Kaya zaidi ya 70 zaathirika mafuriko Musoma
Baadhi ya nyumba katika ktaa wa Welfare Manispaa ya Musoma zikiwa zimezingirwa na maji kufuatia mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia leo Desemba 31,2023. Picha na Beldina Nyakeke
Muktasari:
- Wananchi waomba Serikali iwasaidie na mitaro iliyozibwa izibuliwe ili maji yaelekee ziwani.
Musoma. Baadhi ya wakazi wa Kata ya Kitaji Manispaa ya Musoma mkoani Mara wameiomba Serikali iwasaidie baada ya makazi yao kuzingirwa na maji yaliyotokana na mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia leo, Desemba 31, 2023.
Wakizungumza na Mwananchi Digital, wakazi hao wamesema chanzo cha maji kuzingira katika makazi yao ni kutokana na kuziba kwa mitaro mikubwa iliyopo katika mitaa ya Mukendo na Walfare hivyo maji kushindwa kwenda ziwani kama inavyotakiwa.
"Hadi mchana huu hatujaweza hata kuwasha majiko ili tuwapikie watoto kwasababu maji yapo kila sehemu tunaiomba Serikali itusaidie kwasababu hali ikiendela hivi watoto watakufa na njaa," amesema Neva Muhina
"Kama unavyoona maji yameingia hadi ndani kila kitu kimeloana lakini hadi sasa ni kimya tu hatujui leo tutalala wapi na nini mustakabali wetu," amesema Mahamud Shakur, mkazi wa Musoma.
Akieleza namna hali ilivyotokea, Muganyizi John amesema mvua zilianza kunyesha usiku na maji kuanza kuzingira nyumba kabla ya kuingia ndani na kuharibu samani na mali nyingine zilizokuwemo ndani.
Mwenyekiti wa mtaa wa Welfare, Lucas Kuhenga amesema asilimia 75 ya nyumba katika mtaa wake zimezingirwa na maji huku akiitaka Serikali kuwanusuru wakazi hao.
"Hili tatizo sio kwamba ni jipya, mara nyingi nyakati za mvua kunatokea mafuriko na watu wa manispaa wamekuwa wakifanya tu ukaguzi bila kuleta suluhisho,"amesema
Diwani wa Kitaji, Gordon Marcus amesema nyumba zaidi ya 72 zimezingirwa na maji na kwamba hadi sasa bado hazijapata msaada wowote.
"Nimewaslliliana na uongozi wa Manispaa na watu wa idara ya afya tayari wamefika ila kuhusu mustakabali wa watu hawa hadi sasa bado ni kimya hivyo hatujui usiku wa leo watalala wapi,"amesema Marcus
Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk Halfan Haule hakupatikana kuzungumzia suala hilo baada ya simu yake kuita bila kupokelewa huku Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma, Bosco Ndunguru alipotafutwa amesema yupo nje ya Musoma.