Kawaida: Kidato cha nne kisiwe kigezo cha fursa BBT
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Mohammed Kawaida (kulia) leo Jumatatu Aprili 17, 2023 akipokea taarifa kuhusu kituo cha mafunzo Bihawana cha mradi wa BBT kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli (kushoto).
Muktasari:
- Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Mohammed Kawaida ameshauri kidato cha nne kisiwe kigezo cha kijana kupata nafasi katika mradi wa Jenga kesho iliyobora (BBT).
Dodoma. Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Mohammed Kawaida ameshauri utashi ndiyo utumike kama kigezo kwa kijana kupata nafasi katika mradi wa Jenga kesho iliyo Bora (BBT), badala ya kiwango cha elimu.
Kauli hiyo inatokana na kile alichokieleza kuwa vijana wengi wanajua kuwa ili uingie kwenye mradi huo ni lazima uwe na elimu ya kidato cha nne.
Kawaida ametoa kauli hiyo jijini Dodoma leo, Jumatatu Aprili 17, 2023 alipotembelea mradi wa BBT Kituo cha Bihawana ikiwa ni ziara yake ya kikazi ya kutembelea miradi hiyo katika mikoa tisa (Dodoma, Mbeya, Morogoro, Kilimanjaro, Arusha na Mtwara).
"Ukweli ukienda shambani utakuta wanaolima ni wale wenzangu na mimi wa darasa la saba, kidato cha pili na wengine, tukitangaza wanaohitajika ni kidato cha nne tutawanyima fursa hawa wengine.
"Jeshini wanataka kidato cha nne, kila eneo kidato cha nne hili kundi lingine tunalipeleka wapi," amesema Mwenyekiti huyo. Hata hivyo, amesema mradi huo ni fursa muhimu kwa vijana huku akiwataka kuitumia vema.
Akizungumza kuhusu kigezo cha kidato cha nne, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli amesema makundi yote ya vijana yana nafasi ya kuomba fursa hiyo.
"Tumezingatia na tutazingatia makundi yote ya vijana kupata nafasi katika mradi huu kwa hiyo kila kijana anayo fursa," amesema.
Makamu wa Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Kituo hicho cha mafunzo, Asia Msuya amesema kinachofanyika katika mafunzo hayo ni kinyume na inavyoaminiwa na baadhi.
Ameeleza wapo wanaoamini kuwa mradi huo unafanyika kisiasa, lakini uhalisia ni kinyume chake, kwani wanajifunza kwa kina kuhusu kilimo.
"Mimi nimehitimu shahada ya sheria, nilikuwa najitolea kwenye ofisi mbalimbali za wanasheria baada ya kuiona fursa hii ikabidi niombe na najifunza kwa miezi minne kisha nitakwenda kupewa shamba," amesema.
Mradi wa BBT una lengo la kuongeza ajira katika sekta ya kilimo kwa vijana ambapo mpaka sasa ripoti ya ‘Tanzania in figures 2021’ iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonyesha idadi ya ajira inaongezeka kidogo huku idadi ya watu na wahitimu ikiongezeka kwa kiasi kikubwa.
“Idadi ya wenye ajira nchini mwaka 2019 ilikuwa milioni 22.4 kabla ya kuongezeka mwaka 2020 hadi kufika ajira milioni 23 kabla ya kuongezeka kidogo hadi milioni 23.5 mwaka 2021,”ilisema ripoti hiyo.
Mwaka 2017 kiwango cha wasio na ajira kilikuwa asilimia 9.9, mwaka 2018 kilikuwa asilimia 9.7, mwaka 2019 ilikuwa asilimia 9.6 huku mwaka 2020 kikifika asilimia 9.5 kabla ya kufika asilimia tisa mwaka 2021.