Kelele zinavyoweza kusababisha vifo

Muktasari:

  • Wakati takwimu zikionyesha watoto takribani 12,000 hufariki dunia kila mwaka kutokana na kelele duniani, wataalamu wa masikio, pua na koo nchini wamesema tatizo la usikivu ni kubwa na limeathiri mpaka watu wazima.

  


Dar es Salaam. Wakati takwimu zikionyesha watoto takribani 12,000 hufariki dunia kila mwaka kutokana na kelele duniani, wataalamu wa masikio, pua na koo nchini wamesema tatizo la usikivu ni kubwa na limeathiri mpaka watu wazima.

Hivyo wameishauri Serikali kuangalia namna ya kutumia sensa ya watu na makazi kukusanya taarifa za hali ya usikivu kwa kuwa wapo watoto waliopata uziwi baada ya kusikia kelele na watu wazima waliopoteza uwezo wa kusikia kutokana na kelele za kimazingira na zile zilizosababishwa na matumizi ya spika za masikioni.

Akizungumza juzi katika warsha iliyowakutanisha Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na viongozi wa dini mkoa wa Dar es Salaam, Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Amos Kiyunge alisema kelele zina athari kubwa kwa watoto.

Alisema Shirika la Afya Duniani (WHO) limebainisha kelele ni mojawapo ya vitu hatarishi katika maisha ya binadamu, na kwa mujibu wa European Environment Agency (EEA, 2018) kelele zimeainishwa kuwa mojawapo ya vifo vya mapema vya watoto, kwani takwimu zinaonyesha takribani watoto 12,000 hufariki dunia.

Pia alibainisha utafiti uliofanywa mwaka 2019 na Chuo Kikuu cha Tiba Muhimbili (MUHAS) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) katika viwanda vya nguo vilivyopo Dar es Salaam ulionyesha kati ya wafanyakazi 265 waliofanyiwa utafiti, asilimia 58 wamepoteza usikivu.

Aliongeza kuwa utafiti uliofanywa na kampuni ya African Baricks Gold mwaka 2015 ulionyesha asilimia 47 ya wafanyakazi migodini (246) wamepoteza usikivu kutokana na kelele zilizopita viwango.

“Wafanyakazi walioshiriki utafiti wana umri kati 24 na 29 ambao hufanya kazi kwa kutumia mitambo chini ya ardhi...kwa hivyo mtaona ni jinsi gani kelele zinavyoleta athari, na hii sio kwa binadamu tu, hata wanyama na ndege,” alisema Kiyunge.

Alitaja athari za kelele na mitetemo kuwa ni upungufu wa uwezo wa kusikia, uziwi, upungufu wa uwezo wa kuzaa, huharibu uwezo wa kujifunza, husababisha utoro, kuongezeka matumizi ya dawa ya kujitibu kutokana na kusahau, husababisha ajali pamoja mabadiliko ya tabia.

Awali akifungua warsha hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla aliitaka Idara ya Mipango Miji kufanya kazi karibu na viongozi wa dini, ili kuwapanga na kupunguza adha ya kelele.

Alisema katika ziara yake aliyoifanya katika majimbo 10 amepokea kero 927, ambapo 345 ni za ardhi, zikifuatiwa na miundombinu, mirathi pamoja na kelele.

Aliongeza malalamiko yaliyohusu kelele ni 85 na kati ya hayo, 65 ni kumbi za starehe na 20 yalihusisha nyumba za ibada.

“Jana (juzi) niliagiza operesheni ifanyike kwa baa na kumbi za starehe maana zimekuwa kero, ila kwa nyie tumeamua kutumia njia nzuri kuwaita hapa kwa sababu viongozi wa dini ni watu mnaoheshimika. Kwa hiyo baada ya mawasilisho yote mjitafakari tulipojenga makanisa au msikiti ni sehemu sahihi? Na nini kifanyike?

“Pia elimu lazima iendelee kutolewa, mamlaka za Serikali katika halmashauri, hasa idara ya mipango miji inatakiwa ifanye kazi karibu na jamii, ili kuwapanga vizuri lakini pia sheria na taratibu zilizowekwa ziendelee kufuatwa,” alisema Makalla.

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Samwel Gwamaka alisema, “Tunaamini baada ya warsha hii mtatusaidia kuelimisha jamii kuhusiana na athari za kelele na mitetemo. Pia matumizi ya sound proof ni muhimu.”

Daktari bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya masikio, pua na koo kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Godlove Mfuko alisema mara nyingi baadhi ya watoto huzaliwa wazima, lakini hupata tatizo hilo kutokana na mazingira waliyoyakuta.

“Tatizo kubwa nchi yetu hakuna utafiti ambao umeangalia kama kelele zinaweza kuleta kifo kwa mtoto au kufuatilia vifo vilivyosababishwa na kelele, bali nyingi ziliangalia sababu zinazosababisha kuzaliwa na uziwi au kupata uziwi baada ya kuzaliwa.

“UDOM, Muhimbili wamewahi kufanya utafiti ambao uliangalia sababu ya mtoto kuzaliwa akiwa na uziwi, ulifanyika huo pekee tena kwa watoto wachache. Sisi madaktari wa masikio, pua na koo nchini tunaishauri Serikali waingize hili suala katika sensa ya watu na makazi, kwani watakuwa na uwezo wa kuwapima watu wote usikivu na kujua wangapi wana shida hiyo,” alisema.


Imeandikwa na Rhoda Kivugo, Tatu Mohammed na Herieth Makwetta