Kampuni za simu zaiangukia Serikali

Kampuni za simu zaiangukia Serikali

Muktasari:

  • Siku tano tangu Sheria ya Kodi ya Miamala ya Simu ianze kutumika, Chama cha watoa huduma za fedha kwa simu za mkononi (Tamnoa), kimesema biashara imeshuka kwa kiasi kikubwa na kuiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kusitisha makato mapya.

Dar es Salaam. Siku tano tangu Sheria ya Kodi ya Miamala ya Simu ianze kutumika, Chama cha watoa huduma za fedha kwa simu za mkononi (Tamnoa), kimesema biashara imeshuka kwa kiasi kikubwa na kuiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kusitisha makato mapya.

Mwenyekiti wa Tamnoa, Hisham Hendi alisema mamilioni ya wateja wameacha kutumia huduma zao hasa wale wa vijijini, kutokana na ongezeko la gharama jambo linalotishia biashara zao.

“Wateja wanalalamika sana hasa vijijini ingawa tunaendelea kutoa huduma bora kadri tuwezavyo tukitambua kwamba huduma za fedha kwa simu ya mkononi ni huduma muhimu kwa jamii. Tunaamini Serikali italiona hili na itachukua hatua stahiki kuokoa jahazi kwani kodi hii inaathiri biashara na kuwaumiza wananchi,” alisema Hendi kwenye taarifa ya pamoja iliyotolewa na Tamnoa.

Pamoja na kupoteza biashara, kampuni za mawasiliano zinazotoa huduma za fedha ambazo ni Vodacom (Mpesa), Tigo (Tigopesa), Airtel (Airtel Money), Halotel (Halopesa), Zantel (Eazypesa) na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL Pesa), zimesema kodi hiyo inawapunguzia ushindani sokoni pamoja na kupunguza ari ya kuwekeza zaidi.

Hata hivyo, wakati hali ikiwa hivyo kwa kampuni za simu, mambo ni tofauti kwa benki na taasisi za fedha nchini ambazo zimekuwa zikitoa matangazo yanayoonyesha kuwa zinatoa huduma nafuu zaidi ya miamala ya fedha kuliko washindani wao.

“Tunajiuliza lakini hatupati majibu kwa nini benki hazishiriki kukusanya mapato haya muhimu kwa Serikali kama ilivyo kwa kampuni za simu, ilhali wanatoa huduma kama zetu kama wanavyojieleza kwenye matangazo yao,” inasema taarifa ya Tamnoa.

Kuhusu usawa wa kodi, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPFS), Francis Nanai alisema mfumo mzuri wa kodi ni ule unaowahusisha watu wengi, huku kodi ikitozwa kwa viwango vidogo.

“Wazo la kuanzisha kodi ya miamala lilikuwa zuri ila viwango vinavyotozwa ndio sio rafiki. TPSF tunasikia malalamiko lakini tunaamini hakuna linaloshindikana. Serikali ikae na wadau kujadili upya viwango hivi na benki zisiachwe katika hili. Kutokana na teknolojia, simu nayo ni benki. Wapo watu wanakopa au kuweka akiba kwenye simu zao,” alisema Nanai.

Kwa kusikiliza maoni yanayotolewa na watoa huduma, wateja na mawakala wa huduma za fedha kwa simu za mkononi, mkurugenzi huyo alisema kuna haja ya kufanya utafiti kujua namna sahihi zaidi ya kutekeleza kodi hii.

Kukosekana kwa mazingira sawa ya ushindani, chama hicho kimesema ni suala linalowaumiza kichwa, ingawa wanaamini Serikali italiona hilo na kulifanyia kazi ili kuweka mazingira rafiki ya kuwekeza na kufanya biashara.

“Wanahisa na wawekezaji wetu wana wasiwasi na hali ya ushindani nchini. Wanafuatilia kwa ukaribu sana,” alisema Hendi kwenye taarifa hiyo ya watoa huduma.

Tofauti na sekta ya benki ambako benki kubwa nyingi ni za kizalendo, kampuni nyingi za mawasiliano ni za wawekezaji kutoka nje ambao wasiporidhika kuwekeza nchini, wanaweza kutafuta fursa mahali pengine.

Wawekezaji wakubwa wa Vodacom, kampuni inayoongoza kwa wateja na uwekezaji nchini ni Vodacom Group ya Afrika Kusini, wakati Tigo inayoimiliki pia Zantel, imepata mwekezaji mpya kutoka Madagascar, kampuni ya Axian Group baada ya Millicom International Cellular kutangaza kujiondoa Afrika.

