Kagera yaongoza watu wenye ugonjwa wa selimundu

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Mtandao Wanaopambana na Ugonjwa wa Selimundu Tanzania (Tanscda) umeitaja mikoa ya kanda ya ziwa kuwa na watu wengi wenye vinasaba vya ugonjwa wa selimundu huku Mkoa wa Kagera ukiripotiwa kuongoza kwa kuwa na asilimia 22.99.

Dodoma. Mtandao wa Wanaopambana na Ugonjwa wa Selimundu Tanzania (Tanscda) umeitaja mikoa ya kanda ya ziwa kuwa na watu wengi wenye vinasaba vya ugonjwa wa selimundu huku Mkoa wa Kagera ukiripotiwa kuongoza kwa kuwa na asilimia 22.99.

Mikoa mingine inayoongoza na asilimia zake katika mabano ni Mwanza (21.11), Mara (21.10), Mara (21.10), Shinyanga (19.90) na Geita (16.96).

Mtendaji Mkuu wa mtandao huo Dk Deogratias Soka ameyasema hayo leo Jumanne, Desemba 7, 2021 wakati walipokutana na wadau wa kampeni ya vunja mduara inayolenga kupunguza idadi ya wanaougua ugonjwa huo.

Dk Soka amesema lengo la kukutana ni kutoa ripoti ya utekelezaji wa kampeni hiyo iliyofanyika 13 nchini.

Amesema kampeni hiyo inalenga kupunguza idadi ya watoto wanaozaliwa na ugonjwa wa selimundu nchini ambapo takwimu zinaonyesha watoto 11,000 wanazaliwa kila mwaka na ugonjwa huo.

Amesema Tanzania ni nchi ya nne kwa kuwa na wagonjwa wa selimundu wengi duniani ikizifuatia nchi za India, Nigeria na Congo.

Dk Soko amesema ugonjwa huo umekuwa unachangia vifo vya watoto wadogo chini ya miaka tano kwa asilimia saba yaani vifo vinne kwa kila vifo 1000 vinatokana na ugonjwa huo.

“Tuliona tuje na huu mpango wa kupunguza vifo vya selimundu kwa kutoa elimu. Cha muhimu ni namna gani tunaweza kupunguza tatizo la selimundu ama kujikinga. Sehemu ya pili ni kuwapima pia kugundua kama wanavinasaba vya ugonjwa huu,”amesema.

Amesema asilimia 15 hadi 20 ya watanzania sawa na zaidi ya watu milioni tano wakadiriwa kuwa na vinasaba vya ugonjwa huo.

Hata hivyo, Dk Soko amesisitiza kuwa na vinasaba haimaanishi unaumwa ugonjwa huo lakini kuna unauwezekano mkubwa kupata mtoto mwenye ugonjwa wa selimundu iwapo mtu huyo atazaa na mwenza mwenye vinasaba vya ugonjwa huo.

Amesema njia pekee ya kuepuka kupata watoto wenye ugonjwa huo ni kuhakikisha watu wanapima na kufahamu kuhusu hali ya vinasaba hivyo.