Kamanda Misime akazia usalimishaji silaha

Muktasari:

  • Misime ataka watu kurejesha silaha wanazomiliki kinyume na sheria kwa sababu hawataguswa na mkono wa dola.

Kibaha. Zoezi la usalimishaji wa silaha mbalimbali za moto kwa hiyari linalofanyika nchi nzima limeonyesha kufanikiwa baada ya takwimu za silaha zinazosalimishwa maeneo mbalimbali kuongezeka kutoka silaha 228 mwaka 2021 hadi silaha 1,220 mwaka 2022.

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishina Msaidizi Mwandamizi David Misime, ameyasema hayo leo Alhamisi Oktoba 12, 2023; akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Pwani, iliyolenga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu usalimishaji wa silaha kwa hiari.

Amesema Mkoa wa Pwani ni miongoni mwa mikoa ambayo ilifanya vizuri kipindi hicho ambapo eneo hilo pekee ziliwasilishwa silaha 111 kati ya hizo 1,220.

Misime ameongeza kuwa ziara yake mkoani Pwani ni kuendeleza kampeni hiyo ambayo mkoa huo umeonyesha kufanikiwa na kutolea mfano katika kipindi hiki kifupi tu mwaka huu toka kampeni ianze Septemba Mosi, tayari silaha 11 zimekwisha wasilishwa.

"Mwezi wa kampeni ya uwasilishaji silaha kwa hiari ambayo ilianza Septemba Mosi, utamalizika Oktoba 31, 2023; katika kipindi hiki kila mtu anayemiliki silaha kinyume na sheria anatakiwa kusalimisha kwa hiari na atakwepa kukamatwa kufikishwa mahakamani na pia anakua huru kwa kuendelea na shughuli zake za kujiletea maendeleo," amesema Misime.

Hivyo Kamanda huyo amewataka Polisi Kata kushirikiana na viongozi mbalimbali walioko kwenye maeneo yao katika kuhamasisha wananchi wanao miliki silaha kinyume cha sheria kuzisalimisha kwa hiari.

"Nasisitiza sana wananchi wanaoishi maeneo ya hifadhi (misitu) ya wanyama kuhakikisha wanarejesha silaha walizonazo ikiwemo Ngorongoro, Mikumi na, Serengeti.

Zoezi la usalimishaji wa silaha litafika ukomo Oktoba 31 mwaka huu ambapo amelekeza Polisi Kata nchini kote kutumia muda mchache uliosalia kutoa elimu na kuwahamasisha wananchi wenye kumiliki silaha kinyume na sheria za nchi, kuzisalimisha.

"Nawapongeza Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kwa kuwa miongoni mwa mikoa inayofanya vizuri kwenye zoezi hili, mfano Wilaya ya Kipolisi Chalinze ambapo idadi ya silaha 11 zimekwishasalimishwa tangu zoezi hilo lilipoanza mwezi huu uliopita," amesema Misime.

Awali Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani Pius Lutumo amesema hasara za kutosalimisha silaha katika kipindi hiki ni pamoja na kukamatwa, kufikishwa mahakamani na ukipatikana na hatia kifungo chake ni miaka 15 au faini ya sh. 10 Milioni.

Mmoja wa wakazi wa Chalinze Seifu Ally amesema utaratibu huo ni mzuri na kuomba wengine kutii sheria bila shuruti.