Kampuni za Kichina kutoa ajira 1,000 kwa vijana wa Tanzania
Katibu wa Chama cha Kampuni za Kichina Tanzania, Juma Sharobaro (kushoto) akizungumza pamoja na Zhao Yang (kulia), wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu maandalizi ya Maonesho ya Tano ya Ajira na Mabadilishano ya Vipaji kati ya Tanzania na China.
Muktasari:
- Maonesho ya Tano ya Ajira kati ya China na Tanzania yatakayofanyika UDSM Juni 16, 2026 yanatarajiwa kutoa zaidi ya nafasi 1,000 za ajira kupitia kampuni zaidi ya 100 za Kichina katika sekta mbalimbali kwa vijana wa Kitanzania.
Dar es Salaam. Zaidi ya nafasi 1,000 za ajira zinatarajiwa kutolewa kwa vijana wa Kitanzania wiki ijayo wakati kampuni zaidi ya 100 za Kichina zinazofanya kazi nchini zitakapokutana katika Maonesho ya Tano ya Ajira kati ya China na Tanzania, yakilenga kuwapa fursa wahitimu, wataalamu na wafanyakazi wenye ujuzi kuingia au kupiga hatua katika soko la ajira.
Maonesho hayo yatafanyika Juni 16, 2026 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na yanatarajiwa kuwa makubwa zaidi tangu kuanzishwa kwake, yakidhihirisha kuimarika kwa uhusiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na China pamoja na ongezeko la mahitaji ya wataalamu wa ndani wenye ujuzi.
Tukio hilo linaandaliwa kwa ushirikiano kati ya Chama cha Kampuni za Kichina Tanzania (China Enterprises Association in Tanzania), Ubalozi wa China nchini Tanzania na Taasisi ya Confucius ya UDSM.
Maonesho hayo yatawakutanisha waajiri kutoka sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi, uhandisi, madini, teknolojia, usafirishaji na vifaa, viwanda, nishati, mawasiliano ya simu, pamoja na sekta za habari na utamaduni.
Katibu wa Chama cha Kampuni za Kichina Tanzania, Juma Sharobaro, amesema maonesho hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kuwaunganisha waajiri na watafuta kazi huku yakichangia juhudi za kukuza ajira kwa vijana na maendeleo ya ujuzi.
“Maonesho ya mwaka huu yanatarajiwa kuwa makubwa zaidi tangu yalipoanzishwa, yakishirikisha kampuni zaidi ya 100 za Kichina zinazofanya kazi Tanzania na kutoa zaidi ya nafasi 1,000 za ajira kwa vijana wa Kitanzania,” alisema.
Kwa mujibu wake, nafasi zitakazotolewa zitahusisha taaluma za uhandisi wa ujenzi, umeme na mitambo, pamoja na maendeleo ya programu za kompyuta na teknolojia ya mitandao.
Pia, kampuni zitakuwa zinatafuta wataalamu wa sekta ya habari na ubunifu, wakiwemo wabunifu wa picha, wapiga picha, watengenezaji wa video na wataalamu wa mitandao ya kijamii.
Fursa nyingine zitapatikana katika maeneo ya utawala, rasilimali watu, fedha, manunuzi, usafirishaji wa mizigo, ukarimu, masoko na huduma kwa wateja, sambamba na nafasi za madereva, mafundi na wafanyakazi wengine wenye ujuzi.
“Kuanzia wanafunzi wa vyuo vikuu wanaokaribia kuhitimu hadi wataalamu wenye uzoefu na wafanyakazi wenye ujuzi, kila mmoja ataweza kupata fursa zinazolingana na sifa zake na matarajio yake ya kazi,” alisema.
Sharobaro amesema ushiriki katika maonesho hayo utakuwa bure kwa kampuni na watafuta kazi, huku gharama zote za maandalizi zikigharamiwa na Chama cha Kampuni za Kichina Tanzania.
Watafuta kazi watatakiwa kufika na nakala za wasifu wao (CV) na watapata nafasi ya kukutana ana kwa ana na waajiri, kujifunza kuhusu nafasi zilizopo na kuwasilisha maombi yao papo hapo.
Maonesho hayo yatafanyika kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 11:00 jioni katika viwanja vilivyopo mbele ya Maktaba Mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Alibainisha kuwa kampuni nyingi za Kichina zinazofanya kazi nchini zimewekeza kwa muda mrefu Tanzania, jambo lililochangia kuongezeka kwa ajira na kujenga utaalamu wa wazawa.
Kwa sasa chama hicho kina wanachama zaidi ya 70, wengi wao wakiwa wamekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza vipaji vya Watanzania kupitia ajira na mafunzo ya kazini.
Katika maonesho manne yaliyopita, zaidi ya watu 6,000 walishiriki kutafuta ajira, huku wengi wao wakifanikiwa kupata kazi na kujenga taaluma zao katika sekta za ujenzi, madini, usafirishaji wa mizigo, uzalishaji wa maudhui ya habari, ukarimu na usimamizi wa rasilimali watu.
Sharobaro alisema vijana wengi wa Kitanzania wamefanikiwa kupata ajira kupitia jukwaa hilo na baadaye kujenga taaluma zenye mafanikio.
Amesema baadhi yao walianza katika nafasi za ngazi za chini na sasa wamepanda hadi kushika nafasi muhimu katika taasisi wanazofanyia kazi.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Taasisi ya Confucius katika UDSM, Zhao Yang, amesema taasisi hiyo inajivunia kushiriki katika maandalizi ya tukio hilo ambalo ni daraja muhimu kati ya waajiri na watafuta kazi.
Amesema taasisi hiyo itaendelea kukuza ushirikiano katika elimu, utamaduni na lugha, huku ikiwasaidia wahitimu na wataalamu vijana kupata fursa za ajira zinazotolewa na kampuni za Kichina zinazofanya kazi nchini.