Kaka adaiwa kumuua mdogo wake kwa kufeli mtihani

Kaka adaiwa kumuua mdogo wake kwa kufeli mtihani

Muktasari:

  • Mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya msingi Shibutwa wilayani Mbogwe mkoani Geita, Ziada Masumbuko (15) ameuawa kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali kichwani na kaka yake kwa kile kinachodaiwa ni baada ya kufanya vibaya katika mtihani wa majaribio.

Geita. Mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya msingi Shibutwa wilayani Mbogwe mkoani Geita, Ziada Masumbuko (15) ameuawa kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali kichwani na kaka yake kwa kile kinachodaiwa ni baada ya kufanya vibaya katika mtihani wa majaribio.

Kamanda wa polisi mkoani Geita, Hendry Mwaibambe amethibitisha kutokea kwa tukio lililotokea mwishoni mwa wiki katika kijiji cha Shibutwe kata ya Bunigonzi wilayani Mbogwe mkoani hapa.

Akielezea tukio hilo, kamanda Mwaibambe alisema kaka wa mwanafunzi huyo aliyefahamikakwa jina la Viaga Masumbuko (29) alimpiga mdogo wake kama kumwadhibu baada ya kufanya vibaya mtihani, hali iliyosababisha mtoto huyo kufikwa na mauti.

Kwa mujibu wa kamanda, mtuhumiwa anadaiwa kumpiga mdogo wake mara kwa mara anapofanya vibaya darasani, kitendo ambacho walimu wa mwanafunzi huyo wamekuwa wakimsihi kuacha tabia hiyo bila mafanikio.

Kamanda alidai mwili wa mwanafunzi huyo umekutwa na majeruhi maeneo ya mikononi, mabegani na miguuni na kwamba mtuhumiwa anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za mauaji.

Katika tukio jingine, mwanafunzi Method Hassan (12) wa darasa la saba katika shule ya msingi Kalangalala iliyopo mjini Geita ameuawa kwa kupigwa mateke na ngumi akituhumiwa kuiba Sh15,000 kwenye duka lililopo jirani na nyumba yao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Henry Mwaibambe alisema tukio hilo lilitokea April 7 wakati mtoto huyo akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Geita.

Akielezea tukio hilo, bibi wa mtoto huyo, Grace Mathias alisema siku hiyo akiwa nyumbani saa moja asubuhi aligongewa mlang na watoto wake wanaolala chumba cha nje na alipotoka alimkuta mjukuu wake akiwa na majeraha na alipowahoji walidai amepigwa na muuza duka aliyeko jirani na nyumba yao.

“Wanadai alikuja kuwagongea asubuhi akamuita Method na kwa kuwa ana tabia ya kumtuma alitoka ndio akamtuhumu amemuibia hela. Alimfungia stoo na kumpiga na hata nilipomwambia tumpeleke hospitali hakunijibu kitu hadi mtoto wangu mwingine alipokuja wakataka kupigana ndio akatoroka,”alisema Grace.

Alisema alimpeleka mjukuu wake polisi na badaye hospitali na kufikwa na mauti wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Geita.