Kamati kuu ya Chadema kukutana Mei 4

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe

Muktasari:

  • Wagombea wa nafasi mbalimbali ndani ya Chadema wanatarajiwa kuitwa kuanzia Mei 4 mbele ya kamati kuu kwa ajili ya usaili wa nafasi walizoomba

Dar es Salaam. Vigogo wa Chadema wanatarajia kujifungia katika kikao cha kamati kuu kinachotarajiwa kufanyika Mei 4 kikiwa na ajenda mbalimbali ikiwamo ya uchaguzi wa ndani wa chama hicho.

Ajenda nyingine zitakazojadiliwa na vigogo hao ni tathimini ya wiki wa maandamano ya amani yaliyoingia siku ya saba leo, yenye lengo la kufikisha kilio cha wananchi kuhusu ugumu wa maisha, madai ya Katiba mpya na kupata Tume Huru ya Uchaguzi.

Maandamano hayo yaliyoanza Aprili 22, 2024, yanaongozwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na makamu wake, Tanzania Bara, Tundu Lissu wakiwa wamegawana mikoa tofauti.

Katika maandamano hayo yaliyofanyika Mwanza, Kagera, Simiyu, Geita, Shinyanga, Kilimanjaro na Dodoma, masuala ya ugumu wa maisha, upatikanaji wa Katiba mpya na marekebisho ya mifumo ya uchaguzi ni miongoni mwa mambo yaliyotawala.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani ambazo Mwananchi imezipata, kikao hicho kitakachofanyika Dar es Salaam, kwa siku mbili, huenda kikachukua muda zaidi kulingana na idadi ya wagombea wa nafasi mbalimbali ikiwamo uenyekiti wa kanda watakaoitwa kwa ajili ya usaili wa nafasi walizoomba.

Chanzo hicho cha habari kinaeleza fomu za majina ya wagombea wa nafasi mbalimbali zikiwamo za uenyekiti na umakamu wa kanda zimetumwa kwa ajili ya hatua zaidi za kuelekea kwenye mchakato huo.

Leo Jumanne Aprili 30, 2024 Mwananchi Digital lilimtafuta Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema kujua kuhusu kikao hicho,  alijibu yupo ‘busy’ (kazi nyingi) na kikao kingine atafutwe baadaye.

“Nitafute baadaye nipo katika sekretarieti kwa sasa,” amesema Mrema.

Hata hivyo, kikao hicho cha sekretarieti ni maandalizi ya kufanyika kwa kikao cha kamati kuu ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

Baadaye alipotafutwa tena Mrema alijibu kuwa, “bado hatujapanga tarehe, lakini kikao (kamati kuu) kitafanyika…” amesema.

Katika kikao hicho cha kamati kuu, wajumbe watawaita vigogo waliojitokeza kuwania uenyekiti, umakamu mwenyekiti wa kanda na wahazini, kuwahoji kisha kuwapitisha ili kuanza kampeni za uchaguzi huo, utakaopangiwa tarehe na kikao hicho.

Vigogo 13 wamejitosa kuwania uenyekiti katika kanda nne kati ya 10 za Chadema, hivi sasa wanasubiri usaili ili kuteuliwa na kamati kuu baada ya mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu kukamilika.

Kanda hizo ni Victoria, Magharibi, Nyasa na Serengeti zinazounda mikoa ya Mwanza, Geita, Kagera, Mara, Simiyu, Iringa, Mbeya, Njombe, Songwe, Rukwa na Shinyanga.

Kanda hizi zinafanya uchaguzi baada ya kukamilisha mchakato huo kuanzia ngazi ya chini hadi mkoa. Kanda za kaskazini na kati, zipo katika uchaguzi, lakini kwa ngazi ya chini ikiwemo matawi.

Uchaguzi huo utakwenda sambamba na kuwapata wenyeviti wa mabaraza ya Chadema katika ngazi ya mikoa yakiwamo ya Bazecha (Baraza la Wazee la Chadema) Bawacha (Baraza la Wanawake la Chadema) na Bavicha (Baraza la Vijana la Chadema).

Hadi sasa wagombea uenyekiti wa Kanda ya Magharibi waliochukua na kurejesha fomu ni  Martin Daniel, Gaston Garubindi (anatetea nafasi yake) mawakili Dickson Matata na Nsassa Mboje.

Kanda ya Victoria waliochukua na kurejesha fomu ni Ezekiah Wenje anayetetea nafasi hiyo, akichuana na John Pambalu ambaye ni mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha).

Katika Kanda ya Nyasa inayotajwa kuwa na ushindani mkali, waliochukua fomu ni pamoja na Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na Mchungaji Peter Msigwa anayetetea nafasi hiyo kwa awamu ya tatu.

Wengine ni Emmanuel Ntobi (mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Shinyanga) Lucas Ngoto, Butiko Mwija, James Mahangi na Gimbi Masaba waliochukua na kurejesha fomu kuwania uenyekiti wa kanda ya Serengeti.

Macho na masikio ya wanaChadema na Watanzania yatakuwa katika uchaguzi wa Nyasa wakitaka kujua nani ataibuka kidedea kati ya Sugu na Mchungaji Msigwa ambao walikuwa marafiki na waliingia wote bungeni mwaka 2010.

Mwananchi limewatafuta Sugu na Mchungaji Msigwa kujua mikakati ya yao kampeni endapo kamati kuu ikiwapitisha katika usaili na kusema wamejipanga vema katika kusaka ushindi.

“Usaili ukikalimilika na kupitishwa kituo kinachofauta ni kukutana na wajumbe ili kuwapelekea ilani yangu au vipaumbele, hata hivyo ninakwenda vizuri na timu yangu na nimeshikilia kura zangu.

“Lakini kura zaidi zinaendelea kumiminika kutoka upande wa pili… kadri wanavyozidi kuelewa nia yangu ya kuongoza Kanda ya Nyasa, kadri siku zinazovyozidi kwenda watu wanachambua pumba na mchele,”amesema Sugu.

Mchungaji Msigwa ambaye ni mbunge wa zamani wa Iringa Mjini amesema akipitishwa na kamati kuu atafanya kampeni za kistaharabu, kuheshimiana, za hoja shawishi na fikirishi.

“Nitasikiliza maelekezo na miongozo ya kufanya kampeni kisha nitafuata utaratibu huo, haya ndio malengo yangu makubwa,” amesema Mchungaji Msigwa.

Wapigakura takribani 120 wa kanda ya Nyasa ndio watakaoamua kati Sugu au Msigwa kuongoza kanda hiyo yenye mikoa ya Njombe, Iringa, Mbeya, Songwe na Rukwa.