Kauli ya Lissu yazidisha fukuto Chadema

Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara) Tundu Lissu.

Muktasari:

  •  Chadema iko katika uchaguzi wa ndani wa chama hicho na makamu wake mwenyekiti-bara, Tundu Lissu ameibua tuhuma za fedha kumwagwa ili kukivuruga chama hicho.

Dar es Salaam. Katika hali inayoendelea kufukuta ndani ya Chadema, kufuatia kauli ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho (Bara), Tundu Lissu kwamba kuna fedha zimemwagwa katika uchaguzi wa ndani, kikao cha Kamati Kuu kinachosubiriwa ndio kinatajwa kutegua kitendawili.

Kikao hicho ambacho hata hivyo tarehe yake haijapangwa, kinatarajiwa kuwa cha moto, huku hoja ya fedha kumwagwa kwenye uchaguzi wa ndani pia ikitarajiwa kutawala.

Lissu alitoa kauli hiyo Mei 2, 2024 alipokuwa akihutubia katika mkutano wa hadhara mjini Iringa, akisema chama hicho hakitakuwa salama na fedha hizo, huku akiwaonya wanachama kujiepusha na rushwa ili kuchagia viongozi bora.

Tuhuma hizo za Lissu ambazo jana Ijumaa, Mei 3, 2024 Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Salum Hamduni alisema wanazifanyia kazi, zimeibua mjadala mkali kwa wanachama wa chama hicho.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Katika makundi yao songozi (WhatApp), kumekuwa na minyukano huku wengine wakitumia katiba ya chama hicho kuonesha Lissu ‘alivyoteleza’ kutoa tuhuma hizo hadharani, huku wengine wakimpongeza.

Wametaja sehemu ya kifungu katiba ya chama hicho kinachoelezea kuwa kiongozi asitoe tuhuma juu ya viongozi wenzake pasipo kupitia vikao halali na kuzingatia taratibu na ngazi zilizoelezwa kwenye kanuni za chama.

Msingi wa kauli ya Lissu ni kile kinachoendelea ndani ya chama hicho kuhusu uchaguzi wa ndani ngazi ya kanda nne kati ya kumi. Kanda zinazotarajia kufanya uchaguzi siku za usoni ni ya Nyasa, Victoria, Serengeti na Magharibi.

Kanda hizi zinaunda mikoa ya Mbeya, Njombe, Iringa, Mara, Kagera, Tabora, Geita, Kigoma, Songwe, Katavi, Shinyanga, Simiyu na Mwanza.

Leo, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alipoulizwa amesema suala hilo aulizwe Lissu mwenyewe na mengine atakuja kuyajibu baada ya vikao vya chama.

“Mmewahi kumuuliza Lissu kwanza kwamba kama hilo jambo limewasilishwa kwa Katibu Mkuu? Basi mtafute kwanza uzungumze naye.

“Kama unataka kuninukuu chochote ni kwamba, Katibu Mkuu nitazungumza baada ya vikao vya chama,” amesema Mnyika.

Amesema tarehe ya kikao cha kamati kuu bado haijapangwa. Hata hivyo, taarifa ambazo gazeti hili linazo, vikao hivyo vya kamati kuu vinatarajiwa kufanyia ndani ya wiki mbili kuanzia sasa.

Mbali na madai ya fedha kumwagwa katika chaguzi za ndani, Lissu alieleza kukerwa kwake na mabango yenye picha ya Rais Samia Suluhu Hassan na Mwenyekiti Freeman Mbowe na viongozi wa Baraza la Wanawake (Bawacha) na lingine likimwonyesha Lissu na Rais walipokutana nchini Ubeligiji.

Kutokana na hilo, amesema ataishawishi kamati kuu ya chama hicho kuyajadili mabango hayo na ikiwezekana kufungua kesi ya madai dhidi ya Rais Samia. Tangu juzi, Lissu hapatikani katika simu zake kufafanua kauli zake hizo.

Kauli ya Lissu

Akiichambua kauli ya Lissu kuhusu madai ya fedha za rushwa katika chaguzi za chama hicho, mchambuzi wa siasa, Bubelwa Kaiza amesema inaelekea kuwalenga baadhi ya viongozi wa juu ndani ya chama hicho kwamba wamenunuliwa kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

“Inaonyesha kuwa Lissu amekata rufaa kwa wananchi kwamba kuna viongozi wame compromise (wamerubuniwa) na upande wa CCM. Inawezekana alishasema kwenye vikao vya ndani.

