Kamanda Muliro: Boni Yai, Malisa hawakingwi na sheria

Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam, SACP, Jumanne Muliro katika moja ya tukio akizungumza na waandishi wa habari. Picha na mtandao

Muktasari:

Asema kutoa taarifa za uongo ni kosa kisheria na hawawezi kukingwa na sheria ya kwamba ni watoa taarifa.

Dar es Salaam. Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema sheria ya watoa taarifa kulindwa,  haimaanishi watu kujikite kutoa za uongo, huku wakidai walindwe.

Kamanda Muliro ametoa kauli hiyo leo Aprili 28, 2024 alipotoa elimu kwa umma akijibu kilichoelezwa na Meya wa zamani wa Ubungo, Boniface Jacob maarufu Boni Yai na mwanaharakati Godlisen Malisa.

Baada ya wawili hao kuachiwa kutoka rumande jana Aprili 27, 2024, walitoa ujumbe kwa Jeshi la Polisi wakieleza watoa taarifa walipaswa kulindwa na si kupambana nao kwa kuwashikilia.

“Tuna sheria ya kuwalinda watoa taarifa. Watoa taarifa si wahalifu ila ni watu wenye nia njema kwenye nchi na kwa jamii na kulisaidia Jeshi la Polisi, wakitumiwa vizuri wanaweza kufanya kazi zao vizuri bila kuingia mgogoro au msuguano,” alisema Malisa.

Jacob naye alisema: “Hatutaacha kupigania matukio ya watu kupotea na kutekwa hatutaki kumuonea mtu, tumehojiwa kwa hiyo sitegemei kama Jeshi la Polisi kutuona sisi maadui zao, watuone marafiki namna gani kuhakikisha watu hawapotei na wale wanaopotea wanapatikana.”

Jacob  na Malisa walishikiliwa kwa siku tatu wakihojiwa kwa tuhuma za uchochezi kwa kuchapisha taarifa kwenye mitandao ya kijamii,  kuwa Jeshi la Polisi linaua raia wakilihusisha na taarifa za kifo cha Robert Mushi maarufu Baba G.

Polisi ilieleza taarifa hizo ni za uongo na zililenga kuchochea chuki kati ya jamii dhidi ya taasisi hiyo na kwamba, Mushi alifariki dunia kwa ajali ya barabarani.

Kutokana na taarifa hizo, Polisi iliwaita Boniface na Malisa kuhojiwa Kituo cha Polisi Mkoa wa Kinondoni cha Oysterbay ambako walielekezwa kwenda Kituo Kikuu cha Polisi cha Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.


Ufafanuzi wa Muliro

Akizungumza na Mwananchi leo Aprili 28, 2024 Kamanda Muliro amesema huwezi kutumia haki ya kutoa taarifa kwa kuibuka tu hata kama Katiba inaeleza kila mtu ana haki ya kusema chochote ilimradi asivunje sheria za nchi.

“Hatutaki mtu unaibuka tu na kusema lolote kwa kigezo cha haki yangu ya kikatiba. Mtoa taarifa za kweli huwa hazibamizi ‘paaapu’ mara nyingi taarifa za ukweli unatakiwa kulindwa, sasa utalindwaje wakati mwenyewe umeshajiweka wazi kwa umma,” amehoji Kamanda Muliro.

Amesema: “Kwamba mimi mtoa taarifa lazima nilindwe, utalindwaje wakati umeshajitangaza. Tafsiri ya sheria hiyo haikumaanisha hivyo, ndiyo maana kwenye somo la sheria kuna sehemu inaeleza kwa nini sheria inatungwa.”

Katika maelezo yake ametoa mfano kama watu wanavyotaka kuandamana pamoja na kwamba sheria inaruhusu, huwezi kutumia fursa hiyo kila siku kuandamana na kuzuia watu wengine wasifanye shughuli zao.

“Ina maana watu wasiende hospitali au kwenye kazi ambayo ni haki vilevile ya kikatiba, watu wasiende shule ambayo ni haki vilevile kwa hiyo wakalie haki yako wewe ya kuandamana. Sheria inakupa haki mkono wa kulia lakini inakupa utaratibu mkono wa kushoto, ili ufurahie haki yako unatakiwa kwenda kwa mfumo huu,” amesema.

Kamanda Muliro amesema kutoa taarifa za uongo ni kosa kisheria na hawawezi kukingwa na sheria ya kwamba ni mtoa taarifa.

“Huwezi kuamka tu na kusema huyu mwizi ukiamini sheria ya kutoa taarifa itakulinda, haipo hiyo. Sheria ya kutoa taarifa itawalinda watu wanaoamini taarifa wanazozitoa ni za ukweli lakini huwezi kujenga tabia ya kutoa taarifa za uongo kila siku halafu uhitajike kulindwa na sheria,” amesema Kamanda Muliro.


Makosa ya Jacob, Malisa

Kwa mujibu wa Kamanda Muliro Jacob na Malisa wamekuwa wakiandika taarifa moja kwa moja kwenye mitandao na kutoa hitimisho,  bila kujua na kutambua kuna vyombo vya kisheria vilivyopewa mamlaka ya kufanya kazi hiyo.

“Sisi tunashirikiana na watoa taarifa lakini staili ya Boniface na Malisa wale si watoa taarifa, mfumo ule ni kushambulia Polisi waua,” amesema.

Kamanda Muliro amesema wamekuwa wakishirikiana na watoa taarifa ndiyo maana katika operesheni zao wamekuwa wakifanikiwa, akiwatuhumu Jacob na Malisa kuvuka mipaka.

“Taarifa ukishaichapisha mtandaoni na kuweka hitimisho kule si kutoa taarifa, hiyo sasa inakuwa ripoti na inategeneza chuki kwa taasisi na jamii,” amesema.


Akumbushia tukio la Babati

Kamanda Muliro amesema wamekuwa wakifanya operesheni mitandaoni na walibaini wawili hao wamekuwa vinara, akitoa  mfano kuna tukio lililotokea Babati, Manyara na watu waliiba sehemu hiyo wakaandika: “Polisi waua wapora.”

Amesema baada ya upelelezi wa tukio hilo walibaini ilikuwa ajali iliyotokea mchana na mtu aliyekuwa anaendesha gari alikuwa amelewa.

“Tulipeleleza na kuwajua walioiba mali, alianza Malisa kuchapisha na Boniface aliunga mkono, kwa hiyo imekuwa tabia yao ya kuandika habari za uongo  za kulishambulia Jeshi la Polisi,” amedai akisema huwa wanaweka kumbukumbu.

Kamanda Muliro amesema wana ushahidi wa kumbukumbu na kwamba, katika kuwahoji walikuwa wanazingatia ukweli.

“Hatuwezi kupambana na watoa taarifa, Jeshi haliwezi kupiga hatua bila watoa taarifa, lakini Jeshi haliwezi kuwafurahia watoa taarifa wahuni,” amesema.