Kenya na Sudan Kusini zagombea ukatibu mkuu wa EAC

Kenya na Sudan Kusini zagombea ukatibu mkuu wa EAC

Muktasari:

  • Wakati mkutano wa Baraza la Mawaziri ukiendelea jijini Arusha, nchi za Kenya na Sudani Kusini zachuana kugombea nafasi ya Katibu Mkuu .

Arusha. Mvutano wa kidiplomasia huenda ukaikumba Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kutokana na nchi mbili wanachama kuwania nafasi ya katibu mkuu wa jumuiya kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Nafasi hiyo inatakiwa kuzibwa baada ya katibu mkuu wa sasa anayetoka Burundi, Balozi Liberat Mfumukeko kumaliza muda wake.

Nchi hizo ni Sudan Kusini ambayo ilijiunga na jumuiya hiyo mwaka 2016, imewasilisha jina la Waziri wa Fedha wa zamani wa nch hiyo, Aggrey Tisa Sabuni na Kenya ambayo bado haijawasilisha jina la mtu ambaye inataka achukue nafasi hiyo ya juu katika Sekretariati ya EAC.

Hata hivyo, wakenya ambao wanatajwa  huenda wakachukua nafasi hiyo ni pamoja na mwanasiasa Ababu Namwamba,Waziri anayeshughulikia Jumuiya ya Afrika Mashariki, Aden Mohamed, Waziri wa Michezo, Amina Mohamed na pia Adams Oloo.

Kwa mujibu wa mkataba ulioanzisha EAC, Rais wa nchi ambayo inatakiwa kuwa na Katibu Mkuu anatakiwa kuteua jina la mtu wa kuchukua nafasi hiyo ambalo hupelekwa kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri kisha kwa Wakuu wa nchi kwa ajili ya kuidhinishwa.

Itakuwa ni mara ya kwanza kwa nchi mbili kupeleka majina kwa wakati mmoja kutokana na kutokuwa na uwazi ni nchi ipi inatakiwa kuwasilisha jina la mtu wa kuchukua nafasi hiyo ikizingatiwa tayari nchi zote tano wanachama zimeshawahi kutoa makatibu wakuu isipokuwa Sudani Kusini.

Mmoja wa maofisa wa EAC ambaye hakupenda aandikwe gazetini ameiambia Mwananchi kuwa kwa sasa EAC inahitaji Katibu Mkuu atakayeikwamua kutoka kwenye mkwamo wa ukata unaotokana na nchi wanachama kutokuchangia kwa wakati ada na pia mtu atakayewezesha wadau wa maendeleo kuongeza ufadhili wao.

"Tunapaswa kupata mtu sahihi na sio kuangalia ni zamu ya nchi ipi, tuangalie tumekwama wapi na nani anafaa kuwa Katibu Mkuu anayefahamu changamoto zinazotukabili kwa kushirikiana na viongozi wengine waipeleke mbele jumuiya yetu," aliongeza.  

Katika mkutano wa baraza la mawaziri unaoendelea makao makuu ya EAC jijini hapa ulitanguliwa kwa vikao vya maofisa waandamizi na makatibu wakuu  ambao pamoja na mambo mengine ndio hupanga ajenda za mkutano wa wakuu wa nchi za EAC unaotarajiwa kufanyika Februari 27, mwaka huu.

Katika mkutano wa mawaziri miongoni mwa ajenda zitakazojadiliwa ni pamoja na kupitisha taarifa za maamuzi mbalimbali ya vikao vilivyopita, Ofisi ya Katibu Mkuu wa EAC, idara ya mipango na  miundombinu na sekta za jamii.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na ofisa habari mwandamizi wa Sekretariati ya EAC, Simon Owaka ilisema pia baraza hilo litajadili ajenda ya hali ya kisiasa, forodha na biashara, fedha na utawala pamoja na taarifa zinazohusu mihimili ya EAC ambayo ni Bunge la Afrika Mashariki (EALA) na mahakama ya Afrika mashariki (EACJ).

"Baraza pia hupitisha ajenda na programu zilizopendekezwa kwa ajili ya mkutano wa 21 wa marais wa nchi wanachama wa EAC unaotarajiwa kufanyika siku ya jumamosi , Februari 27,2021. Baraza la Mawaziri ni mhimili wa kutunga sera za jumuiya ukihusisha mawaziri wanaohusika na EAC kutoka nchi wanachama," alisema Owaka,

Katika mkutano wa marais wa EAC, jina la Katibu Mkuu mpya anayechukua nafasi ya Balozi Liberat Mfumukeko litatangazwa.


Makatibu wakuu waliotangulia na nchi zao kwenye mabano ni Balozi Fransis Muthaura(Kenya) aliyeongoza Machi 1996 hadi Machi 2001 na Amanya Mushega(Uganda) April 2001 hadi April 2006.

Katibu Mkuu aliyefuata ni Balozi Juma Mwapachu(Tanzania) April 2006 hadi April 2011, Dk Richard Sezibera (Rwanda) April 2011 hadi Aprili 2016 huku Katibu Mkuu anayemaliza muda wake, Balozi Liberat Mfumukeko (Burundi) akikamata wadhifa huo kuanzia Aprili 2016 hadi Aprili 2021.

Chanzo cha uhakika kimesema kutokana na Sudani Kusini kutokuchangia ada yake kwa wakati ikiwa na malimbikizo ya zaidi ya Dola30 milioni pamoja na migogoro ya kisiasa ya ndani ya nchi hiyo huenda ikawa kikwazo kwao kuchukua nafasi hiyo.