KCBL yazindua huduma za kidigitali

Muktasari:

  • Benki ya Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro (KCBL), imezindua huduma za kidigitali katika benki hiyo lengo likiwa ni kuwezesha upatikanaji wa huduma popote nchini.


Moshi. Benki ya Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro (KCBL), imezindua huduma za kidigitali katika benki hiyo lengo likiwa ni kuwezesha upatikanaji wa huduma popote nchini.

Akizungumza leo Jumatano Novemba 10, 2021 wakati wa uzinduzi huo Meneja Mkuu wa KCBL,  Godfrey Ng'urah amesema teknolojia na mfumo wa kutoa huduma mbadala kwa kutumia mawakala, Visa kadi na ATM ni muhimu  kwa wateja kulingana na hali ya dunia ilivyo kwa sasa.

Amesema kadi ya Visa ya KCBL, iliyozinduliwa itawawezesha wateja wa benki hiyo kufanya miamala ya kutoa na kuweka fedha kupitia mawakala wa benki kote nchini.

 "Leo tumeanza simulizi mpya ya safari yetu ya mwaka mmoja, safari yenye hadithi ya mafanikio mengi, tumezindua kadi ya Visa, ambayo itaruhusu wateja wetu, kupata huduma za kifedha katika benki yoyote mahali walipo"

Akizindua huduma hizo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai, Mkuu wa Wilaya ya Siha, Thomas Apson amesema  benki hiyo kwa sasa inakwenda vizuri na imeonyesha mabadiliko makubwa katika kipindi cha mwaka mmoja.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya KCBL, Dk Gervas Machimu amesema walianza na hasara ya Sh600 milioni na ndani ya robo tatu ya mwaka huu, wameweza kutoka kwenye hasara na kupata faida ya Sh20milioni.

Kwa upande wake Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika Mkoa wa Kilimanjaro, Jackline Senzige amevitaka vyama vya Ushirika nchini kuwekeza hisa kwenye benki hiyo ili wanufaike na gawio.

Imeandikwa na Ombeni Daniel