Kampuni 30 zajitosa uendeshaji mabasi mwendokasi

Abiria wakigombania kupanda katika basi la mwendokasi. Picha na mtandao

Muktasari:

  • Mchakato wa kumsaka mtoa huduma ulianza mwaka 2018 na kuna kipindi Serikali ilitangaza kupatikana kwake, lakini hakuonekana akiendelea na biashara.

Dar es Salaam. Kampuni zaidi ya 30, zikiwemo mbili za Tanzania zimejitosa kuwania zabuni ya uendeshaji wa Mradi wa Usafiri wa Mwendo Haraka (Udart) katika Jiji la Dar es Salaam.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa kwa Udart na Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) kuhakikisha kampuni binafsi inapatikana kabla ya Oktoba mwaka huu.

Kauli hiyo ya Mchengerwa aliyoitoa Machi 20 mwaka huu jijini Dodoma, inatokana na changamoto zilizopo katika utoaji huduma za usafiri huo, hivyo kuwepo umuhimu kuishirikisha sekta binafsi kama ilivyokuwa imepangwa lakini utekelezaji ukasuasua.

Alisema iwapo mradi huo utaboreshwa vizuri asilimia 80 ya wakazi wa Dar es Salaam, jiji lenye watu zaidi ya milioni 5.3, watatumia usafiri wa mwendokasi.

Alionya endapo itashindikana, viongozi wa Udart na Dart waandike barua za kujiuzulu.

Jana, gazeti hili lilimtafuta Mtendaji Mkuu wa Dart, Dk Athuman Kihamia kujua kinachoendelea, naye akasema mchakato haujakamilika, ila muda ukifika watauhabarisha umma, lakini akadokeza kuwa uombaji wa zabuni umekwishaanza.

Alipoulizwa ni kampuni ngapi zimejitokeza, Dk Kihamia amesema: “Zaidi ya 30”, lakini hakuwa tayari kuzitaja majina.

Amesema kuna kampuni mbili za Dubai, nyingine za Asia, Uingereza na nyingine kutoka Afrika.

Hata hivyo, amesema: “Mpaka sasa hakuna kampuni iliyoshinda zabuni na Dart inaendelea na mchakato wa ununuzi.”

Kauli hiyo ya Dk Kihamia imekuja siku moja baada ya Kamishna wa Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), David Kafulila kunukuliwa na Azam TV akisema kampuni ya uendeshaji ya Dubai imekwishapatikana na kinachoendelea ni mazungumzo ya kimkataba baina yake na Dart.

Alipoulizwa ni wangapi wamejitokeza kuwekeza kwenye mfumo wa PPP, Kafulila amesema: “Kwa sasa tuko kwenye hatua ya majadiliano na mwekezaji kwa ajili ya kufunga mkataba na bila shaka pengine ndani ya mwezi ujao, mkataba kati ya mwekezaji na Serikali utakuwa umepatikana”.

Kafulila amesema utaratibu wa kumpata mwekezaji ulifanyika muda mrefu na sasa pande hizo mbili zinajadiliana kuhusu vigezo na masharti ya mkataba baina yao.

“Kinachosubiriwa sasa ni makubaliano ya vigezo na masharti ya mkataba kati ya pande hizo mbili, wakishakubaliana mwekezaji atatangazwa rasmi kama mwekezaji katika mradi huo,” amesema.

Kafulila amesema mwekezaji huyo ni mzoefu katika shughuli za usafirishaji, akiwa anafanya hivyo katika nchi mbalimbali, ikiwemo Dubai na “ndiye aliyeshinda na kufikia hatua hii ya majadiliano.”

Kafulila amesema katika mkataba huo, mwekezaji anatakiwa kuleta mabasi na atayaendesha kwa muda watakaokubaliana na baada ya hapo yatakuwa mali ya Serikali.


Ni jambo jema

Akizungumzia mchakato huo, mwanazuoni wa uchumi, Dk Donath Olomi amesema hatua ya Serikali kukaribisha sekta binafsi, ni jambo zuri.

‘’Tumejenga miundombinu kwa fedha nyingi halafu hatuitumii ile miundombinu kwa sababu hatujapata kampuni ya kuiendesha kiufanisi,” ameeleza.

Dk Olomi amesema ni jambo zuri kupata kampuni zishindanishwe na tuwe na mabasi mazuri ya mwendokasi.

“Serikali ibaki na kazi ya kusimamia sera, sheria na viwango. Serikali ina kazi nyingi za kufanya, huku iwaachie sekta binafsi,” amebainisha.

Hata hivyo, mchumi huyo ametahadharisha kuwa mchakato wa kupata kampuni, unapaswa kufanyika kwa makini na uwazi, kwani kutokufanya hivyo kunaweza kusababisha ikapatikana kampuni isiyokuwa na sifa.