“Alilenga kuleta mjadala ndani na nje ya chama ili kukipa nguvu chama kwa sababu walio wanachama na wasio wanachamwataendelea kukijadili chama,” amesema.

Amesema Lissu amekuwa na msimamo mkali usioyumba tangu awali na amekuwa akiuweka hadharani hasa anapoona mambo hayaendi sawa kwenye chama.

“Kwa mfano mwaka jana Chadema walipomkaribisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano wa (Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), ni ishara kwamba hicho chama kimeingiliwa.

“Utaona tangu mwanzo walipoanza mikutano ya hadhara, Mbowe alianza akiwa na ujumbe wa kupoza, lakini Lissu msimamo wake ni tofauti kabisa, hakubaliani kabisa na Rais Samia,” alisema.

Kwa upande wake Wakili Boniface Mwabukusi amesema anaiunga mkono kwani itasaidia kuondoa uovu ndani ya chama.

“Hivyo ndio inavyotakiwa, utafichaje ujinga? Ujinga unauweka hadharani ili kuusafisha. Ukijadili ujinga unamea na kuota cancer (saratani). Tunataka Taifa la namna hiyo ambacho kinaweza kujisafisha ndani na kukosoa vyama vingine nje,m kwa hiyo Lissu yuko sahihi,” alisema. 

Uchaguzi Kanda ya Nyasa

Tangu uchaguzi wa ndani wa Chadema ulipoanza, Kanda ya Nyasa imeonekana kuwa na ushindani mkali kati ya mbunge wa zamani wa Iringa Mjini, Peter Msigwa na Mbunge wa zamani wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina la Sugu.

Wawili hao wamekoleza joto la uchaguzi kwa wafuasi wao kuandamana na kwenda kuwachukulia fomu za ugombea uenyekiti wa kanda hiyo.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema aliyeomba ahifadhiwe jina lake, alisema uchaguzi wa Kanda ya Nyasa haujawahi kuwa mwepesi akitolea mfano mwaka 2017, mwaka 2019 na huu wa sasa.

Amesema mwaka 2017 alikuwa Mchungaji Msigwa na Patrick Ole Sosopi ambaye wakati huo alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha).

“Sosopi alikuwa na nguvu na alikuwa na uwezekano wa kumwangusha Msigwa, sijui nini kilitokea kipindi hiko Sosopi akakatwa, akwa mgombea mmoja (Msigwa), kura zilivyopigwa za ndio zilikuwa 56 na 48 za hapana,” amesema.

Mjumbe huo amesema mwaka 2019 ulipowadia akawa Mchungaji Msigwa na Wakili Boniface Mwambukusi: “Licha ya Msigwa kushika vizuri lakini kuna kitu bila shaka hakikwenda vizuri na Mwambukusi akaondoka ndani ya chama.”

“Sasa mwaka huu ni Msigwa na Sugu. Wote wana nguvu na ushawishi, nani anakatwa kama 2017 simwoni, wote wanakwenda na mvutano mnaouona ni matokeo ya kukua kwa chama.

“Wapo wanaosema Sugu anaungwa mkono na (Freeman) Mbowe na wengine wanasema Msigwa anaungwa mkono na Tundu (Lissu). Ni mvutano kwelikweli na mwisho chama kitavuka salama tu,” amesema.

“Kinachotokea Nyasa ni kuonesha chama kina nguvu sana ukanda huo ukilinganisha na maeneo mengine. Rejea hata kauli za mwenyekiti (Mbowe) aliwahi kuipongeza Nyansa. Kwa hiyo kila mmoja anatamani kuiongoza,” amesema.

Alipoulizwa jana kuhusu mvutano wake katika uchaguzi huo, Wakili Mwabukusi ambaye sasa ni mwanachama wa NCCR Mageuzi, alisema aliondoka Chadema baada ya kuona baadhi ya viongozi wa juu (hakuwataja), walikuwa hawamtaki.

“Ilionekana ama sihitajiki na viongozi wa juu, wengi wakinihisi mimi na tuhuma mbalimbali, si unajua mambo ya siasa?

“Kulikuwa na madai ya viongozi wa juu kwamba labda kuwepo kwangu mimi chama hakitakuwa salama zaidi,” amesema.