Kambi ya Ruto inavyojipanga kukabidhiwa madaraka Ikulu

Muktasari:

Kambi ya Naibu Rais, William Ruto inahitaji uhakika wa mabadilishano ya madaraka baada ya kupata ushindi katika Uchaguzi Mkuu Kenya, unaotarajiwa kufanyika Agosti 9, mwaka huu.

Kambi ya Naibu Rais, William Ruto inahitaji uhakika wa mabadilishano ya madaraka baada ya kupata ushindi katika Uchaguzi Mkuu Kenya, unaotarajiwa kufanyika Agosti 9, mwaka huu.

Kenya Kwanza imeteua wajumbe wachache ambao wamepewa jukumu la kufuatilia mchakato mzima wa jinsi mabadilishano ya madaraka yatakavyokuwa pale Ruto atakapokuwa ametangazwa mshindi.

Habari ndani ya Kenya Kwanza zinasema kuwa kikosi hicho kinasubiri kwanza Ruto atangazwe rasmi kama mgombea urais, ndipo kitaanza vikao na maofisa wa ngazi za juu wa Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kuhusu mabadilishano hayo.

Moja ya mambo ambayo kikosi hicho cha kambi ya Ruto kitatakiwa kufanyia kazi ni uteuzi wa Katibu wa Baraza la Mawaziri. Kambi ya Ruto inahisi Kenyatta anachelewa kuteua kwa sababu kuna mchezo anajaribu kuucheza.

Katiba ya Kenya ya mwaka 2010, imempa Katibu wa Baraza la Mawaziri jukumu la kuwa Mwenyekiti wa kamati ya watu 22, watakaosimamia makabidhiano ya madaraka, kutoka rais anayemaliza muda wake hadi anayeingia madarakani.

Kikosi cha kambi ya Ruto kilichopewa jukumu hilo la kujadili na kuweka sawa suala la makabidhiano ya madaraka, kinatakiwa kuhakikisha muundo wa wajumbe 22 wa kamati ya makabidhiano ya Serikali, inaundwa kulingana na matakwa ya Katiba.

Muda ukiwa umebaki pungufu ya miezi minne kufikia tarehe ya Uchaguzi Mkuu Kenya 2022, Rais Uhuru Kenyatta anapaswa kutekeleza matakwa ya Katiba, ibara ya 154, kuteua mtu atakayekuwa Katibu wa Baraza la Mawaziri ili akathibitishwe na Bunge. Ni sharti la kikatiba kuwa mteule hatakuwa Katibu wa Baraza la Mawaziri mpaka athibitishwe na Bunge.

Timu ya Ruto inaamini kuwa jinsi Kenyatta anavyovuta muda, kunatoa dalili mbaya kwao kuwa anaweza kuwekwa mtu ambaye hatakidhi matakwa ya kikatiba kwa Bunge kumthibitisha, hivyo kumpa wakati mgumu kufanya naye kazi atakapokuwa ameshakula kiapo cha kuwa Rais wa Jamhuri ya Kenya.

Katibu wa Baraza la Mawaziri, mbali na kuongoza kamati maalumu ya makabidhiano ya Serikali, vilevile kwa nafasi yake ndiye mwenye mamlaka ya kupanga shughuli za Baraza, kutunza mambo yanayojadiliwa na kupitishwa na Baraza, vilevile kufikisha ujumbe kwenye mamlaka nyingine yale ambayo yanakuwa yameamuliwa na Baraza la Mawaziri.

Juni 6, mwaka huu, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), itatangaza majina ya walioteuliwa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi ujao.

Mpango wa kikosi kazi cha Ruto ni kuwa baada ya Juni 6, kitaanzisha vikao na mamlaka za Serikali kuhakikisha hakiharibiki kitu. Na kwa haraka zaidi Katibu wa Baraza la Mawaziri anateuliwa na jina lake kuthibitishwa na Bunge.

Mbunge wa Garissa Mjini, Aden Duale amesema kuchelewa kwa Kenyatta kumtaja mtu ambaye atashika nafasi hiyo kunahatarisha mazingira ya mabadilishano ya madaraka.

Duale alisema, hakuna mtu mwingine, isipokuwa yule aliyeteuliwa na Rais kikatiba na kuthibitishwa na Bunge, ndiye anaweza kuingia ofisini na kuendesha mchakato wa mabadilishano ya madaraka kutoka rais anayeondoka na anayeingia.

“Changamoto ni kuwa Bunge kwa sasa lipo kwenye mapumziko kwa muda. Vikao vitarejea Mei 9 na vitaendelea kwa wiki nne kabla ya kuahirishwa. Mpaka wakati huu hakuna jina ambalo limeshapelekwa bungeni ili lijadiliwe.

“Ukipiga hesabu zako vizuri utaona kuwa zimebaki wiki nne tu kwa Katibu wa Baraza la Mawaziri kuteuliwa. Kama hili halitafanyika, mchakato wa makabidhiano ya madaraka unaweza kuingiwa na hali ya hatari,” alisema Duale.

Maneno kama hayo ya Duale, aliyatoa pia Mwenyekiti wa chama cha United Democratic Alliance (UDA), Johnson Muthama.

“Rais hajali na hazingatii chochote kuhusu sheria za nchi. Anatakiwa kuheshimu Katiba ambayo aliapa kuilinda. Anabanwa na sheria kuteua Katibu wa Baraza la Mawaziri,” alisema Muthama.

Mbali na Katibu wa Baraza la Mawaziri, kuna timu ya watu 21 ambayo inatakiwa kufanya kazi pamoja kwa ajili ya kurahisisha mchakato wa makabidhiano ya madaraka. Wajumbe hao wengine ni pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Paul Kihara, Waziri wa Mambo ya Ndani, Fred Matiang’i, Mkuu wa Majeshi wa Kenya, Robert Kibochi, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa Kenya, Jenerali Philip Wachira Kameru na Msajili Mkuu wa Mahakama, Anne Amadi.

Wajumbe wengine wa timu hiyo ya makabidhiano ya madaraka ni makatibu nane wa Bunge, Mkuu wa Jeshi la Polisi Kenya, Katibu wa Bunge na watu watatu ambao watateuliwa na rais mteule.

Upande wa mgombea urais wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga, hajaonesha wasiwasi wowote kuhusu yeye kukabidhiwa madaraka endapo atashinda.

Utulivu wake unatajwa kujengwa na ukweli kuwa Raila anaungwa mkono na Kenyatta, hivyo hana shaka ya kukabidhiwa madaraka endapo atachaguliwa.

Agosti 27, 2012 aliyekuwa Rais wa Kenya, Mwai Kibaki alisaini sheria ya makabidhiano ya madaraka. Na mwaka 2013, kuelekea makabidhiano kutoka Kibaki kwenda Uhuru, kamati hiyo ilifanya kazi yake kikamilifu.

Hata hivyo, sehemu ya 5 ya sheria hiyo, ikisomeka hadi 6 na 7, inaeleza kuwa kuwepo wazi kwa nafasi ya mjumbe yeyote kwenye kamati hiyo ya makabidhiano, hakutaathiri uamuzi utakaofanywa na kamati.