Katibu mkuu akemea uzinzi mahala pa kazi

Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Said akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa Mtandao wa Mameneja Rasilimali watu katika Utumishi wa Umma Barani Afrika, Tawi la Tanzania (TPS-HRMnet) uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano (AICC). picha na Bertha Ismail.

Muktasari:

  • Amesema hali hiyo inasababisha kushuka kwa utendaji kazi, upendeleo, migogoro na vurugu na watumishi hushindwa kutekeleza majukumu yao kwa wananchi.

Arusha. Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Said ameonya mameneja rasilimali watu wa kada ya utumishi wa umma kujiepusha na vitendo vya ngono mahala pa kazi.

Amesema hali hiyo husababisha upendeleo, migogoro na vurugu na mwisho wa siku morali ya kazi kwa watumishi hushuka.

 Zena ameyasema hayo leo Jumanne Mei 7, 2024 wakati akizindua rasmi Mtandao wa Mameneja Rasilimali watu katika Utumishi wa Umma Barani Afrika, Tawi la Tanzania (TPS-HRMnet) uliofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano (AICC) ulioko jijini Arusha.

“Usizini ni moja ya amri kubwa sana kwa Mwenyezi Mungu na ukiivunja kwenye utumishi wa umma, ndiyo inaleta migogoro mahala pa kazi. Nasema hivi nikimaanisha mahusiano ya kingono yasiyofaa yanasababisha upendeleo, migogoro na kugombana, maana huyu anamgombania huyu sijui nani anamtaka huyu hadi wanapigana,  hii haipendezi yafaa mjiepushe nayo,” amesema.

Mbali na hilo, amewataka maofisa hao kujiepusha pia na wizi wa fedha za umma na matumizi mabaya ya madaraka.

Amesema wapo miongoni mwao huwanyanyasa  watumishi wenzao na kuwadharau lakini pia kuwanenea uongo kwa lengo la kuwakomoa.

“Nawaombeni sana msiwadharau wale mnaowaongoza kutokana na vyeo vyenu,  tendeni  haki na msikilize changamoto zao na kuzifanyia  kazi, tuache majungu na uzushi usiofaa kwa lengo la kuchafuana, bali kila  mmoja atimize wajibu wake kwa wakati tena kwa kuheshimiana,” amesema Zena.

Amewataka maofisa hao kwenda kusimamia vizuri sekta ya rasilimali watu na kutoa elimu kwa wananchi na watumishi walio chini yao kuhusu maswala ya utawala na usimamizi wa kada hiyo, ili kuepuka migongano isiyo na ulazima lakini kukuza matumizi ya Tehama nchini.

Naye Rais wa ‘TPS-HRMnet’, Xavier Daudi amesema lengo la mtandao huo ni kubadilishana uzoefu na kuhakikisha Bara la Afrika linakuwa na rasilimali watu wenye sifa ya kuweza kusaidia Serikali zao.

“Tunachokifanya sisi ni kuhamasishana hasa katika matumizi ya teknolojia, kama kuna nchi katika bara letu anajua chochote cha kiteknolojia ama jambo ambalo limejitokeza linaloweza kusaidia maofisa rasilimali watu kuweza kufanya kazi zao vizuri, basi tunatumia hiyo fursa,” amesema.

Mmoja wa washiriki wa mkutano huo, Gloria Mboya ambaye ni meneja rasilimali watu wa Mfuko wa Pensheni kwa watumishi wa Umma (PSSSF) amesema uadilifu na uaminifu ndio msingi katika utumishi wa umma.

Hivyo, amesema yote yaliyotolewa maelekezo katika kikao hicho wanaenda kuyatekeleza sambamba na kuhamasisha matumizi ya teknolojia katika utendaji kazi wao.