Kamati yakoshwa na miradi ya kimkakati

Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Maharage Chande akizungumzia mradi wa kituo cha upanuzi cha kuzalisha umeme kwa gesi asilia cha Kinyerezi (Kinyerezi I Extension) wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ilipokitembelea kituo hicho siku ya Jumamosi, 18 Machi 2023.

Muktasari:

  • Kamati ya kudumu ya bunge ya nishati  na madini yaipongeza serikali uwekezaji miradi ya  kimkakati

Dar es Salaam. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imesema  kukamilika kwa upanuzi wa kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia cha Kinyerezi 1, kutasaidia kuondoa changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo  na kuchochea uchumi wa nchi.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dunstan Kitandula baada ya kufanya ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa upanuzi wa kituo  hicho kilichopo mkoani Dar es Salaam kinachotegemewa kuzalisha jumla ya megawati 185.

 "Kama Kamati  tumeona mradi unaendelea vizuri na mitambo mitatu tayari imeanza kuzalisha megawati 135 bado mtambo mmoja ambao utekelezaji wake unaendelea vizuri"  amesema Kitandula.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato ameishukuru serikali kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa  miradi mbalimbali ya maendeleo.

 "Hizi ni jitihada zake  Rais na kwa ufadhili huu tuna uhakika utaongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika na wenye ubora na kuwezesha maendeleo mbalimbali kwenye viwanda vikubwa na vidogo na maendeleo ya kijamii" amesema Byabato.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco,Maharage Chande ameeleza kuwa mradi umepiga hatua kubwa tangu ulipoanza mwaka  2022 na mitambo mitatu kati ya minne ipo tayari na imeshaingiza umeme kwenye gridi ya Taifa.

"Ifikapo mwishoni mwa Aprili 2023 mtambo wa nne utakuwa tayari kuanza kuzalisha umeme. Hivyo natumia fursa hii kuwashukuru wateja kwa uvumilivu wakati huu mradi unaendelea kujengwa " alisisitiza  Chande.

Mjumbe wa kama hiyo Consatine Kanyasu ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa hatua zilizofikiwa kwenye mradi huo na kuomba kutia mkazo kwenye kuhakikisha  unakamilika kwa wakati.