Kazi mradi bwawa la Nyerere yafikia asilimia 67

Waziri wa Nishati January Makamba akiwafafanulia jambo wajumbe wa Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) pamoja na wanahabari waliotembelea Bwawa la Julius Nyerere jana. Picha na Mpigalicha Wetu

Muktasari:

Waziri wa Nishati, January Makamba amesema ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere (JNHPP) umekamilika kwa asilimia 67.18.

Rufiji. Waziri wa Nishati, January Makamba amesema ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere (JNHPP) umekamilika kwa asilimia 67.18.

Waziri alisema hayo alipowaongoza wajumbe wa Bodi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), menejimenti, wahariri na waandishi wa habari kutembelea mradi huo uliopo Rufiji mkoani Pwani.

Makamba alisema kazi za ujenzi zinafanyika usiku na mchana kuhakikisha unakamilika kwa wakati baada ya Serikali kuibadilisha bodi ya wakurugenzi wa Tanesco.

“Huu ni ushindi na wenye faraja kwa kufikia hatua hii kubwa. Unajua hizi kazi si kupiga siasa tu, kazi kubwa imefanyika ndani ya mwaka mmoja, si kila kitu ni cha kusema ila matunda ya ukimya na kupiga kazi ndio haya,” alisema.

Moja ya jukumu kubwa alilokuwa akiliona mbele yake baada ya kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Septemba 11 mwaka jana, alisema ni kuhakikisha mradi huo unakwenda kwa kasi kwa kuhakikisha usimamizi unaimarishwa na fedha zinapatikana kwa wakati.

Akijibu lini wataanza kujaza maji kwenye bwawa hilo, mhandisi mkazi wa mradi huo, Lutengano Mwandambo alisema “kujaa kwa bwawa kunategemea mvua lakini misimu miwili inatosha au mmoja ukiwa na mvua nyingi.”

Alipoulizwa kuhusu kukamilika kwa mradi huo, alisema wanatarajia Aprili 2024 uwe umekamilika kwa thamani ya Sh.6.65 trilioni.

Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Maharage Chande alisema, mradi huo ni mkubwa na wenye kiu ya Watanzania kuona unaanza uzalishaji.

Alisema anapoona watu wanahoji maendeleo yake hapati hofu kwa sababu ni haki yao na kikubwa wanausimamia kuhakikisha unakamilika na kuanza kuzalisha umeme.


Panga, pangua Tanesco

Akitoa maelezo ya ziara hiyo, Waziri Makamaba alidokeza sababu iliyosababisha mabadiliko ya uongozi ndani ya Tanesco kuwa nimradi huu.

“Tangu bodi na menejimenti hii imeingia, tumeridhishwa sana na usimamizi wa mradi huu,” alisema Waziri Makamba.

Alisema usimamizi huo aliouita wa kisayansi kwa maana ya ratiba, fedha za watu, umerejea kwenye kasi na utakapokamilika utakuwa katika ubora na uwezo.

Mabadiliko hayo makubwa ndani ya Tanesco yalifanyika Septemba 25 mwaka jana kwa Rais Samia Suluhu Hassa kumteua Maharage Chande kuwa mkurugenzi mkuu akichukua nafasi ya Dk Tito Mwinuka na Omari Issa kuwa mwenyekiti wa bodi ya Tanesco.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu ilisema mabadiliko mengine ni ya aliyekuwa mkurugenzi mkuu Shirika la Kusafisha Mafuta (Tipper), Michael Minja ambaye aliteuliwa kuwa kamishna wa petroli na gesi, Wizara ya Nishati.

Pia, alimteua Felschemi Mramba kuwa kamishna wa umeme na nishati jadidifu. Kabla ya uteuzi huo Mramba alikuwa mshauri mkuu wa kiufundi Chuo cha Ufundi cha Tanesco. Hata hivyo, kwa sasa Mramba ani katibu mkuu wa Wizara ya Nishati.

Mabadiliko mengine yalimhusu Hassan Seif Said kuwa mkurugenzi mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) akitoka kuwa meneja wa kanda mwandamizi wa Kanda ya Mashariki Tanesco ambaye alichukua nafasi ya Amos Maganga.

Wakati huohuo, taarifa hiyo ilisema Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Hussein Kattanga aliwahamisha watumishi waandamizi watano kutoka Tanesco kwenda Ofisi ya Rais, Menejmenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambako watapangiwa kazi nyingine.