka nchi za Sudan Kusini, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi huku nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) iliyojiunga EAC mwaka huu itashiriki kama mtazamani hadi mwakani watakapokuwa tayari.
Awali akikabidhi bendera ya Taifa kwa kiongozi wa kikosi cha Tanzania, Luteni Kanali Lucas Ryoba, Mkuu wa Kamandi ya Nchi Kavu ya JWTZ, Meja Jenerali Anthony Sibuti amewataka washiriki kutoka Tanzania kuonyesha weledi na nidhamu ili kuwa mfano bora kwa wenzao kutoka nchi nyingine.
“Mkaimarishe ushirikiano miongoni mwenu wenyewe kwa wenyewe na kwa washiriki wenzanu kutoka mataifa mengine huku mkijifunza kutoka kwao, nao wakijifunza kutoka kwenu.” ameasa Meja Jenerali Anthony Sibuti