“Mchakato unapaswa kufanyika kwa njia iliyo wazi ili kupata mwekezaji mwenye uwezo. Ukifanyika kwa figisufigisu tunaishia kupata mwekezaji ambaye hatatuletea matokeo,” amesema na kuongeza:

“Hakuna sababu ya msingi ya Serikali kuendesha mabasi na hatuhitaji kabisa ushahidi, kwa kuwa tumeona tayari. Na hii kitu si Tanzania tu, bali sehemu nyingi duniani shughuli kama hizi zinafanywa na sekta binafsi.

Hilo liliungwa mkono na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Raphael Maganga,  aliyesema uamuzi wa Serikali ni hatua kubwa kuona mradi kama huu wa BRT unahusisha sekta binafsi na hasa sekta binafsi ya Tanzania katika kuendesha mradi wa mabasi.”

“Lakini ili kuikuza sekta binafsi nchini, ni muhimu sana Serikali kuhakikisha kampuni za Watanzania wazawa zinaingia ubia na wawekezaji kutoka nje katika kuendesha mradi huu, kwani hii ndiyo njia mojawapo ya kuikuza sekta binafsi nchini,” ameongeza.


Udart bado yajipanga

Wakati uwekezaji huo ukitajwa kufikia hatua hiyo,  Mkurugenzi Mkuu wa Udart, Waziri Kindamba amesema anaendelea kupitia mafaili ya ofisi na historia yake, lakini maelekezo ya Waziri (Mchengerwa) wameyasikia na wanapaswa kuyafanyia kazi.

“Wiki hii nimalizane na wafanyakazi kuweka malengo ya taasisi, kisha wiki ijayo sasa nitaanza kukutana na wadau mbalimbali,” amesema.

Machi 9 mwaka huu, Kindamba aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Udart, akichukua nafasi ya Gilliard Ngewe ambaye ilielezwa atapangiwa kazi nyingine.

Mmoja wa wakazi wa Kimara, Dar es Salaam, Mariam Mussa akizungumzia mikakati ya Serikali kukaribisha uwekezaji binafsi, amesema ikiwa kinachofanyika kitafanikiwa, basi mradi huo utarejea kama ilivyokuwa ulipoanzishwa.

“Unajua unapokuwa unafanya biashara mwenyewe bila mshindani kuna kujisahau, si unaona kampuni za simu, ukizembea wanahamia mtandao mwingine, sasa ndio kama huu mradi, kukiwa na washindani kila mtu ataboresha huduma kuvutia wateja,” amesema Mariam.

“Serikali ihakikisha huu mchakato unafanyika haraka. Kwa sasa unaweza kukaa kituoni hata dakika 30 au saa moja hakuna mabasi, kwa hiyo hili ni jambo jema sana, kama Serikali itafanikiwa kumpata mshindani mwingine.”

Mchakato wa kumsaka mtoa huduma ulianza mwaka 2018 na kuna kipindi Serikali ilitangaza kupatikana kwake, lakini hakuonekana akiendelea na biashara.

 Baadaye mwaka 2019 Serikali ilitangaza kumsaka mtoa huduma mpya atakayekuwa na uwezo wa kununua mabasi 170, yaliyotarajiwa kutosheleza huduma kwa wakati huo, lakini naye hakuonekana barabarani.

Hata hivyo, mwaka 2022 Serikali ilitangaza kupatikana kwa mwekezaji mpya, ambaye ni kampuni ya Emirates National Group.

Kampuni hiyo kutoka Falme za Kiarabu ilitajwa ingenunua mabasi 750, yatakayosafirisha abiria kati ya 600,000 hadi 700,000 kwa siku. Hata hivyo, nayo iliyeyuka, hadi mchakato huu wa sasa.

 Katika kipindi hicho mradi wa mabasi yaendayo haraka, umekuwa ukilalamikiwa kwa huduma mbovu na zinazokwenda kinyume na matarajio ya wananchi.

 Miongoni mwa malalamiko ni mrundikano wa abiria vituoni, huku baadhi ya mabasi yakipita bila kuwabeba.

 Mzizi wa changamoto hiyo ulitajwa ni uchache wa mabasi, huku mengine zaidi ya nusu yakiwa mabovu.

 Wakati njia ya Kimara - Gerezani-Kivukoni - Morocco ikikabiliwa na uchache wa mabasi, ile ya Gerezani - Mbagala imekamilika, lakini haina mabasi ya kutoa huduma.

 Njia nyingine zinazoendelea kutengenezwa katika awamu ya tatu ni ya Gerezani - Gongolamboto – Magomeni - Chang’ombe.

 Pia, ujenzi wa barabara maalaum za zege zenye urefu wa kilomita 33.5, za Morocco – Kawe kilomita 7.8, upanuzi wa BRT1 (Kimara – Kibaha) kilomita 20.7 na upanuzi wa BRT 2 (Mbagala rangi tatu – Vikindu) kilomita 5.0 nazo ziko mbioni.