Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kauli ya Mwandosya yaibua mjadala

Muktasari:

  • Hayo yamesemwa siku nne tangu Rais John Magufuli alipozungumzia sakata la makontena hayo yenye samani mbalimbali yaliyokwama bandarini yakidaiwa kodi ya Sh1.2 bilioni.

Dar es Salaam. Wanasiasa, wanasheria pamoja na wanaharakati wamemkalia ‘kooni’ Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakitaka awajibike kwa madai ya kupoteza uadilifu kusimamia shughuli za maendeleo kutokana na sakata lake la kutaka kusamehewa kodi ya makontena 20 yaliyopo bandarini Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa siku nne tangu Rais John Magufuli alipozungumzia sakata la makontena hayo yenye samani mbalimbali yaliyokwama bandarini yakidaiwa kodi ya Sh1.2 bilioni.

Kabla ya Rais Magufuli kulizungumzia, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango aliingia katika malumbano na Makonda baada ya mkuu huyo wa mkoa kusema yeyote atakayejitokeza kununua makontena hayo atalaaniwa yeye na uzao wake kauli ambayo ilijibiwa na Dk Mpango kwamba yatauzwa na hakuna laana itakayompata mtu.

Agosti 30, Rais Magufuli akizungumza na madiwani, viongozi na watumishi wa Halmshauri ya Wilaya ya Chato alisema sheria za nchi zinasema wazi ni mtu mmoja tu katika nchi mwenye dhamana ya kupokea misaada kwa niaba ya wananchi.

“Sasa ukichukua makontena kule, umezungumza na watu wengine labda na wafanyabiashara, unasema ni makontena yako, halafu ukasema tena labda ni ya walimu, wala hata shule hazitajwi, maana yake nini?

“Maana yake si unataka utumie walimu, ulete haya makontena, utapeleka shule mbili au tatu, ndizo zitapewa mengine unakwenda kuyauza unapeleka kwenye ‘shoping mall’ (maduka makubwa). Lakini walimu walikuambia wanahitaji makochi, sofa,” alisema.

Juzi, mwanasiasa mkongwe nchini, Profesa Mark Mwandosya bila kumtaja jina Makonda, aliandika ujumbe katika mtandao wake wa kijamii wa Twitter ambao ulisambaa mitandaoni ukisomeka, “Nilipofundishwa misingi ya utawala, mkuu wa nchi akikukosoa mtumishi hadharani, unapeleka barua ya kujiuzulu ili kulinda heshima yake na kwa kufanya hivyo unajijengea heshima mbele ya umma. Nikiri kwamba huenda misingi hiyo imepitwa na wakati.”

Alipopigiwa simu jana ili kutoa ufafanuzi kuhusiana na ujumbe huo, Profesa Mwandosya alisema “Mimi sijamlenga mtu yeyote, nimetoa mawazo yangu kama mzee wa nchi hii.”

Akichangia ujumbe huo mtandaoni, mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Privatus Karugendo aliandika, “Prof, hii misingi haijapitwa na wakati, ila wazee tumeshindwa kujenga utamaduni wa kuwajibika. Hawa vijana wadogo watajifunza wapi? Hatuna utamaduni wa kujiuzulu. Si kujenga heshima tu, bali pia ni kumsaidia Rais, kufanya maamuzi magumu na wepesi wa kuliongoza Taifa.”

Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania, Abdul Nondo aliandika kwenye mtandao akimjibu Profesa Mwandosya, “Kiongozi wa umma anaweza ishi hajui hata anaongozwa na kanuni zipi za uongozi wa umma au sheria zipi! Yeye anafanya kazi anavyojisikia tuu!! Ilimradi aambiwe ni mbunifu au anayethubutu basi wala hajali kuhusu maadili ya uongozi sio kipaumbele sasa hivi mzee wetu.”

Wakati baadhi wakitumia mitandao ya kijamii kufikisha ujumbe wao, mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kupitia barua yake ya wazi kwa Rais Magufuli alielezea sakata hilo na kuzusha hoja kadhaa.

Lissu ambaye yupo Ubelgiji kwa matibabu alitaka mjadala wa makontena hayo usiishie tu kumtaka kiongozi huyo kuambiwa akalipe kodi, bali uende mbali zaidi kwa kuangalia uwezekano wa kuwapo makosa mengine ya kijinai.

Mwenyekiti wa chama cha CCK, Renatus Muabhi akizungumza na Mwananchi jana alisema ingawa viongozi wa Afrika wamekuwa na tabia ya kugomea kuwajibika wakati wanapokumbwa au kutumbukia katika kashfa, kwa hili linalomhusu Makonda anapaswa kutafakari mara mbili kauli ya Rais.

“Kwa kuangalia kauli ya Rais, Makonda angefanya jambo... nadhani alipaswa kujitathmini na kisha aone hatua za kuchukua,” alisema.

Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu) alisema sakata hilo ni kubwa na tena linamhusu mtu aliyeteuliwa kuongoza mkoa mkubwa hivyo haliwezi likaachwa limalizike kimyakimya bila mhusika wake kuchukuliwa hatua za kisheria.

Mwenyekiti wa Chama cha Umma (Chaumma), Hashimu Rungwe alisema, “Rais kishasema alipe kodi, akalipe kodi. Yeye ni kiongozi wa umma na ili basi arejeshe heshima na sifa yake aende akalipe kodi lakini pia Rais ataangalia mwenyewe hatua za kuchukua sisi hatuwezi kumwamulia kitu cha kufanya angalau sasa anajua kwamba kupitia kashfa hii kiongozi aliyenaye ni mtu wa namna gani.”