Ingawa Serikali inazo hisa ndani ya Airtel ila mwanahisa mkubwa ni Airtel Group ya India huku Halotel ikimilikiwa kwa kiasi kikubwa na Serikali ya Vietnam.

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) ndiye mtoa huduma pekee anayemilikiwa na Serikali kwa asilimia 100, lakini anahudumia wateja wachache zaidi wa mawasiliano, intaneti hata huduma za fedha.

Upande wa pili, benki zenye mtandao mkubwa zaidi wa matawi na hata miundombinu ya kuwahudumia Watanzania wengi ni NMB na CRDB, huku kwa pamoja zikimiliki asilimia 40 ya thamani ya sekta hiyo. Benki hizi, kwa kiasi kikubwa zinamilikiwa na wazawa. Nchini kuna zaidi ya benki 60 zinazotoa huduma.

Kutishika kwa wawekezaji, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kuendeleza Huduma za Fedha Tanzania (FSDT), Sosthenes Kewe alisema linapaswa kutazamwa kwa umakini ili waendelee kuiona Tanzania ni sehemu salama kwao.

“Matangazo ya benki yanaonekana mitandaoni. Linapokuja suala la kodi, mlipaji anatakiwa kulipa kwa namna zote zinazowezekana na asiwepo wa kuachwa. Kama Serikali iliona kuna fursa kwenye miamala ya kielektroniki sijui kwa nini iliziacha benki. Kama kodi inatozwa kwenye miamala ya kidijitali hata akaunti ya benki ni dijitali pia,” alisema Kewe.


Imani kwa Serikali

Katika kutafuta nafuu, Hendi alisema kampuni za mawasiliano zinaendelea kuwasiliana na Serikali pamoja na Bunge kueleza hoja zao anazoamini zitafanyiwa kazi kwa mustakabali mwema wa Taifa.

Alisema wanachukua hatua hizo kwa kutambua kwamba hali inaweza kuwa mbaya zaidi huko mbele, kwani tayari siku nne za kuanza kwa makato hayo biashara haiendi vizuri.

“Mapato yameshuka kwa kiasi kikubwa kwa sababu wateja hawatumii huduma zetu kama ilivyokuwa mwanzo. Hali si nzuri,” alisema.

Kuhusu kodi ya muda wa maongezi inayotarajiwa kuanza siku chache zijazo, Hendi alisema wanazungumza na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kupata namna nzuri ya kutekeleza hilo bila kuathiri biashara iliyopo.

Akifafanua kwa nini benki hazishirikishwi kutoza kodi ya uzalendo kwenye miamala yao ya kidijitali, Mkuu wa kitengo cha mawasiliano serikalini katika Wizara ya Fedha na Mipango, Benny Mwaipaja alisema huu ni mwanzo huko mbele kutakuwa na fursa ya kutanua wigo.

“Watu wakielewa tunaweza kutanua maeneo ya kukusanyia kodi hii. Tumeanza tu kwenye miamala ya simu lakini huko mbele tunaweza kuangalia namna ya kutanua zaidi wigo na tukazihusisha benki za biashara,” alisema.


Tume ya Ushindani na Benki Kuu

Alipotafutwa ofisa mwandamizi wa habari na mawasiliano wa Tume ya Ushindani (FCC), Frank Mdimi alisema mkurugenzi mkuu wa tume hiyo anaweza kulizungumzia vizuri zaidi suala hilo.

“Ninachofahamu ni kwamba benki huwa zinatoa taarifa za gharama zao mara kwa mara ili wateja wao wazifahamu. Ukimpata mkurugenzi atakueleza vizuri zaidi. Unaweza kuwatafuta Benki Kuu pia wao ndio wasimamizi wa taasisi za fedha,” alishauri Mdimi.

Alipotafutwa mkurugenzi mkuu wa FCC, William Erio alisema tangu kuanza kuanza kutumika kwa sheria hiyo hajafuatilia taarifa hivyo hajui kinachoendelea.

“Sijafuatilia televisheni wala redio. Kuna mambo yamenibana na hapa nilipo najiandaa kwenda kijijini,” alisema Erio.

Hata Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga hakuwa na ufafanuzi wa kutosha kwenye jambo hilo akipendekeza atafutwe Waziri wa Fedha na Mipango.

“BoT ni regulator wa monetary sector (msimamizi wa sekta ya fedha). Masuala ya mapato ya Serikali hasa kodi ni ya wizara,” alisema Profesa Luoga.