Kauli za maaskofu ibada ya Ijumaa Kuu
Muktasari:
Jamii imeaswa kudumisha upendo, kujali wengine
Dodoma/Mikoani. Katika kuadhimisha ibada ya Ijumaa Kuu, maaskofu wamekemea tabia za watu wanaojiua, kwenda kwa waganga wa kienyeji na wanaojinufaisha kupitia shida za wengine.
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dodoma, Beatus Kinyaiya amewataka watu wanaofikia hatua ya kutaka kujiua wanapopata shida kuacha kufanya hivyo, badala yake wamkimbilie Yesu wa Msalabani.
Ametoa kauli hiyo kukiwa na matukio ya watu, wakiwamo watoto wadogo kujiua. Takwimu za Jeshi la Polisi zinaonyesha watu 666 walijiua katika kipindi cha kati ya mwaka 2016 hadi 2019.
Askofu Kinyaia amesema hayo leo Machi 29, 2024 wakati wa ibada ya Ijumaa Kuu kitaifa iliyofanyika katika Parokia ya Paulo wa Msalaba, jijini Dodoma.
Amesema mwanadamu anapopitia mateso na shida wakati mwingine Mungu huruhusu kitu kizuri kitokane na matatizo hayo.
Ametoa ushuhuda wa mwanamke aliyeenda kwake kumweleza matatizo ya mume wake kuwa hampendi akawa anamwombea anaondoka.
Askofu Kinyaiaya amesema kwa miezi mitatu hakumuona tena mwanamke huyo, lakini wa nne alifika ofisini kwake na kupiga magoti jambo lililomfanya kumuuliza imekuaje siku hiyo amekuja na staili hiyo.
Amesema mwanamke huyo alimjibu amefika kumuomba msamaha Mungu kwa sababu alikuwa anadhani mume wake hampeni lakini kumbe anampenda.
Alimweleza alifahamu hayo baada ya kulazwa hospitali ambako mume wake alimhudumia kwa kumlisha chakula na kumfulia nguo zake.
Askofu Kinyaia amesema Mungu anaweza kugeuza ugonjwa, akaleta kitu chema ambacho mwanamke huyo hakujua.
Amesema mwanadamu anaweza kupita katika shida wakati wowote, lakini kinachotakiwa ni kumkimbilia Mungu.
“Usikate tamaa na wale wanaopata shida wanafikiria kujiua tafadhali sana acha kabisa, badala yake mkimbilie Yesu wa msalabani anajua mateso ni nini na atakusaidia, wala usikimbie familia na kutoroka. Usitoroke baki na mke wako, sali kwa Yesu anayebeba msalaba atawapeni majibu kwa mnayoyapitia,” amesema.
Ametoa ushuhuda wa muumini aliyekuwa akiumwa saratani aliyeenda kwake akimtaka amuombee maana madaktari walimweleza ana miezi sita ya kuishi.
“Nilimjibu basi nitakuombea. Mwenyezi Mungu ndiye daktari lakini aliyeniambia baada ya miezi sita nitakufa bado yupo hai mpaka leo, Hayo ndio maajabu ya Mungu ukimwamini,” amesema.
Askofu Msimbe
Askofu wa Kanisa katoliki Jimbo la Morogoro, Lazarius Msimbe amewaasa waamini kumtumainia Mungu katika mahitaji yao, waache kwenda kwa waganga kwani wakifanya hivyo watakufa.
Akiongoza ibada katika Kanisa la Mtakatifu Patrick jimboni humo, Askofu Msimbe amesema Ijumaa Kuu iwe kumbukumbu nzuri kwa waamini wote na wahakikishe wanamrejea Mungu.
"Nawaomba waamini wote waache dhambi, wamgeukie Mungu. Waamini wameacha kumuamini Mungu na kumgeukia shetani kwa kwenda kwa waganga ili wasaidiwe kutatuliwa matatizo yao jambo ambalo halina msaada hata kidogo," amesema.
Askofu Msimbe amesema dunia imejaa magonjwa mengi, watu hawaamini kwamba wakienda hospitali wanaweza kupona, badala yake wanaenda kwa waganga wa kienyeji ili wawaponye.
“Siku zote mganga hana dira na afya yako, badala yake yeye jicho lake ni kwenye fedha, na akishapata fedha yako yeye amemaliza,” amesema.
“Kama mkipata magonjwa nendeni hospitali mkatibiwe, msipopona tafuteni watumishi wa Mungu kweli-kweli ili mkaombewe, maana kufanya hivyo ni kujiweka karibu na Mungu na Pasaka hii ikawe na upatanishi kwenye mioni yenu mkakatae waganga," amesema.
Amesema siku hizi baadhi ya watu wamechukulia magonjwa ya watu kama biashara, kwa kutokuwa waelewa wanadhani wakitumia njia hizo za kwenda kwa waganga watapona.
Mbali ya hilo, amesema roho ya msamaha miongoni mwa waamini imetoweka, hivyo Pasaka ikalete upatanisho na misamaha katika maeneo yote.
"Ndugu zangu Pasaka hii ikawe yenye kuleta upatanisho kwa wote, tumeshuhudia viongozi wa dini hawasemezani, viongozi wa Serikali hawasemezani, viongozi wa jumuiya hawasemezani, wale wa kisiasa nao hawaongei. Ukiangalia chuki zimewatawala hawana kabisa mpango wa kusameheana, watumie Pasaka hii kuwasaheme wenzao, ikalete upatanisho miongoni mwao," amesema.
Askofu Sangu
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga, Liberatus Sangu, amewataka watu wenye tabia ya kujinufaisha kupitia shida za wengine kwa kujipatia mali na heshima kuacha vitendo hivyo, badala yake wawe mstari wa mbele kuwasaidia wenye uhitaji.
Akizungumza wakati wa ibada ya Ijumaa Kuu katika Kanisa Katoliki la Mama Mwenye Huruma, Parokia ya Ngokolo, Askofu Sangu amesema yanapotokea matatizo kwenye familia ikiwemo misiba baadhi ya watu wamekuwa wakitumia fursa hiyo kujinufaisha kwa kuchukua mali na kuacha watoto wakihangaika.
Amesema kupitia mateso ya Yesu Kristo msalabani inawapasa watu kubadilika na kuwa watetezi wa wajane, yatima na walio katika shida mbalimbali na si kuwakandamiza.
"Wakati wa msiba watu wanajinufaisha kupitia mirathi ya marehemu watoto wanabaki wanahangaika. Tuwe watetezi wao yatima, wajane na wengine wenye shida mbalimbali, tusiwakandamize," amesema.
Amesema mara nyingi kina mama ndiyo wamekuwa mstari wa mbele kuomba msamaha katika familia lakini kina baba wengi hawaombi, akisisitiza msamaha unasaidia kulinda ndoa zidumu.
Neema Chala, mkazi wa Mtaa wa Ngokolo, ambaye ni muumini wa kanisa hilo amesema mafundisho hayo wakiyazingatia yatawawezesha kuwa katika msingi mzuri, ikiwamo kuwasaidia watu wenye uhitaji na kulinda ndoa zao.