Kamati ya Bunge yabaini sababu meli kuchelewa kushusha mafuta

Mbunge wa Sengerema (CCM), Hamis Tabasamu akichangia jambo walipotembelea miundombinu inayotumika kupakua mafuta Oil Jet iliyopo Kurasini, jijini  Dar es Salaam. Picha na Pamela Chilongola

Muktasari:

  • Serikali kupitia kwa Wakala wa Uagizaji wa Mafuta (PBPA) imeshauriwa kuboresho suala la uhifadhi wa mafuta pamoja na kusimamia mfumo wa SCADA uliobuniwa kwa lengo la kudhibiti changamoto ya upotevu wa mafuta yanayoingizwa nchini.

Dar es Salaam. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imebaini kuwa kutokuwepo kwa miundombinu ya kuhifadhia mafuta kumesababisha meli kukaa muda mrefu kusubiri kushusha nishati hiyo muhimu.

 Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk David Mathayo  amesema hayo leo Jumamosi, Februari 24, 2024 wakati wa ziara ya kutembelea miundombinu inayotumika kupakua na kuhifadhi mafuta katika Bandari ya Dar es salaam.

Amesema kutokuwepo kwa miundombinu hiyo  kunasababisha  gharama kubwa kwenda kwa mtumiaji wa mwisho.

Dk Mathayo amesema kamati imetoa ushauri kwa  kampuni ya kuhifadhia mafuta ya Tiper isafishe matanki yasiyotumika, ili wahifadhi  mafuta hayo na meli  hizo zishushe mafuta hayo haraka na kuondoka.

"Kampuni ya Tiper kwa sasa wanahifadhi mafuta kwa bei ambayo inasababisha kampuni ndogo kushindwa, kwa sababu tumesikia kuweka mafuta tani moja ni dola 700  za Marekani, hivyo kampuni hiyo iangalie uwezekano wa kupunguza gharama za uhifadhi," amesema Dk Mathayo.

Amesema pia kampuni ya Tiper iangalie uwezekano wa kupunguza gharama ya kuhifadhi mafuta kwenye matenki yake, jambo litakalosaidia kuwapunguza gharama wafanyabishara wadogo wanaotumia miundombinu ya kampuni hiyo kuhifadhi mafuta yao.

Kadhalika, Dk Mathayo amesema ikiwezekana eneo la nyumba za Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) likatumike katika kujenga matenki mengine, ili  kuongeza uwezo wa kuhifadhi mafuta na kuondokana na adha ya meli kusubiri muda mrefu.

Kuhusu mfumo wa kudhibiti upotevu wa mafuta (SCADA), ambao upo chini ya Wakala wa Uingizaji wa Mafuta (PBPA), Dk Marhayo ameshauri ufanyiwe maboresho ili malengo yaliyokusudiwa ikiwemo usalama wa mafuta rekodi zake zikae vizuri.

Kamati hiyo pia imeshauri flow meter zote zilizopo Bandari ya Dar es salaam ziwekewe uzio pamoja na kufunga kamera za kisasa (CCTV), kwa sababu zinasaidia kutazama usalama wa nchi kwenye masuala ya mafuta, ikiwemo udhibiti na ubora wa mafuta.

"Nchi inakuwa na akiba ya mafuta na fedha kutokana na uwekezaji uliowekwa, mafuta yanaingia bila wasiwasi lakini sisi kamati hatufurahishwi na usalama ulivyo kwa kuwa mtu yeyote anaweza kuingia, tunahitaji zijengewe uzio ziwe salama," amesema Dk Mathayo

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba amesema maelekezo yote yaliyotolewa na kamati hiyi ya Bunge yatafanyiwa kazi.