Kampuni nne kuwezesha wamiliki wa vyombo vya usafiri

Muktasari:

  • Kampuni nne zimengia makubaliano kutoa bima kwa waendesha vyombo vya moto kila wanapoweka mafuta.  

Dar es Salaam. Katika kufikia lengo la Serikali la kuwa na asilimia 50 ya Watanzania wawe na angalau aina moja ya bima ifikapo 2028, mpango mpya wa bima ya ajali na maisha unaohusisha waendeshaji wa vyombo vya moto umezinduliwa.

Mpango huo unaohusisha kampuni za Sanlam, Selcom, TanManagement utawanufaisha watumiaji wa vyombo vya moto wanaoweka mafuta kwenye vituo vya Puma nchi nzima na kulipia kwa njia ya mtandao.

Kupitia huduma hiyo kila atakayenunua mafuta ya kuanzia Sh10,000 na kulipia kidigitali  atapata bima ya ajali na maisha itakayodumu ndani ya siku saba

Mkurugenzi Mkuu wa Sanlam Tanzania Khamis Suleiman amesema mpango huo unalenga kutafsiri kwa vitendo maelekezo ya serikali ya kuifanya sekta ya bima kuchangia asilimia 5 kwenye pato la taifa.

Amesema fursa hiyo itawasaidia vijana wengi wakiwemo waendesha bodaboda, bajaji na daladala kuwa na uhakika wa maisha yao ikitokea wamepata ajali.

 “Ukiacha kuongeza idadi ya watumiaji wa bima mpango huu utasaidia kupunguza umaskini kwa kutoa fidia kwa walioathirika. Pia inasaidia kupunguza uwezekano wa kutembea na fedha, ukienda kituo cha mafuta unalipa kidigitali iwe ni kwa master card au QR Code,” amesema Suleiman.

Akizungumzia hilo Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Dominic Dhanah amesema kampuni yake itaendelea kushirikiana na wadau wengine wenye lengo la kuboresha huduma zitolewazo kwa wateja wake.

“Huduma hizi za bima kwa wateja wetu ni jitihada chanya. Hii inaakisi maudhui ya kampuni yetu ambayo ni kuchagiza maendeleo chanya kwenye jamii inayotuzunguka,” amesema Dhanah.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Selcom Tanzania Sameer Hirji amesema mchakato huo utatumia teknolojia ya kisasa ya malipo kuhakikisha lengo la kufikisha huduma ya bima kwa watu wengi.

Amesema, “Tukiwa waongoza njia katika mifumo ya malipo hapa nchini ni heshima kwetu kuendeleza juhudi hizi za kupunguza lengo la kidigitali sokoni.”